Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwigizaji wa tamthilia ya Mpali afariki dunia

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Televesheni ya Taifa ya Zambia, Wanga Zulu aliyeigiza katika tamthilia ya Mpali akitumia jina la Mai Guru, amefariki dunia Alhamisi Oktoba 9, 2025 katika Hospitali ya Mafunzo ya Levy Mwanawasa baada ya kuugua.

Muigizaji kwenye tamthilia ya Mpali ya nchini Zambia aitwaye Wanga Zulu maarufu kwa jina la Junza, aliyekuwa akiigiza kama mke mkubwa wa Nguzu, amefariki dunia.

Kwa mujibu wa Televesheni ya Taifa ya Zambia, Wanga Zulu aliyeigiza katika tamthilia ya Mpali akitumia jina la Mai Guru, amefariki dunia Alhamisi Oktoba 9, 2025 katika Hospitali ya Mafunzo ya Levy Mwanawasa baada ya kuugua.

Wanga ambaye kwenye tamthilia ya Mpali aliigiza kama mke mkubwa wa Nguzu mwenye wake saba, pia alifahamika kama mama wa Hambe, mtoto wa kiume aliyelelewa na Nguzu.

Nguzu ambaye ameigiza kama mumewe kwenye tamthilia hiyo, ameelezea kifo chake kama pigo binafsi na taaluma ya uigizaji, akikumbuka jinsi yeye ndiye aliyemuhimiza kujiunga na Mpali.

Naye mtayarishaji wa Mpali, Frank Sibbuku amemtaja Wanga kama kitovu cha onyesho hilo, uwepo wa kupendwa ambaye ari yake isiyo na kifani na mapenzi yake yalimtia moyo kila mtu aliyehudhuria.

Wanga, ambaye aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 51, ameacha mume anayefahamika kwa jina la Daniel Mutale, na watoto wao watano.

Taarifa kutoka Zambia, zinabainisha kwamba, siku kumi kabla ya kifo chake, alipatwa na kiharusi cha sehemu ya mwili (partial stroke).

Mwigizaji huyo, mwaka 2014 alibainika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi, lakini matibabu aliyoyapata, alipona tatizo hilo.

Wakati wa uhai wake, alifanya mahojiano na Janet Chinyama, aliyekuwa Afisa Mawasiliano wa CIDRZ (kwa ushirikiano na CDC), ambapo Wanga Zulu alisimulia safari yake ya mapambano na ugonjwa huo.

"Nilipogundua nina saratani ya shingo ya kizazi mwaka 2014, ilikuwa safari yenye maumivu makubwa ambayo sitamani mwanamke mwingine aipitie. Nilikuwa nasikia kuhusu upimaji lakini nilikuwa siutii.

Nilipoanza kupata ute wa ajabu na wenye harufu mbaya, nilitembelea kliniki kadhaa lakini nilikuwa nikipatiwa dawa tu. Baadaye, mkwe wangu ambaye ni mtaalamu wa maabara alinisisitiza niende kupimwa saratani ya shingo ya kizazi. Nilipofanyiwa uchunguzi, waligundua uvimbe mkubwa uliokuwa umefunika uke wangu, na nikapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Taifa (UTH). Baada ya vipimo, majibu yalionyesha nilikuwa na saratani ya shingo ya kizazi.

"Nilihisi kama ni mwisho wa maisha yangu. Nililia nikifikiria watoto wangu, hasa wa mwisho ambaye wakati huo alikuwa na miaka saba. Nilijiuliza, “nitamwacha na nani?” Lakini madaktari walinipa matumaini wakaniambia bado inawezekana kutibiwa kwa kuwa ilikuwa katika hatua ya pili (2B).

"Wauguzi na madaktari walikuwa wazuri, lakini changamoto kubwa zilikuwa mashine zinazovunjika mara kwa mara. Nililazimika kusitisha matibabu kwa wiki kadhaa hadi mashine zitengenezwe. Hata hivyo, nilijitahidi kumaliza tiba yangu.

"Familia yangu ndiyo nguzo yangu. Nilimwambia rafiki yangu wa karibu, mwigizaji Anne Katamanda, tu. Mtoto wangu wa pili ndiye aliyekuwa akinifuata hospitalini kila siku. Leo hii, yeye ni muuguzi, aliwahamasishwa na changamoto nilizopitia.

“Ninapenda kuona dunia isiyo na saratani. Sitamani mtu mwingine apitie maumivu niliyoyapitia. Saratani ni ugonjwa hatari unaoendelea kimyakimya hadi unapoenea mwilini. Nawaomba wanawake wote, tafadhali nendeni mkapimwe. Usingoje mpaka iwe imechelewa. Nilijutia kupuuza uchunguzi mapema, msifanye kosa kama langu.”