Mama Diamond amliza Shilole, sababu hii hapa
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea Bi Sanura alipokuwa akiwasili kwenye ukumbi wa sherehe Madale na Shilole alisikika akipaza sauti akisema, "Mama... mama... mama yangu!" huku akilia, jambo lililowavutia wageni wengi waliokuwa wakifuatilia hafla hiyo.
Hisia zilitawala kwenye sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa ya mama mzazi wa mwanamuziki Diamond Platnumz, Bi Sanura, baada ya msanii wa Bongo Fleva, Shilole kushindwa kuzuia machozi alipomuona mama huyo akiingia ukumbini.
Tukio hilo lilitokea Bi Sanura alipokuwa akiwasili kwenye ukumbi wa sherehe Madale na Shilole alisikika akipaza sauti akisema, "Mama... mama... mama yangu!" huku akilia, jambo lililowavutia wageni wengi waliokuwa wakifuatilia hafla hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya tukio hilo, Shilole amesemahakutarajia hisia zake kumzidi, lakini kumwona Bi Sanura kulimrudisha kwenye kumbukumbu za mama yake mzazi aliyefariki dunia miaka iliyopita.
"Nilipomuona Mama Diamond akiingia ukumbini, nilimkumbuka mama yangu. Nilijikuta tu machozi yananitoka nikaanza kumuita, 'Mama... mama... mama yangu.' Sikuweza kujizuia," amesema Shilole.
Msanii huyo amewahi kueleza kwenye mahojiano mbalimbali kuwa kumpoteza mama yake akiwa mdogo ni moja ya majeraha makubwa aliyobeba maishani na alilazimika kuanza kujitafutia maisha mapema baada ya kifo cha mzazi wake huyo.
Kutokana na historia hiyo, tukio la kumwona Bi Sanura akiingia ukumbini lilimgusa moja kwa moja na kumfanya akumbuke upendo wa mama yake, hali iliyompelekea kushindwa kuzuia hisia zake mbele ya wageni waliohudhuria sherehe hiyo.