Msafiri Diouf watoto tisa kila mmoja na mama’ake

UTASEMA nini kuhusu kipaji kikubwa alichonacho katika kuimba na kughani. Anabebwa na sauti yenye kuitika kila eneo. Anajua kupangilia mistari na anajua kuchizisha mashabiki.

Huyu ni Msafiri Diouf ‘Sokoine’, mmoja wa nyota wa muziki wa dansi nchini aliyeamua kujivua gamba Twanga Pepeta akiwa na wenzake na kwenda kuunda kundi jipya la VDS Chama la Wana na mwenyewe amefichua kilichomkimbiza ni kuchoshwa kufanya kazi za wengine akiwa na maisha yaleyale.

Diouf anasema ana wiki moja tangu aachane na bendi hiyo na kuanzisha kundi hilo jipya baada ya kuona anahitaji kujiongoza na kubadilisha upepo wa safari ya maisha binafsi na muziki kwa jumla, huku akifunguka mambo mbalimbali alipofanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti.

Katika mahojiano hayo, Msafiri amefichua ana watoto tisa ambao kila mmoja ana mama’ake, huku akiweka bayana anavyopambana nao kuwajengea maisha ya kesho kupitia sanaa hiyo ya muziki. Endelea naye.


CHANZO KUSEPA TWANGA
Kuna taarifa zilizozuka kuwa Diouf na wenzake wamefukuzwa kwenye bendi Twanga Pepeta aliyodumu nayo muda mrefu, lakini mwenyewe anasema ameondoka na kupata baraka zote kutoka kwa mkurugenzi wao, Asha Baraka.

Ilivyokuwa: Diouf alifanya kosa baada ya kwenda kupiga shoo na wanamuziki wa Twanga siku ambayo bendi hiyo haikuwa kazini, huku wakitumia jina la bendi hiyo.

Baada ya hapo, uongozi uliwasimamisha lakini baadaye ukawarudisha na yeye pamoja na Victor Nkambi hawakutaka kurudi kazini na siyo kwamba walifukuzwa kama watu wanavyodhani.

Anasema yeye na Asha hawana tatizo na hata alivyokwenda Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) hivi karibuni kusajili Bendi yake ya VDS Chama la Wana, alikutana naye na kuwapa ushauri wa jinsi ya kujiongoza ili waifikishe sehemu nzuri bendi yao.

“Mimi nimetoka Twanga kwa hiyari yangu tangu wiki iliyopita. Sijafukuzwa kama baadhi ya watu wanavyosema, nimeona nimekua nahitaji kujiongoza na wala sina ugomvi na mwanamuziki yeyote wa Twanga Pepeta wala Asha Baraka, kwani kwenye kuanzisha bendi hii mimi na Victor Nkambi, Asha ametupa baraka zote," anasema Diouf.

“Na tumeanzisha bendi hii sio kwa lengo la  kushindana na Twanga Pepeta kwani bendi yetu ya VDS Chama la Wana katika asilimia 100 ndio kwanza tuna asilimia 15 yaani bado sana kusimama kama bendi zingine.”


MIPANGO CHAMA LA WANA
Diouf anasema kwa sasa bendi hiyo inafanya utaratibu wa kuingia mazoezini kwani wameanza kufanya shoo jukwaani bila ya kufanya mazoezi.

Anasema wana mpango pia wa kuingia studio kwa kuwa hadi sasa tayari wana nyimbo mbili na nyingine wanaendelea kutunga na pia wanatafuta kuongeza watu wawili kwenye safu ya uimbaji na rapa mmoja kwani yeye kwa sasa sio rapa, bali ni muimbaji.

Diouf anadai mambo ya kurapu amewaachia vijana wapya kwenye muziki wenye kupenda kufanya rap katika bendi


VDS INA MAANA GANI
VDS ni vifupi vya majina ya wamiliki wa benchi hiyo, Victor Nkambi, Msafiri Diouf na Stella Manyanya ambao wote wametokea Twanga Pepeta.

Nkambi alikuwa mpiga kinanda wa muda mrefu wa bendi hiyo, huku Stella akiwa mcheza shoo machachari na umoja huo kiongozi mkuu ni Diouf akisaidiwa na Victor, na anasema Stella hapo baadaye atakuja na saprazi ambayo haijawahi kutokea katika dansi.

Akizungumzia maana ya Chama la Wana, Diouf anasema maana yake ni kwamba hawachagui mashabiki kila shabiki ni mwana wao.


VYOMBO VYA BENDI
Kuhusu vyombo vya bendi, Diouf anasema hawana bosi, ila mabosi ni wao wenyewe hivyo bado hawajanunua vyombo vya muziki na kwa sasa wanakodi kama zinavyofanya baadhi ya bendi nyingi hapa nchini.

“Niseme tu ukweli sisi VDC Chama la Wana hatuna bosi. Mabosi ni sisi wenyewe hivyo tukipata kazi ya shoo tunakodi vyombo vya muziki na kwenda kufanyia kazi, kwa maana ya kwamba pesa tunayolipwa ya kazi tunakodi vyombo na kugawana posho inayobaki tunaipeleka benki maana tushafungua akaunti ya bendi,” anasema Diouf.



Diouf anasema muziki wa dansi sio kama umeshuka kama baadhi ya watu wanavyodai, lakini mameneja wa bendi na wanamuziki wanaishi kwa mazoea ndio maana umekuwa haubadiliki wala kufika mbali.

“Ngoja nikwambie ukweli. Huu muziki sio kwamba umeshuka tatizo lipo kwa mameneja wa bendi ndio wanashindwa kujiongeza ama kuboresha huu muziki, wanaishi kwa mazoea," anasema Diouf.

