Mzee Yussuf kuweka amapiano kwenye taarabu, azitaja tuzo za Grammy
Muktasari:
- Mzee ameyasema hayo, katika mahojiano maalum na Mwananchi, kuhusu anavyouona muziki huo wa taarabu ulipo kwa sasa na nini mikakati yake katika kuhakikisha unaenda mbele na watu kuupenda kama ilivyokuwa zamani.
Kutokana na soko la muziki Bongo kwa sasa kuzitaka nyimbo za amapiano, mwimbaji wa taarabu, Mzee Yussuf, amesema anafikiria kuweka vionjo hivyo kwenye nyimbo zake zinazokuja.
Mzee ameyasema hayo, katika mahojiano maalum na Mwananchi, kuhusu anavyouona muziki huo wa taarabu ulipo kwa sasa na nini mikakati yake katika kuhakikisha unaenda mbele na watu kuupenda kama ilivyokuwa zamani.
Akilizungumzia hilo, amesema kwa sasa anaona muziki upepo umekuwa kwenye ladha ya amapiano, hivyo kama mdau mkubwa wa muziki wa taarabu anaona na wao wana haja ya kubadilika kulingana na wakati.
“Watu tunaona wanapenda amapiano, sasa kama soko lipo huko kwa nini tusiguse kidogo ambapo nyimbo zangu nitaingiza ladha haiyo kwa mbali, naamini watazipenda,”amesema Mzee.
Akizungumzia kuhusu tuzo za Grammy zilizotolewa hivi karibuni na nafasi ya taarabu katika tuzo hizo, Mzee amesema inawezekana kupeleka muziki huo huku akitaja mambo matatu ya kuyafanyia kazi.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kufupisha urefu wa nyimbo zao, kurekodi video ambazo zitaendana na matakwa ya waandaaji wa tuzo hizo.
Jambo la tatu amesema kumekuwa na mfumo mmoja katika kucheza nyimbo hizo na kuonekana hakuna jipya wala ubunifu katika muziki huo ambapo alitaka watu wabadilike.
Katika hatua nyingine Mzee amezungumzia kuhusu maonyesho yake atakayoyafanya katika mikoa mitano ndani ya Desemba.
Maonyesho hayo amesema yamelenga kujipa maua yake katika mchango alionayo kwenye muziki wa taarabu na yatafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, Songea na Mwanza.
“Nimeona nisisubiri watu wanipe maua yangu, kwa kuwa ukweli ni kwamba hata watu wasiposema najua mchango wangu katika muziki wa taarabu na wala sijataka nife ndio watu waanze kunisifia,”amesema Mzee.
Amewataja wasanii watakaoshiriki maonyesho hayo kuwa ni pamoja na Khadija Kopa, Mosi Suleiman, Fatma Mcharuko na Joha Kasim.
Wengine ni Isha Mashauzi, Leila Rashid, Hadija Yusuf na bendi ya Nakshi Nakshi Modern Taarab.
Ikumbukwe mwaka 2016, Mzee Yusufu alitangaza kuacha kuimba taarabu na kuomba nyimbo zake zisipigwe kokote, lakini ilipofika Julai alitangaza kurejea tena katika muziki huo, na tayari ameshatoa nyimbo mbalimbali.
Kati ya nyimbo hizo ni pamoja na Najiripua, Full Dozi , Udugu Mtamu, Sina Wema na Wema.