Les Wanyika kupagawisha mashabiki wa Rhumba leo Arusha

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Bendi ya Les Wanyika yenye chimbuko lake jijini Arusha miaka ya sabini ilipoundwa ikijulikana kama ‘Arusha Jazz Band,’ na baadae ikahamia nchini Kenya na kuitwa Simba Wanyika, chini ya Profesa Omar Shaaban waliojiengua kutoka Simba Walipotea kuimba zaidi ya miaka 10 na sasa wamerudi tena wakianza na Shoo Arusha.


Wataalamu wa burudani wa nyimbo za miondoka ya Rhumba Afrika Mashariki na kati, 'Les Wanyika' wamerudi tena kwa kishindo nchini na wanatarajia kufanya shoo ya kibabe leo jumamosi May 27 jijini Arusha.

Bendi ya Les Wanyika yenye makao yake makuu kwa sasa nchini Kenya, walipotea kwenye fani zaidi ya miaka 10 iliyopita na sasa wamerejea tena ulingoni na wanatarajia kujitambulisha upya kwa wana Arusha leo katika viwanja vya makumbusho ya Via via vilivyoko katikati ya jiji la Arusha.

Burudani hiyo ya bendi ya Les Wanyika nchini ni sehemu ya Tamasha la kimataifa la Utamaduni, Sanaa na Michezo la Afrika 'FestacAfrika' linaloendelea  jijini Arusha tangu may 21 na litahitimishwa may 27 mwaka huu

Meneja wa bendi Boni Nyaga akizungumza na waandishi wa habari amesema jumla ya wasanii 10 wanatarajia kuimba nyimbo zaidi ya 20 zinazopendwa na Mashabiki wao wa Tanzania ikowemo Sina makosa, Afro,’ ‘Nimaru,’ ‘Pamela,’ ‘Kasuku,’ na ‘Safari ya Samburu.

"Sasa kwa mara ya kwanza baada ya miongo kumi, tangu iondoke nchini Les Wanyika inarejea nyumbani ilikozaliwa, Watu waje wapate ladha halisi ya Les Wanyika, maana wengi huwa wamezoea kusikia bendi zingine zikipiga kopi za nyimbo zetu,” aliongeza Nyaga.

"Bendi yetu chimbuko lake ni jijini Arusha, miaka ya sabini ilipoundwa ikijulikana kama ‘Arusha Jazz Band,’ na baadae ikahamia nchini Kenya na kuitwa Simba Wanyika, chini ya Profesa Omar Shaaban waliojiengua kutoka Simba Wanyika na kuanzisha Les Wanyika" alisema Nyaga

Alisema kuwa tamasha hilo linatarajia kuanza majira ya saa mbili usiku hadi asubuhi ambapo kiingilio  ni shilingi 5000 kwa mashabiki wa kawaida na shilingi 10,000 kwa VIP .

"Tumetoa viingilio vidogo viwe rafiki kwa mashabiki wetu wengi kuja kushuhudia wanamuziki wa bendi yao halisi na sio zile wanazoimbiwa na bendi chipukizi, hivyi niwakaribishe waje kwa wingi kuona wataalamu wa kupiga vyombo na kuchekecha koo kutoa sauti ya kuimba" alisema