Mastaa Bongo waiteka shoo ya dabi

Muktasari:

  • Wasanii wa Bongo mbali na kuigiza na kuimba, wamefunguka mahaba yao kwa timu zao hizo na kila mmoja ameichambua mechi hiyo akiamini timu yake itafanya vizuri na kuibuka na ushindi.

MCHEZO wa 112 wa Watani wa Jadi, Yanga na Simba utachezwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam na umeteka hisia za mashabiki kila kona nchini hadi tasnia ya burudani.


Wasanii wa Bongo mbali na kuigiza na kuimba, wamefunguka mahaba yao kwa timu zao hizo na kila mmoja ameichambua mechi hiyo akiamini timu yake itafanya vizuri na kuibuka na ushindi.


Wale wa Yanga wamesema kinachoenda kutokea ni mwendelezo wa kilichotokea Novemba 5 na mabingwa hao watetezi walishinda mabao 5-1 dhidi ya watani zao, huku wale wa Simba wakitamba hakuna maumivu mara mbili na wengine wakikata tamaa kutokana na matokeo ya mechi zao za mwisho na wengine wakisema liwalo na liwe.


Kinachovutia zaidi kwenye tambo hizi za dabi ni wasanii wawili waliohusishwa kuwa na uhasama kwenye muziki na mashabiki lia lia wa timu hizi, Sir Juma Nature na Inspector Haroun.


Achana na muziki wao, huku kwenye soka kila mmoja kwa wakati wake pamoja na wasanii wengine wa Bongo Fleva na Bongo Muvi, wametoa maoni yao na tambo juu ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki ndani na nje ya nchi.

JUMA NATURE - YANGA HII MTAUMIA
Juma Nature anasema yeye ni shabiki kindakindaki wa Yanga na msimu huu ni hatari zaidi na anaona kabisa Stephane Aziz KI atakuwa mchezaji bora wa mechi na Djigui Diarra kipa bora.
Anasema ingawa Yanga itatawala mcheza hususan nyota huyo wa Burkina Faso.


Anasema timu hiyo haitabiriki na imekuwa ikifanya vyema na katika imebeba makombe licha ya ushindi mdogo lakini ushindi ni lazima.


Kuhusu kukosekana kwa wachezaji baadhi kwenye mechi, kuelekea mchezo wa dabi, alisema, "Sio Yanga hii labda ile ya miaka iliyopita akikosekana mtu inafunga. Lakini hii, iko vizuri sana," alistamba na kuongeza;


"Yanga hii hata akikosekana mchezaji mmoja inashinda. Si unakumbuka walikosekana wachezaji wanaowategemea lakini wakaweza kuwabana Mamelodi Sundowns. Labda golini akitoka Diarra kuna cheche, lakini wengine sidhani, Yanga hii iko vizuri."


Kuhusu wachezaji alisema "Kama kuna wachezaji umri umeenda wanastahili kupumzishwa na wale wenye mikataba iangaliwe ili kutafuta wengine ingawa Yanga inajiweza."


INSPECTOR - KIBU ANAWAPIGA TENA
Kwa upande wa mtani wake Inspector Haroun alisema ana imani na Simba na hasa mshambuliaji wa timu hiyo, Kibu Denis atafanya makubwa kwa sababu ni mpambanaji na ana nguvu na kwa kipindi cha hivi karibuni amekuwa akifanya hivi, hivyo Yanga ijipange.


Kuhusu mchezo huo alisema dabi ina changamoto zake lakini hawatakubali kufungwa tena na Yanga kwani Kocha wa miamba hiyo, Abdelhak Benchikha ana mbinu zake na anajua atawapanga nani na nani.


