Mlimani Orchestra kuadhimisha miaka 45

Bendi ya Mlimani Park Orchestra inatarajia kufanya tamasha lake la kuadhimisha miaka 45 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1976.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa bendi Mipango na Matukio, Hassan Msumari alipozungumza na waandishi wa habari kuelekea tamasha hilo.

Msumari amesema tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Septemba 30 mwaka huu na ndani ya wiki tatu hizo kutakuwa na shughuli mbalimbali zitakazofanyika zikiwemo za kijamii.

"Ukiacha maadhimisho ya miaka 45 katika tamasha hilo, pia tutazindua albamu...," amesema Msumari

Kwa upande wake Kiongozi wa bendi, Habibu Mgalusi amesema wakati wanaenda kutimiza miaka 45 wanapitia changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa bendi na kuwataka wadau kuwa wavumilivu ili kuufanya muziki huu kuendelea kuwepo.

"Wenye kumbi tunaomba  wawe wavumilivu, wasiangalie tu maslahi bali na kuendeleza muziki wa dansi kwani wengi wao hupiga tu disco kwa kuona muziki wa  bendi haurudishi hela yao," amesema Mgalusi

Kuhusu albamu yao wanaoenda kuizindua kuongozi huyo amesema itakuwa ina nyimbo sita na kuzitaja kuwa ni  Maadili, Hasama, Umbea, Roho Mbaya na  Hujafa Haujaumbika wimbo uliyotungwa na mwanamuziki mkongwe Hassan Bichuka.

Naye Hiza Francis ambaye ni Meneja Miradi  Shirika la Masoko Dar es Salaam (DDC) amesema wamefurahi kuungana na bendi yao katika maadhimisho hayo ya miaka 45 na kueleza kuwa  tamasha hilo litafanyika ukumbi wao wa DDC Magomeni  Kondoa  katika eneo ambalo bendi hiyo ndipo iliasisisiwa.