Laizer Classic producer aliyeisimamisha lebo ya WCB

Muktasari:
- Huyu ni prodyuza wa supastaa Diamond Platinumz na lebo nzima ya Wasafi ila amefanya na anaendelea kufanya ngoma kali na wasanii wengine wengi ndani na nje ya nchi.
Mmoja wa watu ambao wamefanya makubwa kwenye tasnia ya uzalishaji wa muziki ‘prodyuza’ lakini wamekuwa wakimya na kuacha kazi ziongee ni Siraju Hamis Amani, maarufu Laizer Classic.
Huyu ni prodyuza wa supastaa Diamond Platinumz na lebo nzima ya Wasafi ila amefanya na anaendelea kufanya ngoma kali na wasanii wengine wengi ndani na nje ya nchi.

Mwanaspoti limempata na kupiga naye stori, ambapo amezungumza mambo mengi kuhusu maisha ya muziki tangu aanze hadi sasa alipo na kupitia makala haya utapata kumfahamu vyema Laizer ni nani.
KUIMBA HADI KUZALISHA
Sio wote wanafahamu kama Laizer alikuwa anaimba, bali Mwanaspoti linakujuza kwamba staa huyo alianza kuimba kabla ya utayarishaji muziki. “Nilianza kuimba na nilikuwa nasikiliza nyimbo za kina Dully na Q Chilla lakini nikienda studio kuwaomba waandaaji kurekodi kuna vitu nilikuwa nataka kufanya japo walikuwa wanashindwa kufanya, hivyo nikajikuta natamani kujifunza kuwa mtayarishaji ili nifanye vile walivyoshindwa. Hapo ndipo niliacha kuimba nikaanza kujifunza kupitia kwa wengine mtaani. Sijaingia darasani.”
WCB NI KAZI TU
Mkali huyo anaeleza kwamba mkataba wake na Wasafi sio wa maandishi, bali walikubaliana kwa mdomo na analipwa kwa kazi.
“Nina studio yangu kwa sababu Wasafi ni kazini na nahitajika pale kazi zinapotakiwa kufanyika. Siendi kila siku kwani ajira yangu sio ya hivyo,” anasema.

Laizer anaongeza kitu kingine ni wasanii pekee walio katika lebo ya Wasafi ndio wanatakiwa kufanya kazi kwenye studio hiyo kwa sababu ipo nyumbani kwa Diamond, hivyo ni ngumu msanii wa nje ya lebo hiyo kufanya kazi labda kwa marafiki wa karibu.
BURUNDI HADI TANZANIA
Wengi walikuwa wakijua Laizer ni Mrundi, lakini hapa pia anaweka wazi ilikuwaje hadi akatua katika lebo ya WCB.
“Mimi ni Mtanzania niliyezaliwa Kigoma ingawa Kigoma na Burundi ni jirani, hivyo nilienda kujitafuta kule. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa sasa naona mambo yananiendea vizuri kwa sababu ndani ya miaka mitano nimejijengea ufalme,” anasema.
Laizer anasema kipindi ambacho alitua Burundi alikuwa na hofu na Marco Chali kwa hapa Bongo kutokana na ukubwa wake kwa sababu ndio kwanza alikuwa anajitafuta hivyo akaona njia rahisi ni kwenda kujitafuta huko na sio Dar es Salaam.
“Diamondi alikuja kufanya tamasha Burundi na Loliloo (msanii wa Burundi) alimleta studio kwangu ndio na hapo ndipo tulikutana na kupenda nilivyofanya kazi yao, hivyo alipopata wazo la kufungua studio akanifikiria mimi moja kwa moja,” anasema.
“Kwa kipindi kile nilikataa kwa sababu ni kama nilivyo saa hizi hapa Tanzania mtu atokee aje kunitoa. Kilichonifanya nimkubalie kuja kufanya naye kazi ni vurugu zilizotokea Burundi kati ya wananchi na Serikali baada ya kuona mambo ni magumu.”
SWEET LOVE KAZI YA KWANZA
Laizer aliingia Wasafi akikutana na utawala wa Prodyuza Tuddy Thomas ambaye alikuwa anafanya kazi nyingi na Diamond kipindi hicho na anaeleza wakati anafika Bongo aliwakuta wakiwa na kazi kali ya ‘Nana’ iliyokuwa inafanya poa sana.
“Kazi yangu ya kwanza kufanya sikumbuki na haikutoka lakini wimbo niliofanya ukatoka wa kwanza ni ‘Sweet Love’ ambao ulikuwa ni wa msanii Akothe kutoka Kenya akimshirikisha Diamond, hivyo ikawa rahisi kwangu kwa sababu nikawa kama familia.”
