Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuhusu Tausi, Julias, Lovennes ipo siku mtajikuta jela

Muktasari:

  • “Vifungu vya sheria vipo wazi kabisa katika makosa ya kumdhalilisha mtu, ni ukatili ambao mtu anatendewa na kumsababishia maumivu ya kiakili/ kihisia au hofu na mtu mwingine hawezi kutambua kuwa mwenzake ametendewa ukatili hadi mazingira  yatakapojitokeza na mtendwa kujieleza.

JE, unajua sheria inasema nini kuhusu kumshushia mtu hadhi, wakili Emmanuel Kiarri anasema  kifungu cha 138 D na 240 vya sheria ya kanuni za adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022 vinazuia kumkashifu au kumtukana na kumfanyia  mtu vitendo vya udhalilishaji.

“Vifungu vya sheria vipo wazi kabisa katika makosa ya kumdhalilisha mtu, ni ukatili ambao mtu anatendewa na kumsababishia maumivu ya kiakili/ kihisia au hofu na mtu mwingine hawezi kutambua kuwa mwenzake ametendewa ukatili hadi mazingira  yatakapojitokeza na mtendwa kujieleza.

“Mfano ukatili wa kisaikolojia ni matusi kwa njia ya maneno au ishara yenye lengo la kudhalilisha, vitisho na kutishia kufanya fujo, maneno ya kufedhehesha, kudharauliwa hadharani, kutishia kutoa siri, kuingiliwa faragha, kutishiwa kuuawa na wivu wa kupindukia vilevile ukatili huu unahusishwa na kufanyishwa kazi ngumu bila kupumzika.”

Mwanaspoti limefanya mahojiano na watu maarufu mbalimbali ambao kulingana na muonekano wa miili yao, wamekuwa wakikumbana na changamoto za kudharaulika katika jamii.


TAUSI MDEGELA-MUIGIZAJI

Msanii wa filamu na mfanyabiashara Tausi Mdegela anasema kutokana na kimo chake kifupi, kuna baadhi ya watu katika jamii na mitandao wanaona hastahili kufanya baadhi ya vitu.

Japokuwa anasema kwa sasa amezoea  kudhihakiwa na akiwa  anatimiza majukumu  yake anajisahau kujiona mfupi anakuja kujigundua wakati anafungua mlango, kwani hafikii.

“Nikitaka kufungua mlango ndio nakumbuka mimi ni mfupi, naanza kumuita dada yangu wa kazi anifungulie, nje na hapo sijiwazii kimo changu, napenda kufanya kazi kwa bidii na siangalii uigizaji pekee,” anasema.

Anaulizwa kitanda chako kina futi ngapi? Anajibu “Nina kitanda kikubwa lakini godoro naweka chini kwa sababu siwezi purukushani za kupanda na kushuka, lengo langu la kukinunua ni kumfanya binti yangu azoee mazingira hayo ili akienda kwa watu asione vitu vigeni.

Anaongeza “Ukiachana kitanda ndani kwangu hakuna viti vya kukalia, nimeweka zuria na mito kwani siwezi kujitesa kupanda juu, nimeamua kujikubali nilivyo, nitaishi maisha ya furaha na siyo kufurahisha watu, pia nikitaka kushona nguo nakata mita mbili.


Hataki unyonge kwa binti yake

Tausi amejaaliwa kupata mtoto wake kike jina lake Pavitrah, anasema kipindi cha nyuma alikuwa akienda kucheza na wenzake walikuwa wanamtania na kumwambia mama yake ana mwili mdogo na mfupi, jambo ambalo lilikuwa linamuumiza.

“Pavitrah mwanzoni alikuwa anakuja kusemelea anavyotaniwa na wenzake ananiambia mama wanasema wewe una kamwili kadogo na mfupi, nikawa namwambia mwanangu ni kweli mimi ni mfupi, ila nakupenda sana wakikwambia tena wajibu ndiyo mama yangu mfupi ila ni staa kuliko mama zenu.

Anaongeza “Siku moja akaenda kucheza wakaanza kumtania akawajibu kama nilivyomwambia, akarudi akanimbia mama nimewaambia kama ulivyonifundisha hawajarudia kunitania tena.


Changamoto za huduma za kijamii

Anasema kuna wakati akienda kupata huduma za kijamii sehemu kuna ghorofa kwake inakuwa ni ishu, kwani anaona kuna umbali mrefu kupanda ngazi.

