Nay wa Mitego arudia alichokatazwa na mama yake

Thursday January 07 2021
NEY PIC
By Kelvin Kagambo

JUNI 11 mwaka jana msanii wa muziki wa kizazi kipya, Emmanuel Elibariki maarufu Nay wa Mitego aliachia wimbo wake unaoitwa Mungu Yuko Wapi ambao ulipata mchanganyiko wa mapokeo ikiwemo ya kupingwa na baadhi ya mashabiki kwa kile kinachotajwa kuwa mashairi yake yalikuwa yakikosoa uwepo wa Mungu.

Moto zaidi kuhusu wimbo huo ulipamba baada ya Nay kuachia video yake ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa imetawaliwa na picha zenye mahadhi ya kutisha (horror) mfano picha zinazoonyesha watu wananyongwa na hata uhariri wa rangi wa video hiyo ulifanywa kwa namna ya ambayo filamu nyingi za kutisha hufanya, mtindo wa kiza.

Video hiyo ilileta utata sio tu kwa mashabiki wake bali mpaka kwa mama yake Nay wa Mitego ambaye aliibuka na kudai kuwa video hiyo imemchukiza na kumtaka mwanaye aifute haraka, hata hivyo Nay hakuifuta licha ya kwamba alikiri kupewa maoni hayo na mama yake.

"Bimkubwa anasema nifute video ya Mungu Yuko Wapi hajanipa sababu kasema tu nifute." aliandika Nay kwenye Instagram.

Sasa leo, Januari 7, Nay wa Mitego ameachia video ya wimbo wake mpya unaoitwa 'Go Baba' ambayo inafanana kwa kiasi kikubwa na video ya Mungu Yuko Wapi.

Baadhi ya vipande katika video hiyo mpya iliyoongozwa na muongozaji Joowzey kutoka Tanzania inaonyesha matendo ya kutisha kama vile Nay kunywa kimiminika kinachofanana na damu, baadhi ya madansa katika video hiyo kupaka rangi za kutisha usoni, uvaaji wa mashuka mekundu na meupe kama kwenye filamu za kutisha lakini pia hata uhariri wa rangi umefanyika kwa aina ile ile iliyofanyika kwenye video ya Mungu yuko wapi.

Advertisement

Video hiyo imejivunia watazamaji elfu 10 ndani ya lisaa limoja tangu kuachiwa kwake katika mtandao wa YouTube. Huku ikiwa imependwa (likes) na watu zaidi ya 1,800, na kutokupendwa (dislike) na watu 26.

Aidha, Go Baba inakuwa ni mradi kazi wa kwanza kwa Nay wa Mitego ndani ya mwaka 2021 na audio yake imetengenezwa na muandaaji Mr. T Touch.

Advertisement