"Mchezo wa mwisho watani zetu walitufunga ingawa Kibu Dennis alifunga. Amekuwa strong na anafanya vizuri licha ya kutokufunga kwenye baadhi ya mechi za Ligi na zile za kimataifa ingawa ana bahati kwenye mechi za Yanga na Simba. Pia nina imani na Sadio Kanoute eneo la 'Holding Midfielder' na Mzamiru Yassin. Sijajua mwalimu atampanga nani siku hiyo. Kama Kanoute atashuka chini na Mzamiru akawa juu wakavuruga vuruga hawa ni watu wanaoiweza dabi na wapinzani wetu wataogopa wakimwona Kanoute kati kuliko akiwa juu zaidi.


"Nina imani kubwa sana na ushindi kwa timu Yanga. Tumekuwa na msimu mbaya kwa takriban mechi mbili za kimataifa tumefanya vibaya. Tumerudi nyumbani tumekuwa tukisuasua, lakini dabi ni dabi na nina imani wachezaji watataka kurudisha imani kwa wapenzi wao, hivyo waajipanga na kufanya vizuri kupata pointi tatu na kujitoa kwenye matokeo mabaya tunayoyapata."


Kuhusu Simba ya msimu huu Inspector anasema; "Soka ni mchezo hai na dakika 90, ni vibaya tukianza kukata tamaa mapema japo tuna tatizo kidogo la washambuliaji katika umaliziaji na waliopo hawajatupa kile tunachokihitaji wakiwamo Pa Omary Jobe na Freddy (Michael).


"Ipo wazi hata Benchikha anapambana na viongo kuona kama watapata mabao na kwenye dabi naona kutakuwa na mabadiliko na maoni yangu kwa timu na benchi zima la ufundi kama watapata nafasi ya kutumia vijana damu changa kama kina Chasambi (Ladick) na Karabaka (Salehe) wanaweza kufanya mageuzi makubwa kuliko hawa tunaowaona wa kimataifa."


“Tatizo la kutofanya vizuri Simba ni lile lile. Nafasi zinatengenezwa na viungo kama Chama (Clatous) anafanya vizuri tu nikiangalia beki wa kulia na kushoto wanajituma kwa kweli ila wanakosa namba saba ambaye ana spidi kali ya kumsaidia Shomary Kapombe na Tshabalala (Mohamed Hussein) akiwa amepanda lakini timu ukianzia namba moja kama tutakuwa na Ayubu (Lakred), nina uhakika golini kutakuwa na mtu."


Wapo pia mastaa wengine ambao hawajaficha hisia zao za mchezo huo wa dabi na hapa wanafunguka;


GIGY MONEY - YEYOTE TWENDE
Gift Stanford ‘Gigy Money’ msanii wa Bongo Fleva, anasema bado anajitafuta kwani hajajua yuko timu gani, inategemea siku hiyo wamechezaje na timu  itakayoshinda ndio anashangilia.


“Yaani mimi kwa kweli niseme tu ukweli, kwenye mpira hapa nitakudanganya tu, maana nitajitafuta kuongelea hadi asubuhi, mimi bado sijajua nipo timu gani. Yaani naweza kukaa na mtu nikamwambia nipo timu hii, halafu nikajisahau hapo hapo nikashangilia timu nyingine. Kiufupi sijielewi ila nina jezi ya Simba ya Yanga, Azam tu ndio sina.”



AMINI - SIMBA INATOBOA
Huyu ni msanii wa Bongo Fleva aliyeibukia katika Jumba la Vipaji Tanzania (THT). Anasema ni shabiki wa Simba anasema dabi haina mwenyewe na haizoeleki.


“Kitu cha kwanza tukizungumzia dabi haina mwenyewe. Unaweza ukakisia mchezaji fulani atafanya vizuri na asifanye vizuri na dabi haizoeleki hata siku moja. Mimi naona simba inaenda kucheza kitimu na wachezaji watashirikiana kwa pamoja, hivyo kila mchezaji atakayeshiriki mchezo huo, amepangwa katika 'First Eleven' naamini atafanya vizuri."


