Mahaba ya Nandy kwenye ‘Nibakishie’ yamuibua mke wa Ali Kiba

Mahaba ya Nandy kwenye ‘Nibakishie’ yamuibua mke wa Ali Kiba

Muktasari:

Alikiba  walifunga ndoa na Amina miaka miwili iliyopita ambapo wamejaliwa kupata mtoto mmoja waliyempa jina la Keyan.

IKIWA imepita wiki moja tangu kutoka kwa video ya wimbo ‘Nibakishie’  ulioimbwa na msanii Nandy akimshirikisha  Ali Kiba, hatimaye mke wake aibuka na kuizungumzia.

Video hiyo imekuwa gumzo huko mitandaoni ikiwemo mahaba yaliyoonyeshwa  kati ya wasanii hao wakati wa upigaji picha za video.

Moja ya kipande ambacho kimekuwa gumzo ni kile kinachomuonyesha AliKiba akiwa anapiga kelele wakati akiwa anakaa katika jakuzi  lililokuwa limejazwa maji kumfuata Nandy ambacho kimekuwa gumzo kuliko hata wimbo wenyewe.

Kipande hicho hadi  kufika leo Jumanne Novemba 24, 2020 kinakamata namba 12 kwa kutazamwa YouTube huku video ya wimbo yenyewe ikishika namba tatu.

Ni kutokana na hilo, mmoja wa mashabiki anayetambulika kwa jina la Officialneisazy, ameandika “Kiba atajuta kwa nini  alifanya video na Nandy daah ukiwa mume wa mwanamuziki inabidi ufumbe macho usione chochote.


Muwekaji andiko huyu hakuishia hapa kwani aliweka picha mbili, moja ikimuonyesha Kiba akiwa na mkewe Amina na nyingine Alikiba akiwa amemkumbatia Nandy.

Jambo hilo limeonekana kumshinda uvumilivu, mwanamke huyo ambaye ni raia wa Kenya na kujikuta akimjibu shabiki huyo.

Akijibu posti hiyo,  ameandika “Usilolijua ni kama usiku wa giza, peleka ufafanuzi wako maktaba.

Amina anatoa jibu hilo ambalo watu hawajategea ukizingatia ni mtu ambaye hajazoeleka kuwa na majibizano kwenye mitandao kama baadhi ya  wake wengine wa mastaa.

Alikiba  ambaye jina lake halisi ni Ally Salehe Kiba walifunga ndoa na Amina miaka miwili iliyopita ambapo wamejaliwa kupata mtoto mmoja waliyempa jina la Keyan.

________________________________________________

By NASRA ABDALLAH