Mwana FA awatolea uvivu Basata sakata la ukaguzi wa nyimbo za wasanii

Mwana FA awatolea uvivu Basata sakata la ukaguzi wa nyimbo za wasanii

Muktasari:

  • Mbunge wa Muheza (CCM), Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA amelitaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kutafuta utaratibu mwingine wa kuzihakiki nyimbo za wasanii wanaodaiwa kutumia lugha chafu katika tungo zao.

Dar es Salaam. Mbunge wa Muheza (CCM), Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA amelitaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kutafuta utaratibu mwingine wa kuzihakiki nyimbo za wasanii wanaodaiwa kutumia lugha chafu katika tungo zao.

Mwana FA ambaye pia ni mwanamuziki wa Bongofleva ameeleza hayo jana Jumanne  Mei 4, 2021 kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram na kuungwa mkono na wasanii wenzake, wakitaka baraza hilo kujiweka sawa kwa kuwa utaratibu huo utawabana wasanii wengi na hauna mashiko.

“Naomba niandike kuhusu hili la huu utaratibu mpya wa Basata. Binafsi sikubaliani nao na nitalipinga kwa nguvu nyingi. Sidhani kama sheria hii inafaa hata kuwepo achia mbali kutumika. Haina tija yoyote, hamsaidii msanii kwa namna yoyote ni ya kidwanzi.”

“Inatakiwa kurekebishwa kama sio kuondolewa kabisa. Tutafute namna nyingine za ku’censor sanaa matusi yasisikike kwa kadri inavyowezekana na sio kwa utaratibu huu dhaifu na wa kikandamizaji. Siungi mkono nyimbo “chafu” lakini kutengeneza urasimu usio na msingi kwa kisingizio cha kuwepo kwa nyimbo zisizofaa ni jaribio la kuzorotesha tu sanaa,” amesema Mwana FA..

Amesema kama Basata na Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota) wanataka kutekeleza kila sheria inayowahusu wangeanza na sheria namba 7 ya mwaka 1999 inayowapa Cosota haki ya kutoa leseni kwa maeneo ya hadhara yanayotumia kazi za sanaa na  kukusanya mirahaba.

Amesema hizo ndio sheria zitakazomsaidia msanii lakini wamezifumbia macho kwa miaka mingi na wasanii wanaendelea kupoteza fedha nyingi.

“Bahati nzuri tuna waziri mkuu na katibu mkuu wasikivu, tutalisemea kwa namna nyingi na tunaamini kero hii itaondolewa haraka. Msifanye kutoa wimbo iwe kama kuomba hati ya kusafiria au Viza mnaonea wasanii, tunakwamisha sanaa,” amesema.

Mbunge huyo amesema jambo linalofanywa na Basata huwapa kazi kubwa kuwaeleza watu hasa mashabiki wa sanaa kuhusu kazi za baraza hilo pale yanapoibuka madai kuwa lipo kwa ajili ya kuwafungia na kuwafungulia wasanii.

“Kuweka kumbukumbu sawa, jambo hili liliwahi kuja kwa majadiliano kwenye bodi ya Basata wakati nikiwa nahudumu kama mjumbe wa bodi, nililipinga sana wakati ule kama ninavyoendelea kulipinga sasa,” amesisitiza.

Baada ya kueleza hayo, wasanii mbalimbali wa Bongofleva walimuunga mkono Mwana FA akiwemo Gnako aliyeandika, “hili bangoo limenyooka nadhani inabidi liwe reposting kwa kila anayesoma.”

Naye Ambwene Yesaya maarufu AY ameandika, “Basata wanakagua nyimbo za Tanzania peke yake tu na kuruhusu nyingine za nje ya Bongo zipigwe hewani au? Kutoa wimbo kama unaomba Viza ya North Korea bwana sio sahihi na si haki, njia mbadala zipo nyingi tu.”

Msanii mwingine Mrishompoto ameandika, “nilikuwa naangalia pakuongezea kwenye waraka huu nimekosa..., nawasalimu kwa jina la Jamuhuri ya Muungano..., FA sijapigia kura Muheza lakini nimekichagua.”