Muziki wa Mwana FA na fedha ni damdam!

Muktasari:
- Msanii huyo wa Bongofleva ametoa albamu, ameshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) na sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akiwa ni mwanamuziki wa kwanza nchini kushika wadhifa huo. Fahamu zaidi.
KWA sasa MwanaFA ana miaka zaidi ya 20 ndani ya Bongofleva tangu alipotoka 2002, lakini alikuwepo kwenye gemu tangu 1996 aliposhika nafasi ya tatu kwenye mashindano ya kuchana huko Tanga.
Msanii huyo wa Bongofleva ametoa albamu, ameshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) na sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akiwa ni mwanamuziki wa kwanza nchini kushika wadhifa huo. Fahamu zaidi.
1. Akiwa bado hajatoka kimuziki, P-Funk Majani alimgomea Mwana FA kuingiza vesi katika wimbo wa rapa wa HBC, Profesa Jay 'Na Bado' unaopatikana kwenye albamu yake ya kwanza Machozi, Jasho na Damu (2001).
2. Kipindi hicho Profesa Jay alikuwa anafanya kazi Tanga alipomuagiza Mwana FA kwa Majani pale Bongo Records, alijibiwa kuwa Profesa Jay na Imamu Abbas walishaingiza vesi, hivyo akiongeza na yake wimbo utakuwa mrefu sana. Hata hivyo, vesi hiyo Mwana FA alikuja kuiweka kwenye ngoma 'Hii Leo' ambayo ilirekodiwa kwa Master J, mwanzilishi wa MJ Production 1996 ambayo sasa inajulikana kama MJ Records.
3. Februari 2, 2002 ndio siku ya kwanza kwa wimbo wa kwanza wa Mwana FA kusikika redioni. Wimbo huo unaitwa 'Ingekuwa Vipi' ambao amemshirikisha Jay Moe na ulirekodiwa na DJ Bonny Luv ambaye alimsubiri kwa miezi 18 arudi kutoka Uingereza.
4. Jina la Mwanafalsafa (Mwana FA) alipewa na DJ Bonny Luv baada ya kurekodi wimbo uitwao 'Mwanafalsafa'. Katika muktadha huo DJ Bonny Luv akatoa pia jina la albamu ya kwanza ya Mwana FA ambayo ni Mwanafalsafani (2002).
5. Kwa ujumla hadi sasa Mwana FA ametoa albamu tatu, Mwanafalsafani (2002), Toleo Lijalo (2003) na Habari Ndio Hiyo (2008) akiwa na AY na wimbo uliobeba jina la albamu hiyo ulishinda TMA kama Wimbo Bora wa Kushirikiana 2008.
6. Kipande anachoimba Linah katika wimbo wa Mwana FA, Yalaiti (2011) ni kutoka katika wimbo wa Siti Binti Saad wa Zanzibar unaokwenda kwa jina hilo hilo ambao pia Bi Kidude naye aliurudia. Hata hivyo, Mwana FA aliamua kuurudia wimbo huo baada ya kusikia toleo la Malika wa Mombasa, Kenya na kukoshwa nalo hadi kufikia hatua ya kumpa mtoto wake wa kwanza jina la Malika.
7. Lady Jaydee ndiye mwanamuziki wa kike Bongo ambaye ameshirikiana sana na Mwana FA. Wawili hao wametoa nyimbo kama Sitoamka (2002), Wanaume kama Mabinti (2003), Alikufa kwa Ngoma (2004), Hawajui (2005), Msiache Kuongea (2009) na kadhalika.
8. Wimbo wa Mwana FA wa Binamu ndio ulimtambulisha Marco Chali katika Bongofleva kama mtayarishaji muziki na kipindi hicho Marco alikuwa anafanya kazi 'Kama Kawa Records' ndipo baadaye akapata nafasi MJ Records. Hata hivyo, Mwana FA, mwanachama wa zamani wa kundi la East Coast Team tayari alikuwa alisharekodi wimbo huo miaka mingi nyuma na ulikuwepo katika albamu yake ya pili, Toleo Lijalo (2003).
9. Neno 'Fedha' limetamkwa sana kwenye nyimbo za Mwana FA. Fedha imetajwa kwenye nyimbo zake zaidi ya 10 baadhi ya nyimbo hizo ni Binamu (2003), Nazeeka (2009), Msiache Kuongea (2009) na Unanijua Unanisikia (2011). Nyimbo nyingine ni Unanijua Unanisikia (2011), Mfalme (2014), Kiboko Yangu (2014), Asanteni kwa Kuja (2016), Upo Hapo? (2017), We Endelea Tu (2018), Sio Kwa Ubaya (2022) na kadhalika.
10. Baada ya kumaliza kurekodi wimbo wake, So Crazy (2013), Maua Sama kupitia rafiki yake aliwatumia wasanii kama Alikiba, Ommy Dimpoz na Ben Pol ila ni Mwana FA pekee aliouelewa ndipo wakarudia kuurekodi na alipotoka ukamtambulisha Maua Sama. Ikumbukwe tayari Maua Sama alikuwa amesharekodi wimbo huo huko nyumbani kwao Moshi, ila alipotua Dar es Salaam na kukutana na Mwana FA waliamua kwenda kuurudia kwa Marco Chali, mshindi wa TMA kama Mtayarishaji Bora 2008.