“Hata kama kuna lifti lazima niwe na mtu ambaye anaweza akanisaidia kubonyeza zile namba za lifti kwani siwezi kufikia zilipo.

Anaongeza “Changamoto nyingine ninayoipata nikitaka kutoa pesa ATM sifikii kwenye mashine ile, hivyo nakuwa namuomba bodoboda wangu ama dereva bajaji anayeniendesha, sasa hiyo ni hatari muda wote kumtajia mtu namba yako ya siri, nashauri wahusika kwa kuwa mashine za kutolea pesa zinakuwa mbili moja waweke ya watu wafupi, ili na sisi tuwe na uhuru wa kutunza pesa zetu.

Nje na hilo anasema ni ngumu kuvuka barabara, kwani inakuwa shida kuonekana na magari marefu,

“Mfano unavuka ni usiku siyo rahisi dereva kukuona kwani hawezi kutazama chini.”


Jamii inavyomchukulia

Anasema kuna baadhi ya watu hawamchukulii kama binadamu anayestahili uhuru wake na kufanya anachokipenda, anakutana na changamoto ya kudharaulika kutokana na ufupi wake kupitia mitandao ya kijamii, huku wengine akiwasikia wakimsema vibaya.

“Unakutana mtu anasema huyu naye kwa nini anavaa hivi, sasa nakuwa najiuliza kwa nini wasivae wao vile wanavyoona nastahili kuvaa mimi, siku moja nilipanda basi nikawa naseng’enywa na wamama kwa kiluga cha kihehe, hawakujua mimi ni kabila lao, nikanyamaza kimya baada ya kufika kituo ninachoshuka nikawajibu kwa kihehe sijajiumba mwenyewe ni mpango wa Mungu, ikabidi washuke kuniomba msamaha,” anasema.


AOMBWA MSAMAHA BAADA YA UMARUFU

Anasema kipindi anajitafuta alikutana na kitu kilichomkatisha tamaa, ila akajikaza na kuweka nguvu kujaribu ishu nyingine ili mradi mambo yaende.

“Niliunganishwa na  mtu ambaye nilikuwa namuomba nafasi ya kuigiza, baada ya kufika eneo ambalo nilihitaji kukutana naye, nikapiga simu akapokea kisha akasema ndio wewe uliyesimama hapo nikamjibu ndio, akasema hakuna kazi kiukweli niliwaza mengi sana.

“Nikaondoka huku moyo wangu ukiwa na huzuni, nikampigia simu rafiki yangu alikuwa Tanga nikamwambia nahitaji niwe mnenguaji akasema sawa njoo Tanga ujaribu maisha.

“Ikafika muda nikaenda Tanga baada ya kufika huko rafiki yangu  aliniambia anafahamiana na  mzee  King Majuto (marehemu), ataniombea nikaigize naye, akampigia na kumuelezea ishu yangu akamwambia twende kwake, baada ya kufika pale akasema mmekuja na nguo za kuigizia, baada ya stori za hapa na pale na  kazi ikaanza siku hiyo hiyo.

“Hakuishia hapo akanichukua nikawa naishi naye nyumbani kwake na kunilea kama binti yake na kipindi hicho alikuwa maarufu sana, basi alikuwa akikutana na wasanii anawaambia huyo ni mwanangu mpeni nafasi ya kufanya kazi, nikawa napewa kipaumbele, katika maisha yangu sitakaa nimsahau yule mzee, apumzike kwa amani.”

Anasema alipopata  umaarufu akakutana mtu  aliyemdharau wakati anaomba nafasi ya kuigiza “Baada ya kuniona akaniomba msamaha, ila nilimwambia ukweli katika maisha yake asimhukumu mtu kutokana na uumbaji wa Mungu, bado yupo kwenye tasnia hiyo na akitaka nifanye naye kazi nitafanya, jambo la msingi nazingatia masilahi.”

Tausi aliwahi kuonekana gym akiwa na Loveness Tarimo ambaye ni mkufunzi wa mazoezi, analifafanua hilo kwamba ilikuwa ni matangazo na siyo  kitu kingine.

“Niliambiwa kuna tangazo nilipofika eneo la tukio ndio nikamuona Loveness, sasa nikapandishwa kwenye mashine za kukimbia mikono yangu ikawa haifikii sehemu ya kushika, nikapewa mpira ukawa mzito siwezi kuubeba, nilichokifanya nikakalia mpira basi shughuli ikaishia pale,”anasema.

