Mashauzi, Kopa walivyonogesha Raha za Pwani

Muktasari:

  • Licha ya hali ya hewa kuwa na mvuamvua na tope jingi kuwepo mitaani, lakini hiyo haikuwazuia mashabiki wa miondoko hiyo kujitokeza kwa wingi kupata burudani kupitia onyesho la Raha za Pwani 2024 lililoandaliwa na Mwanamitindo Khadija Mwanamboka.

NANI aliyekuambia muziki wa Taarabu umezimika? Waliokuwa ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana Jumamosi ndio wanaojua nini kilichotokea.

Licha ya hali ya hewa kuwa na mvuamvua na tope jingi kuwepo mitaani, lakini hiyo haikuwazuia mashabiki wa miondoko hiyo kujitokeza kwa wingi kupata burudani kupitia onyesho la Raha za Pwani 2024 lililoandaliwa na Mwanamitindo Khadija Mwanamboka.

Zile kelele baadhi ya waimbaji mahiri wa muziki huo hawaivi chungu kimoja, juzi usiku ilidhihirisha ni blah blah kwa namna wakali watano wa miondoko hiyo kupanda jukwaa moja na kushusha burudani iliyowakumbusha mbali mashabiki waliojitokeza.

Malkia wa Mipasho, Khadija Kopa, Isha Mashauzi, Afua Suleiman, Leila Rashid, Mwanaidi Shaaban na Fatma Issa wa miondoko walitoa burudani ya nguvu kwenye jukwaa moja ambayo iliwafanya mashabiki wa miondoko hiyo washindwe kutulia katika viti vyao.


Tamasha lilianza rasmi saa 4:00 usiku na muimbaji wa zamani wa East African  Melody ambaye pia aliwahi kufanya kazi  kundi la Muungano Cultural Troupe, Mwanaidi Shaaban alianza kuimba wimbo wake wa ‘Jinamizi’, uliompatia umaarufu akiwa na East  African Melody.

Baada ya Mwanaidi kushuka, Fatuma Issa kutoka visiwani Zanzibar alipanda na wimbo wa ‘Adui Kiumbe’ kutokana na umri mkubwa na miguu kumsumbua kila wakati, aliimba akiwa amekaa kwenye kiti, lakini aliweza kuwanogesha mashabiki kwa sauti yake maridhawa.

Washehereshaji wa onyesho hilo lililohudhuriwa na mastaa mbalimbali wakiwamo waigizaji wa filamu nchini, walikuwa Gea Habib na Hadija Shaibu ‘Didah’.

AFUA NA KHADIJA KOPA
Kwa upande wa Afua Suleimani alikuwa mtu wa pili kupanda jukwaani na kuimba wimbo wa ‘Unajidodo’ uliopatia umaarufu akiwa na East African Melody miaka ya nyuma na kuwapagawisha mashabiki.


Utamu ulizidi baada ya kufika zamu ya Malkia wa Mipasho, Khadija Kopa aliyekuwa wa tatu kupanda jukwaani na aliimba wimbo wa ‘Mtie Kamba Mumeo’ yeye kama kawaida yake kusepa na kijiji akiwa jukwaani.

Leila Rashid,  mke wa Mzee Yusuf alikuwa wa nne kupanda  na wimbo wa ‘Langu la Rohoni’ wimbo huu alitamba nao sana kipindi cha nyuma na bendi aliyopo sasa ya Jahazi Morden Taarabu chini ya Mzee Yusuf.

Kwake Isha Mashauzi, mama wa kutikisa kifua akiwa anaimba, alikuwa mtu wa tano kupanda jukwaani na kuimba wimbo wake wa ‘Tugawane Ustaarabu’. 


Wimbo huu Isha aliupatia umaarufu kwenye bendi yake ya Mashauzi Clasic  alivyotoka bendi ya Jahazi Mordrn Taarabu ya Mzee Yusuf.

UTAMU ZAIDI
Mashabiki walijitokeza kwa wingi katika viwanja hivyo huku wakimshangilia kila msanii aliyekuwa akipanda stejini kutoka shoo hiyo ya aina yake iliyoandaliwa kwa mbwembwe nyingi, ilifika raundi ya pili ya kutoa burudani na Fatuma Issa kama kawaida alipanda jukwaani na kiti aliimba kwa pamoja na Leila Rashid wimbo wa ‘Aso Kasoro’ kisha Afua Suleiman aliimba wimbo wa ‘Ngoma Iko Huku’ kisha kupisha Khadija Kopa aliimba kibao cha ‘Mjini Chuo Kikuu’ kabla ya Isha Mashauzi kushuka na ‘Viwavi Jeshi’.

Kwa namna mashabiki waliokuwa na hamu ya kuwaona wakali hao katika jukwaa moja, kila aliyepamba na kushuka alituzwa fedha na kufanya mashabiki waliojitokewa ukumbini kujimwayamwaya kwa raha zao kufurahia burudani hiyo iliyofanyika sambamba na kuadhimishwa kwa Miaka 60 ya Muungano.


HILI NA LILE
Kama kawaida katika kila tamasha hata liandaliwe vipi, huwa hapakosi mambo mazuri na dosari zake.
Juzi usiku moja ya mambo mazuri na yaliyovutia ni namna ukumbi ulivyopambwa.

Asilimia kubwa ya mapambo yalikuwa ni ya asili kama Kanga, Mkeka na vingine vinavyoiwakilisha Ukanda wa Pwani kama lilivyo jina la tamasha hilo ‘Raha za Pwani’.

Hata hivyo, kulikuwa na dosari ingawa sio kubwa na moja ya hizo ni upande wa kipaza sauti ‘Microphone’ na zilikuwa chache na kusababisha waimbaji kupokezana hata ilipofika zamu ya kuimba wawili wawili.

Hata kwa washereheshaji ilikuwa hivyo hivyo na mmoja akitangaza ilibidi ampe mwingine ingawa mambo mengine yalienda sawa.

Pia hakukuwa na mpangilio kwa mashabiki kwenda kuwatuza waimbaji na kuonekana hali ya vurugu iliyosababisha mashabiki wengine kutokuona jukwaani waimbaji wanaotumbuiza ambao ndio haswa waliowafuata ukumbini hapo kusuuza roho zao.

Hata hivyo, kwa kifupi ni tamasha hilo lilikuwa bab’kubwa kwa namna utamu ulivyonogeshwa na waimbaji hao sambamba na wapiga ala akiwamo Mzee Yusuf aliyepapasa kinanda kwa ustadi mkubwa akikumbushia enzi zake.