Miss Tanzania watembelea Mwananchi, wafunguka

Miss Tanzania watembelea Mwananchi, wafunguka

Muktasari:

Fainali za mwaka huu zitafanyika Jumamosi kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam zikishirikisha warembo 20 kutoka kanda tofauti nchini ambapo mshindi atazawadiwa gari aina ya Subaru Impreza wakati mshindi wa pili atapewa kiwanja eneo la Kigamboni.

WAREMBO 20 wanaowania taji la Miss Tanzania 2020 wametembelea makao makuu ya kampuni ya Mwananchi Communication Limited Tabata Dar es Salaam na kujionea mambo mbalimbali yanayohusu uzalishaji wa magazeti ya kampuni hiyo.

Warembo hao ambao keshokutwa Jumamosi watapanda jukwaani kuwania taji la mwaka huu wamefanya ziara hiyo kwa lengo la kujionea namna kampuni ya MCL inavyozalisha bidhaa zake yakiwemo magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen.

Katika ziara hiyo, warembo hao wamezungumza na viongozi mbalimbali wa chumba cha habari cha MCL, studio za Mwananchi Digital na kiwanda cha uchapishaji.

"Sikutarajia kukutana na mazingira bora ya kampuni ya Mwananchi, ziara hii imenitamanisha kuwa mwanahabari," amesema mmoja wa warembo wa Miss Tanzania, Verynice Deokari anayeiwakilisha kanda ya Dar es Salaam.

Mrembo mwingine Zenitha Deodatus anayetokea kanda ya Mashariki amesema amejifunza mambo mbalimbali ya habari katika ziara hiyo.
"Mimi ni msomaji wa magazeti ya Mwanaspoti na Mwananchi, lakini sikuwa naelewa na ninamna gani yanaandaliwa hadi kutufikia, lakini kwa ziara hii nimejifunza mengi," amesema Zenitha.  
Kwa nyakati tofauti warembo hao wameeleza ndoto zao kwenye fainali ya Miss Tanzania, huku kila mmoja akiamini atatwaa taji hilo na kuiwakilisha nchi kwenye shindano la dunia (Miss World).

Mhariri mtendaji wa gazeti Mwananchi, Angetile Osiah amewambia wote ni washindi na ndiyo sababu wameingia kwenye fainali akiwapongeza kwa hatua hiyo.

"Hadi kuingia fainali maana yake wote nyie ni  washindi ingawa taji la Miss Tanzania liko moja, lakini uwepo wenu kwenye fainali ni fursa ya kufika mbali zaidi bila kujali umeshinda taji au la," amesema Angetile.

BY Imani Makongoro