Laizer anasema ilikuwa changamoto kubwa kwake kufanya kazi na Diamond kwani kuna muda alikuwa anajikuta anafanya kazi chini ya kiwango kutokana na uoga.
“Kuna kipindi nakumbuka Diamondi aliniita na kuniuliza ‘hivi zile kazi kubwa nilizokuwa nasikiliza ulikuwa unafanya wewe kweli?’ Hiyo ni kutokana na kushindwa kufanya kazi zake kwa ubora kutokana na uoga hivyo akawa anafanya na Tuddy ingawa nilimzoea.”
KWETU ILIMRUDISHA WASAFI
Uoga aliokuwa anauonyesha baada ya kutua Wasafi ulimpa wasiwasi Diamond na kumfanya amteme kwa kuacha kufanya naye kazi, lakini hilo halikumkatisha tamaa akaibuka na kazi ya ’Kwetu’ iliyoimbwa na Rayvany ikiwa ni ngoma iliyomtambulisha staa huyo wa sasa.
“Nakumbuka mbali na Diamond kunikataa pia Harmonize hakuwa na imani na mimi kwenye suala la kufanya naye kazi lakini mtu ambaye alinifanya niaminike zaidi ni Rayvany ambaye hachagui mtayarishaji alikuwa na ‘vibe’ muda wote hivyo tukawa tunafanya kazi pamoja,” anasena.
Laizer anasema baada ya hapo akafanya kazi ambayo ilikuwa tangazo japo hawezi kuitaja ni mtandao gani aliyoipeleka kwa Master J ambaye alipenda alichofanya, kisha akampa maua yake na ndipo Diamond aliposikia akampa pongezi.
WCB UHURU KAMA WOTE
Licha ya Diamond kuwa na Studio imebainika wasanii waliopo kwenye lebo hiyo akiwemo Zuchu wanaruhusiwa kwenda kurekodi nje ya studio yao.
“Ni kweli kulikuwa na wasanii wengi kipindi hicho kabla ya Rayvan na Harmonize kuondoka lakini hiyo ilikuwa hainipi shida kwani Diamond ambaye ni bosi, alikuwa anawaruhusu kutoka kwenda kurekodi nje,”
“Haikuwa kazi yangu mwenyewe kwa sababu nikiwa na kazi nyingi walikuwa wanaruhusiwa kutoka kwenda kufanya kazi sehemu nyingine na hadi sasa ipo hivyo.” anasema mtayarishaji huyo ambaye amekiri tangu amekutana na Diamond amekwenda nchi nyingi.
WIZKID, DIAMOND
Wakati wadau wengi wakijiuliza maswali mengi kuhusiana na kazi ya Diamond na Wizkid kutoka Nigeria baada ya kuona picha wakiwa studio mtayarishaji wake amefichua siri. “Unajua wasanii wana ratiba zao. Anaweza akarekodi leo na akaitoa baada ya miaka mitatu au mitano, hivyo kuna kazi na staa huyo kwa sababu zipo nyimbo tatu wamefanya ingawa sio msanii huyo tu ila wapo wengi na itakuwa kama ‘sapraizi’.”
MAVOKO MMMH!
Rich Mavoko amefanya kazi Wasafi lakini ni moja ya msanii ambaye hakudumu kwa muda ndani ya lebo kutokana na mambo ya kimkataba kutokwenda sawa huku Laizer akifunguka uwepo wake.
“Sijui nisemeje! Nimekaa na Mavoko muda mwingi ila ninachoweza kumzungumzia ni mtu ambaye ukifanya naye kazi ni lazima uwe umejipanga kwani mnaweza mkamaliza kazi pamoja lakini akaja na jambo lake lingine,” anasema.

“Utasikia ‘sasa hapa tumemaliza nataka uweke maunyama yako’ muda huo mimi hapo nimeshafanya kila kitu hivyo alikuwa ananipa mtihani, nilichokuwa nafanya ni kumuambia haya unataka unyama upi? ili nijue nafanyaje.” anasema Laizer aliyekiri tangu Mavoko ameondoka Wasafi hawakuwa tena washikaji.
HARMONIZE AMCHANGIA GARI
"Kitu ambacho nakikumbuka kwa Harmonize gari yangu ya kwanza alichangia kiasi cha fedha nilikuwa nimekwama milioni mbili aliniongezea.
