MC Pilipili kuzikwa Novemba 20, Dodoma
Muktasari:
- Tarehe hiyo imetajwa leo jioni Jumatatu Novemba 17,2025 na mratibu wa mazishi hayo MC John Mwangata ambaye amesema tayari kila kitu kimeandaliwa.
Mwili wa Emmanuel Mathias (MC Pilipili) utazikwa Alhamisi wiki hii, Novemba 20,2025 jijini Dodoma baada ya ndugu kujadiliana na kukubaliana.
Tarehe hiyo imetajwa leo jioni Jumatatu Novemba 17,2025 na mratibu wa mazishi hayo MC John Mwangata ambaye amesema tayari kila kitu kimeandaliwa.
Mc Pilipili alikutwa amefariki dunia jana Jumapili, Novemba 16,2025 majira ya jioni na ilikuwa muda mfupi kabla ya kwenda kwenye sherehe aliyotakiwa kwenda kuongoza ushereheshaji.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi alithibitisha kuwa mwili wa mshereheshaji huyo ulipelekwa hospitalini hapo na wasamaria wema kati ya saa 10.30 hadi saa 11 jioni.
Mapema leo dada wa MC Pilipili, Veronika Mathias amesema bado hawajapanga taratibu za maziko kwani walikuwa wakimsubiri kaka yao mkubwa anayeishi Dar es Salaam.
Ilipofika saa 12 jioni MC Mwangata ametangaza tarehe ya mazishi.
"Familia imeshapanga kuwa ndugu yetu MC Pilipili tutamuweka katika nyumba yake ya milele siku ya Alhamisi ya Novemba 20,2025, naomba tuendelee kuwa wapole na tuzidi kutoa michango yetu kama tunavyotakiwa," amesema MC Mwangata.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bahi, Stewart Masima amesema chama hicho kinaendelea kusaidia uratibu kwa karibu kwani MC Pilipili alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya hiyo.
Masima amesema CCM Wilaya ya Bahi wamepoteza kiongozi mwenye uwezo na maono ambaye alitegemewa kwa wakati huu na siku za usoni.