“Na nikwambie tu Simba ya msimu huu ubingwa inawezekana wachezaji wakiendelea kuwa na morari mzuri na kocha akiendelea kuwaweka katika mazingira mazuri ya ukaribu kwa kuwashauri wafanye nini uwanjani wakiwa karibu na goli."


“Simba kutofanya vizuri kwa mechi za hivi karibuni ni matokeo tu ya mpira kuna kufungwa, kushinda na droo kwa sababu hata hao Bacerona na Madrid wanafungwa na kudroo. Kwa hiyo kama timu inakuwa inashinda basi wamepata bahati kwani soka ni mchezo wa mchezo wa bahati na Simba ni timu nzuri na itaendelea kufanya vizuri."


“Na hiyo Tarehe 20 mchezaji Chama hawezi kukosekana sababu chama ni mchezaji ambaye anaweza kukupa matokeo muda wowote ule na anajua kuchezesha foadi, winga namba sita. Kama chama atakuwa anatokea pembeni, yaani unaona kabisa ni kiungo fulani mwenye akili nyingi hivyo katika mchezo huu Chama hatakiwiki kukosa,” anasema. 



KALALA JUNIOR AINGOJA SHOO YA PACOME
Ni mwanamuziki wa dansi na Mkurugenzi wa bendi ya Tukuyu Sound. Ni shabiki wa Yanga na anasema;


“Kwanza nianze kwa wachezaji siku hiyo kila mtu na hata mimi natamani nimwone Pacome (Zouzoua) amerudi uwanjani ili burudani ya Aziz KI watu waione kama kawaida na atatupia tu iwe isiwe."


“kiukweli yanga ya msimu huu na mbio zake za ubingwa, wachezaji wamefanya timu yetu sasa hivi hata watu kuangalia, yaani bora wasiangalie Manchester au timu nyingine, hata ikiwa Manchester au Arsenal ama timu nyingine yupo radhi aingalie Yanga kuliko kuangalia hizo timu."


MSAGA SUMU AMJAZA UPEPO AZIZ KI
Mwanamuziki wa Singeli na shabiki wa Yanga  anasema "Kwanza mimi elewewa ni shabiki kindaki ndaki wa yanga na ni mwanachama kabisa halali. Katika timu yetu kuna wachezaji kama watatu hivi naamini Tarehe 20 watafanya vizuri Mkude (Jonas), Mudathir (Yahya) na kama atacheza Pacome na Azizi KI ambaye haina mjadala. Kuhusu ubingwa naona majibu kamili ni Jumamosi kama tutamfunga mtani nina imani njia itakuwa nyeupe kuliko tukifungwa. Labda pia sare ubingwa upo vizuri. Tukishamfunga mtani tutakuwa tumemwacha pointi kama 12 hivi, kwa hiyo 12 na yeye na Azam atakuwa hajacheza."


“Hivyo inabidi sisi tumfunge mtani ili tule pensheni, lakini akitufunga kidogo itakuwa utata, lakini asilimia kubwa tunachukua ubingwa. Tunahitaji straika mtupia mabao kuja kumsaidia Mzize (Clement) au Guede (Joseph) yaani kazi yake ni kufunga tu akipata nafasi tatu, moja bao, nafasi sita, mabao matatu."


MONALISA - LIWALO NA LIWE
Ni msanii wa filamu Yvonne Cherrie ambaye pia ni shabiki wa Simba anasema kwa sasa wamevurugwa na matokeo wanayopata na timu inafanya vibaya hadi anaona kero na liwalo na liwe kwenye mchezo huo anaoona utakuwa mgumu upande wao (Simba).


"Sasa hivi timu hakuna labda hadi msimu ujao usajili ukifanyika. Kwa sasa sina imani kama tutabeba ubingwa, tusidanganyane. Kwenye dabi wacheze tu shauri yao. Hakuna timu na hakuna mchezaji aliyekosekana ikawa kuna pengo. Timu inatoka sare na Ihefu? Kwa sasa hakuna kitu, wanaboa bana.”