Mwaitege, Nkone kunogesha tamasha la kumshukuru Mungu

Sunday September 05 2021
msama pic
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Waimbaji wa muziki wa injili  Upendo Nkone, Bonny Mwaitege na Christopher Mwahangila wanatarajiwa kuwepo kwenye orodha ya wasanii watakaopamba tamasha la kumshukuru Mungu.

Tamasha hilo lililoandaliwa na kampuni ya Msama Promotion litafanyika Oktoba 31 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama amesema bado wanaendelea kuchambua  orodha ya waimbaji  kutoka katika idadi kubwa inayopendekezwa na mashabiki wa tamasha hilo.

msama pic 1

Akizungumza leo Msama amesema tamasha hilo litakua la kumshukuru Mungu kwa namna ambavyo amelivusha salama Taifa la Tanzania katika mambo magumu ambayo imepitia.

"Tamasha hili litakua la kihistoria kwa sababu hatujafanya takribani miaka sita, niwaambie mashabiki wote waliomiss matamasha yetu kuwa tunarejea kwa nguvu kubwa na tutahakikisha kila ambaye atalipa kiingilio chake atapata burudani ya kutosha.

Advertisement

Kutakua na wasanii tofauti tofauti, wa ndani ya Nchi na wa nje ya Nchi, tutaalika waimbaji wazuri kutoka mataifa mbalimbali, lengo ni kuhakikisha kila mmoja anafurahia tamasha letu," amesema Msama.

Mratibu wa tamasha hilo Emmanuel Mbatila amesema, “Maandalizi yanayoendelea kufanyika yanadhihirisha kuwa tamasha hilo litakuwa kubwa kuliko yaliyopita na litagusa hisia za wengi. Waimbaji wameshaingia kambini kujifua kwa ajili ya siku hiyo muhimu,”

Advertisement