Mitihani itakayomkabili mpenzi mpya wa Harmonize

Saturday January 01 2022
harmo pic
By Peter Akaro

MEI 2016 wakati Harmonize ameanza kupata mafanikio kimuziki baada ya kuachia nyimbo zake mbili, Aiyola na Bado, ziliibuka tetesi kuwa amezama kwenye penzi na Staa wa Bongo Movie, Jacqueline Wolper.

Wolper tayari alikuwa amewahi kuwa na mahusiano na Alikiba na Diamond Platnumz miaka kadhaa nyuma, hilo likatajwa kama lingekuwa kikwazo kwa Harmonize wakati uvumi huo umeanza kushika kasi.

Hata hivyo, walikuja kuwa wapenzi na Juni 2016 Harmonize alimpeleka Wolper nyumbani kwao Tandahimba, Mtwara kwa ajili ya kumtambulisha kwa wazazi wake.

Machi 16, 2017 Harmonize aliachia video ya wimbo wake ‘Niambie’ huku Wolper akitokea kama video vixen, siku kadhaa mbele, Wolper aliiambia Clouds TV kuwa ameachana na Harmonize miezi mitatu iliyopita kabla hata wimbo huo haujatoka ila waliamua kufanya siri kutokana na biashara hiyo ya muziki.

Kuachana kwao kukatoa nafasi kwa Harmonize kuzama katika penzi jipya na mrembo toka Italia, Sarah ambaye baadaye alikuja kupewa tuhuma kuwa ndiye aliyemchukua Harmonize kutoka kwa Wolper kutokana na fedha zake.

Naye Sarah alitambulishwa kwa wazazi wa Harmonize huko Mtwara Machi 2019. Katika mapenzi yao, Sarah ametokea kwenye video mbili za Harmonize, Niteke na My Boo ambao alishirikiana na Q Chief.

Advertisement

Walifunga ndoa ya kimya kimya hapo Septemba 2019 ambapo hakuna mtu yeyote toka WCB Wasafi aliyealikwa jambo lililokoleza tetesi za mwimbaji huyo kuachana na lebo hiyo. Waliachana Desemba 2020, kufikia Februari 2021 Harmonize akaanzisha mahusiano na Kajala Masanja ingawa walidumu kwa kipindi kifupi sana.

Wakati anafikia mwishoni mwa ziara yake ya kimuziki Marekani, Novemba mwaka huu, Harmonize aliweka wazi kuwa yupo katika mahusiano mapya na mrembo toka Australia, Briana.

Novemba 27 mwaka huu Briana aliwasili Tanzania akiwa na Harmonize wakitokea Dubai, moja kwa moja alipelekwa Mtwara ambapo msanii wa Konde Music, Ibraah alikuwa na shoo yake. Briana alionekana jukwaani akiwa na mama mzazi wa Harmonize akifurahi kufika ukweni kwa mara ya kwanza.

Wakati penzi hilo changa linazidi kukua, Briana anakabiliwa na mitihani mitatu katika mahusiano hayo. Je, ipi na kwa namna gani?, makala haya yanaenda kuangazia hilo.


USALITI

Tetesi za usaliti ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakikumba sana mahusiano ya Harmonize kila mara, iwe ni yeye kumsaliti mwenzake au kusalitiwa.

Kipindi yupo na Sarah, Mei 2017 zikaibuka tetesi kuwa amempa ujauzito msanii wa muziki wa Injili toka Kenya, Veronica Wanja ëNicah The Queení, kufuatia kuonekana pamoja nchini humo, lakini hilo baadaye likaonekana halikuwa kweli.

Agosti 2018 ikaibuka kashfa mbaya zaidi kuwa Sarah alichepuka na Mlinzi wa Diamond kwa wakati huo, Mwarabu Fighter, licha ya Sarah kukanusha vikali hilo, Mwarabu alijikuta akifutwa kazi WCB Wasafi.

Kufika Desemba 2020 Sarah alitangaza kuachana na Harmonize kufuatia mwimbaji huyo kuisaliti ndoa yao na kwenda kuzaa nje, Harmonize alikiri hilo ni kweli na hawezi kuikana damu yake.

Briana mrembo asiye na hatia kwa sasa, mwenye picha safi mbele ya mashabiki na mitandao ya kijamii Bongo, ajiandae kukabiliana na sarakasi za mtindo huo. Ni suala la muda tu.


VIJEMBE

Hakuna mahusiano ya Harmonize ambayo yamewahi kukosa drama, hii ni kutokana na uzito wa jina lake, drama hizo mara nyingi hutoka kwa wanawake ambao amewahi kuwa nao penzini kipindi cha nyuma.

Mathalani Mei 2018 Wolper alimvaa mpenzi wa Harmonize kwa wakati huo, Sarah na kuimuita ‘mlezi wa wana’, akiwa na maana kuwa Sarah amekuwa na mahusiano na wanaume wengi kabla ya Harmonize.

Harmonize akajibu mapigo kwa kutaja orodha ya wanaume 11 aliyodai wamewahi kuwa na Wolper, wanaume hao ni Dallas, Mkongo, Diamond, Marco Chali, G Modo, Chid Mapenzi, Konde Boy (yeye mwenyewe), Chazi Baba, Brown, Engene na Jux.


MAADUI

Kwa mujibu wa Harmonize, wale wanaowaita maadui zake kimuziki wamekuwa wakitumia wapenzi wake kwa kuwarubuni kujua mipango yake jambo linalomfanya sasa kuogopa kuwa mahusiano na mwanamke toka Bongo.

Hiyo ni kufuatia penzi lake na Kajala kuisha vibaya hadi kupelekana Polisi kwa madai Kajala kusambaza picha zake za faragha, ikumbukwe ni wakati huo video za Harmonize na Paula (mtoto wa Kajala) ambaye ni mpenzi wa Rayvanny sasa zilivuja.

Advertisement