"Nakumbuka gari ilikuwa inauzwa milion 13, ilikuwa Toyota Ractis mimi nilikuwa na milioni 11, hivyo alimalizia kiasi kilichobaki bure kabisa.
"Kuna kazi nyingi tulifanya na Harimonize, zilikuwa nzuri na nilikuwa na imani kuwa zingetoka zingeweza kuwa kazi kubwa sana lakini ndio hivyo mambo yakaingiliana akaondoka Wasafi, ni wimbo mmoja tu aliutoa akiwa nje ya Wasafi nyingine zote sijui ilikuwaje kwani hazijatoka," anasema Laizer ambaye pia kwa sasa hana mawasiliano ya mara kwa mara na Harmonize.
EYOOH HADI KAMIX LAIZER
Siku hizi kuna aina mbili za jingo zinazomtambulisha Laizer. Kuna ile ya Eyooh Laizer na nyingine ni Kamix Laizer. Huu hapa ufafanuzi wake.
“Kipindi cha kwanza nilivyokuwa naanza ‘Kumix na kufanya Mastering’ kazi za maprodyza wengine nilikuwa naweka ‘Eyooh Laizer’ lakini nikaona bora niiondoe ili kutoa changamoto ya kuonekana mimi ndio nimefanya kila kitu kwani watayarishaji wanachukia,” anasema Laizer.
“Ndio nikapata wazo la kutengeneza ‘Kamix Laizer’ ili kuonyesha utofauti kuwa mimi nimehusika kwenye mixing na mwingine atajulikana kafanya mdundo na vitu vingine.”
ABBAH, S2KIZZY NOMA
Ni nadra kwa mtu yeyote aliye na mafanikio akakubali mafanikio ya mwingine ila kwa upande wa Laizer amekiri nchini imebarikiwa watayarishaji wengi wa muziki huku akiwataja baadhi. “Kwa sasa kuna watayarishaji wengi wazuri na wakubwa ninaowakubali namna wanavyofanya kazi mfano Abbah, S2Kizzy, Marco Chali na Kimambo wote wanafanya vizuri,” anasema. “Kwa haraka ni hao lakini wakubwa zangu waliopita ninaowakubali ni Master J, Mika Mwamba, P Funk wote walikuwa bora na ni wazuri hadi sasa.”
SIRI YA KUDUMU WCB
Watu wengi wamepita Wasafi na wengi wameondoka lakini Laizer amefunguka aina ya maisha anayoishi ndio siri kubwa ya kudumu lebo hiyo.
“Sijawahi kuyumbishwa na kitu chochote Wasafi. nNafikiri aina ya maisha nayoishi ndio siri kubwa ya kudumu muda mrefu. Situmii kilevi chochote wala sio mtu wa kutoka sana hivyo kutojichanganya kunanifanya nakosa changamoto nyingi mbaya zinazoweza niondoa kwenye mstari.”
AMTAJA KIBA, OMMY DIMPOZ
Ukaribu na bosi wake Diamond haujawahi kumfanya akashindwa kufanya kazi na wasanii kama ambavyo anakiri amepata bahati ya kufanya na wasanii wote wakubwa.
“Alikiba, Dimpoz sijakaa nao sana ni muda mchache wa kufanya kazi na ikaisha haraka hivyo ninayeweza kumzungumzia kwa ukubwa ni Diamond ambaye nakaa naye muda mwingi.”
WAMDHULUMU MARIOO
Kuna kipindi studio ya Wasafi ilitoa ofa kwa wasanii kutoka nje ya lebo hiyo kurekodi nyimbo na ndipo Marioo aliitumia fursa hiyo, lakini wimbo alioimba haujawahi kutoka hadi sasa. “Marioo kabla hajatoka kimuziki alikuja kutafuta njia ya kurekodi ngoma ili Diamond aisikilize lakini ile kazi ilifanyika nje ya ofisi na mimi niliifanya ingawa haikutakiwa bosi afahamu,” anasema.
“Kulikuwa na jamaa alikuwa anaitwa Mafia ambaye alikuwa msimamizi wa studio akikutana na wateja wote, alinipa hiyo kazi lakini hakutaka Diamond afahamu na mimi sikuwa na neno kwa sababu yeye pia alikuwa bosi wangu nilifanya ila haijawahi kutoka na pesa alichukua Mafia na kunipa kiasi,” anahitimisha Laizer ambaye licha ya kumiliki studio ya muziki na Picha, pia naye ana lebo yake iitwayo Gogumaga Music yenye msanii mmoja aitwaye Narah Elba.