Mikasa mitano ya Mkude

Muktasari:

Mashabiki wa Simba wanahofu kumkosa katika mechi muhimu ya leo, lakini kama taasisi inasimamia taratibu zake

KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude atakosekana katika mechi ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum baada ya kusimamishwa kwa tuhuma zilizotajwa kuwa ni masuala ya kinidhamu ambayo hayakuwekwa wazi.

Mkude ambaye amedumu Simba kwa takriban miaka 10 sasa amekuwa na mikasa mbalimbali ya kinidhamu aliyokutana nayo kwa nyakati tofauti ingawa baadhi imekuwa ikiwekwa wazi na mengine kupita kimya kimya.

Tuhuma ambazo zinamkabili Mkude wakati huu mpaka kusimamishwa si za kwanza kwake. Mwanaspoti imekukusanyia matukio matano ya utata ya kiungo huyo ndani ya kipindi hicho klabuni na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

AMUNIKE AMTEMA

Juni mwaka juzi aliingia matatizo na kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike ambaye alimtema kikosini wakati wanajiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri uliofanyika Juni 13, 2019.

Mkude baada ya kuitwa alishindwa kufika mazoezini kwa wakati kama ambavyo wachezaji wengine walioitwa wakati huo walifika na kuanza mazoezi.

Amunike aliamua kumtema Mkude baada ya kushindwa kuhudhuria mazoezi huku ikidaiwa kuwa aliomba apumzike kwani alichoka kutokana na kucheza mechi nyingi mfululizo akiwa na timu yake.

KUJIUNGA NA KAMBI

Miezi mitatu baadaye baada ya tukio hilo na Amunike, Mkude aliingia matatani na Simba akituhumiwa kuwa na utovu wa nidhamu baada ya kushindwa kujiunga na na timu kwenye mechi mbili za Kanda ya Ziwa zilizofanyika Septemba 26 dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United iliyopigwa Musoma Septemba 29.

Baada ya kikosi hicho kuondoka kwenda kucheza mechi hizo mbili aliyekuwa kocha wa Simba wakati huo, Patrick Aussems alitaka Mkude ajiunge na wenzake lakini uongozi wa Simba ulipinga jambo hilo na kataka kumchukulia hatua za kinidhamu.

Oktoba 3 mwaka juzi uongozi wa Simba ulifanya kikao chake cha ndani cha kinidhamu na Mkude akiwa pamoja na wachezaji wengine Gadiel Michael, Erasto Nyoni na Clatous Chama walikutwa na hatia ambapo walipewa adhabu ya kinidhamu ambayo haikutangazwa.

MKUDE, NDAYIRAGIJE

Machi mwaka jana, Mkude aliingia tena matatani kwa utovu wa nidhamu baada ya kushindwa kufika kambini kwa wakati katika kambi ya Stars iliyokuwa ikijiandaa na mashindano ya Kombe la Chan.

Kocha wa Stars, Etienne Ndayiragije alinukuliwa akisema kuwa Mkude hakutokea kambini kwa siku kadhaa na hakumpa taarifa yoyote na hajui yuko wapi.

“Hajafika kambini licha ya wenzake kuanza mazoezi na sijui yuko wapi hivyo siwezi kumhukumu moja kwa moja kwa sababu sijui nini kimempata, nasubiri mpaka nikipata taarifa zake kamili ndipo nitatolea uamuzi jambo hili,” alikaririwa akisema Ndayiragije.

Hata hivyo. siku chache baadaye kambi hiyo ilivunjwa baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutangaza kusitisha shughuli zote za michezo kutokana na kuibuka kwa janga la virusi vya corona duniani.

KUCHELEWA KAMBINI

Siku chache kabla ya mwaka jana kumalizika Mkude alishindwa kucheza mchezo dhidi ya Coastal Union uliofanyika Novemba 21 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha ambao Simba ilishinda mabao 7-0.

Na mara baada ya mchezo huo kumalizika kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alikaririwa akisema kuwa sababu ya kiungo huyo kukosa mchezo huo ni kutokana na kuchelewa kufika kambini.

Siku chache baadaye Mkude alijiunga na kambi ya Simba iliyokuwa ikijiandaa kucheza mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Plateau United kutokea Nigeria, ambayo walishinda bao 1-0, kiungo huyo mkabaji alianza kikosi cha kwanza.

SABA KUONDOLEWA STARS

Mwaka 2019, kocha wa Stars wa wakati huo, Amunike aliwaondoa wachezaji watano wa Simba katika kikosi chake kilichokuwa kinajiandaa kucheza dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ katika mchezo wa Kombe la Mataifa Afrika.

Wachezaji ambao waliondolewa ni Mkude, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe na sababu kubwa ilielezwa ni kuchelewa kufika kambini kwa muda uliopangwa kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine waliofika kwa wakati.

WASIKIE HAWA

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Ally Mayay ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Yanga na Stars anasema kitendo cha Mkude kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu sio kiashirikia kizuri kwa kipaji chake maana ni mchezaji mwandamizi hivyo anatakiwa kuwa kioo kwa wanaochipukia.

“Licha ya kwamba Simba hawajatoa sababu gani imewafanya wamsimamishe Mkude lakini hii si mara ya kwanza, ya pili au ya tatu mchezaji huyo kukumbwa na matukio ya utovu wa nidhamu, hivyo anatakiwa ajitathimini na kujua wapi anakosea na ajirekebishe kwani sio kiashiria kizuri kwa maendeleo ya kipaji chake.

“Nidhamu ni kufuata utaratibu mliokubaliana hivyo Simba wako sahihi kwa uamuzi waliochukua kwani hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu.

“Mkude ni brandi, ni kioo cha chipukizi wanaochipukia katika soka anatakiwa kuwa mfano na sio kila siku linaibuka jambo jipya dhidi yake, kama atalichukulia uzito jambo hili basi liwe tukio la mwisho kwake. Abadilike sasa. Ni mchezaji mzuri lakini masuala haya yatamuharibia,” anasema Mayay.

Kocha Mohammed Adolph Rishad anasema Mkude anajitia mwenyewe kasoro wakati ni mchezaji mzuri mwenye kuweza kuyaepuka mambo hayo.

“Mchezaji mzuri lakini huwa nashangaa ana matatizo gani yanayomfanya kuwa na mambo mengi yanayomtia matatizoni kila wakati. Anatakiwa kubadilika na kutambua kuwa mpira ni nidhamu hivyo asipojirekebisha mwenyewe anajitia kasoro zitakazomharibia kazi yake,” alisema Adolph.