Msanii wa Bongo Fleva Spack, afariki dunia
Muktasari:
- Spack alijipatia umaarufu mkubwa kupitia kundi la Tip Top Connection, pamoja na nyimbo ya Nipe Ripoti aliyoshikiana na Tundaman.
Msanii wa Bongo Fleva, Selemani Mvamba maarufu kama Spack, amefariki dunia leo Aprili 27, 2026 nyumbani kwake Chanika jijini Dar es Salaam.
Spack alijipatia umaarufu mkubwa kupitia kundi la Tip Top Connection, pamoja na nyimbo ya Nipe Ripoti aliyoshikiana na Tundaman.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Aprili 27, 2026, Meneja wa msanii huyo Abdulrahman Hassan maarufu Malefti amesema jana alizungumza na msanii huyo kuhusu mpango wao wa ‘kushoot’ video ya wimbo mpya.
"Ni kweli amefariki mara ya mwisho nimezungumza nae saa saba usiku. Akaaga akaenda kulala sasa asubuhi alienda kugongewa kwa ajili ya kutoa nauli za watoto kwenda shule akawa haamki,”
“Jana tulivyozungumza alikuwa mzima alinitumia wimbo akasema niusikilize kwa sababu leo tulikuwa tunaenda Sinza kukutana na director Lenzo kwa ajili ya kuandika script za video ya wimbo wake mpya," amesema meneja.
Meneja huyo amesema baada ya yaliyotokea majirani walimpeleka hospitali ya Nguvu Kazi iliyopo Chanika ndipo daktari alithibitisha kuwa msanii huyo amefariki dunia.