"Nasema hivi nikimaanisha meneja wa bendi anajua tu kazi yake ni kutafuta tu shoo basi. Baada ya hapo asubiri wanamuziki wamalize shoo awalipe posho wanamuziki 30 ama 25 au 20, ndio anajua amemaliza kazi ya umeneja. Kumbe meneja wa bendi inatakiwa utafute mbinu ya kututoa kwenye posho za ishirini.. thelathini elfu na kutupeleka kwenye sabini ama laki kwa kuupeleka muziki mbali zaidi.

"Mimi nikipewa nafasi ya kuongoza muziki Tanzania naanza na mameneja wa bendi kutaka wawe na mfumo wa kutafuta kazi  zenye mafanikio ya pesa. Kuwa na ‘connection’ hadi nje ya nchi kwa ajili ya kupeleka muziki wetu huko kwa wenzetu. Sio kuzoea tu kupiga kwenye baa na kumaliza kazi.”


ALIPOTOKEA
Diouf anasema ameanza kufanya muziki tangu 2003 na alikuwa na uwezo wa kuimba na kurapu na hata kutunga nyimbo.

Kabla ya kujiunga na Twanga Pepeta alifanya kazi na wanamuziki wakongwe Muhidin Gurumo (marehemu) na Ali Choki kwa kutoa Albamu inayoitwa Special Remix.

Anasema Special Remix ndio ilimpeleka bendi ya Tam Tam baada ya kushikwa mkono na mwanamuziki mwenzake aitwaye Msichole Kombo ambaye kwa sasa ni marehemu, huyu ndiye aliyempokea hapa Tanzania akitokea Kenya.

Diouf anasema hakukaa muda mrefu Tam Tam na kujiunga Twanga Pepeta baada ya kuona anafanya vizuri kwenye baadhi ya  nyimbo hasa wimbo wa Usia wa Baba uliopo kwenye Albamu ya Spicail Remix.


DAWA ZA KULEVYA
Diouf anasema hataki kuzungumzia hilo kwani anajuta kutumia na anaumia sana akikumbuka.

“Jua mimi Msafiri Diouf sitaki kuzungumzia habari za nyuma hasa kipindi natumia dawa hizo za kulevya. Hayo yalishapita na sababu kubwa ya kusema ‘no comment’ najutia kwa kitendo  cha kutumia dawa za kulevya na nimeshaachana nao sababu hakuna faida yoyote niliyoipata zaidi ya kushusha kipaji changu na kudhalilika.”

Anasema kwa sasa hatumii sigara wala bangi zaidi ya kunywa pombe tena baada ya kumaliza kazi na wala sio kwamba anaiendekeza, bali anakunywa mara chache.

Pia anawashauri watu wanaotumia dawa hizo waache na ambao  hawajaingia wasithubutu kuingia kwenye utumiaji kwa sababu madhara yake ni makubwa.

“Niwashauri tu mtu kama hajawahi kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya, basi asithubutu kuingia ila kama ameshaingia basi aache mara moja kwani ni hatari sana na inakuharibia mwenendo wa maisha yako,” anasema.

Anasema hali ilivyokuwa inazidi kuwa mbaya aliamua kutafuta msaada wa kuepukana na dawa hizo, akatokea mwanamke ambaye alikuwa na mahusiano naye kimapenzi akampeleka Uingereza  kuishi naye ambako alikuwa na afya njema.

Akiwa huko akaachana na huyo mwanamke na kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na mwanamke mwingine hadi aliporudi Tanzania na hadi sasa anasema yupo na huyo mwanamke kwani wanawasiliana.


WATOTO TISA, MAMA TOFAUTI
Anapoulizwa na Mwanaspoti nje ya muziki Diouf ni mtu wa aina gani, mwanamuziki huyo anasema kwa sauti ya kujiamini: “Mimi Diouf ni mtu mmoja mkimya sana na mpole. Napenda kujishusha sana na sipendi ugomvi. Muda mwingi nikiwa mapumziko ya kazi  (off) nashinda nyumbani nalala na kuangalia muziki wa nje kwenye Youtube.”

“Pia nina watoto tisa kwa mama tofauti na katika watoto wangu sitaki hata mmoja arithi kazi hii ya muziki. Nawatengenezea mazingira ya kuona mbali kwenye kazi zingine kwani hii kazi ya muziki ina changanoto nyingi sana japo kila kazi ina changamoto.”

Diouf bila kufafanua watoto hao amezaa na wanawake gani kwani ni mambo yake binafsi, ila anataka jamii ijue ana watoto tisa kwa mama tofauti.


JINA LA SOKOINE
Diouf anasema anapenda kujipa majina ya a.k.a kutokana kutembelea upepo, hivyo jina likivuma sana akilipenda  na kumkubali mtu, basi anajipa a.k.a. ndio maana a.k a zake za majina huwa zinabadilika badilila kila wakati.

Diouf aliyewahi kujipa jina la aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine anasema alikuwa anamkubali
kutokana na utendaji wake wa kazi.

Sasa hivi upepo wa jina umehamia nchini DR Congo ambapo amejipa jina la Diouf Muteba Chilamwina.

Chilamwina ni bosi mmoja wa DR Congo anayesapoti sana muziki wa dansi nchini humo, hivyo anamkubali na kaamua kujiongezea a.k.a nyingine.


FAIDA KATIKA MUZIKI
Mwanamuziki huyo anasema hawezi kuwa muongo kwani vitu kama mali huwa vinajionyesha tu, hivyo anavyo ambavyo binadamu anavihitaji, akiwa na gari na nyumba pamoja na watoto wake anaowasomesha kupitia kazi yake.