Linex afichua siri ya kupungua mwili
Muktasari:
- Staa huyo wa Salima, Sawa Baby, Moyo wa Subira, Mama Halima na nyingine amekuwa na mabadiliko ya muonekano kwa siku za karibuni tofauti na ilivyokuwa.
NYOTA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Linex Mjeda ameamua kufunguka juu ya mabadiliko ya mwili wake, akikanusha kupunguzwa kutokana na matumizi ya vinywaji vikali.
Akizungumza na Mwanaspoti mitaa ya Sinza, Dar es Salaam wikiendi iliyopita Linex alisema amekuwa akipata tuhuma nyingi kuhusu matumizi ya vilevi vikali na mengineyo, lakini hakuna hata moja lenye ukweli na kwamba hali yake ya kuonekana kukonda inatokana na mwenyewe kujiweka kwani anaifurahia kuliko kuwa mnene.
“Napata sana tuhuma za kuambiwa natumia dawa za kulevya, mara navuta bangi nyingi mara mara nimeukwaa, ila kikubwa mimi afya yangu iko fiti na napenda hivi nilivyo sasa,” alisema Linex na kuongeza;
“Wapo wengine wanasema maisha yangu ni magumu, niwaambie mimi sijawahi kuwa na maisha magumu hata siku moja, nakula vizuri nalala pazuri na starehe nafanya kama kawaida. Na huwa napenda kuonekana mwembamba kuliko kuwa kibonge, hivyo wakae kwa kutulia. Najifurahia nilivyo.”
Staa huyo wa Salima, Sawa Baby, Moyo wa Subira, Mama Halima na nyingine amekuwa na mabadiliko ya muonekano kwa siku za karibuni tofauti na ilivyokuwa.