Anasema siyo mpenzi wa michezo wala mazoezi, kwani haoni utakaomfaa kulingana na kimo chake”Ndio maana siwezi kufuatilia mambo ya mpira wala michezo ya aina yoyote zaidi ya uigizaji, unenguaji na MC.”


LOVENES TARIMO-MKUFUNZI WA MAZOEZI

Loveness Tarimo ni mkufunzi wa mazoezi ya ufiti pia anashiriki mashindano ya warembo watunisha misuli (miss fitiness)  mwaka 2019 alinyakua taji la Tanzania Miss Extreme.

“Changamoto ngumu nikiwa katika mkusanyiko wa watu inakuwa ngumu kuingia chooni kwani muonekano wangu wengi wanashindwa kuamini mimi ni mwanamke, vinginevyo niende na mtu.

Anaongeza “Nilienda Mwenge kununua hereni za kwenda kuvaa katika mashindano Kenya yaliyofanyika mwaka huu,  huyo mama muuzaji alikataa kuniuzia akidhani ni mwanaume aliyekengeuka, iliniumiza sana ila nikakosa cha kufanya, ikabidi niondoke, pia siwezi kutoka na mchumba wangu auti, maana naogopa tunaweza kuleta sintofahamu.

“Nilivyo ni kitu nimekuwa nacho, kwani nilianza kucheza mpira wa miguu baada ya kuona sioni kama nitafanikiwa nikaamua kujikita na mazoezi ya kutunisha misuli, hilo halifuti kuwa mwanamke, sasa atakayeamini aniamini, wanaobisha nawaacha sina cha kuwafanya.”


JULIAS CHARLES-MSANII

Mwingine anayepitia changamoto kutokana  na mrefu ni Julias Charles msanii anayefanya vizuri  kwenye tamthilia ya Huba, anacheza move za kupigana pia amewahi kuonekana katika wimbo wa Rose Muhando wa Secret Agenda.

Kutokana na urefu alionao anakumbana na changamoto mbalimbali akitaja usafiri kwake ni ishu, kwani gari la saizi yake linauzwa kuanzia Sh400 hadi 500 milioni na yanatengenezwa Japan au Ujerumani, uwezo huo kwa sasa hana bado hajajipata.

“Sijapata gari la saizi yangu hapa nchini ambalo naweza nikakaa kwa uhuru kama wengine,  kupanda daladala ni ngumu, kiti kinachoweza kunitosha ni kiti cha kati kwenye siti za mwisho nakuwa naweza kunyosha miguu yangu.

“Zamani nilikuwa nikikuta gari limejaa nilikuwa sipandi,mimi ni mrefu hivyo siwezi kusimama wala kumnyanyua mtu aliyekaa ili nikae mimi, ila usafiri wa ndege una huduma tofauti kuna siti za watu wa aina yangu.”

Anasema kwa sasa huwa anakodisha gari binafsi ama anachukua bodaboda kwenda sehemu anapotakiwa kufanya majukumu yake, pia hakai kwa kujiachia.

“Nikitaka kuingia ndani lazima nitainama mlangoni, kwa sababu bado sijajipata kujenga nyumba ambayo itakuwa ya ndoto zangu, kitanda ninacholalia  ni futi 8 kwa sita natengeneza kwa oda maalumu, viatu naagiza kutoka nje navaa namba 18 sawa namba 55 za viatu vya kawaida, ninachoshukuru nina marafiki nje ambao wananiletea, ila kwa mara ya mwisho kununua kwa pesa yangu ilikuwa Sh.200,000.

“Natumiwa viatu kutoka China, Canada, Marekani na marafiki zangu, Mungu anapokuumba tofauti anakupa na njia ya kufanya maisha yako yaende, nakumbuka zamani nilikuwa natembea bila viatu na sikumbuki kwa mara ya mwisho lini nilivaa kandambili zaidi ya sandozi ambazo pia naagiza kutoka China.


Ana miaka mitatu katika mapenzi

Anakumbuka akiwa na miaka 16 alikutana na wanawake watatu waliomzidi umri, baada ya kumuona wakaanza kucheka mmoja wao, akasema hata dunia iishe yote abakie Julias hawezi kukubali kuwa naye, maneno hayo yalimuumiza sana moyo wake.

“Kauli ile ilinifanya nijiulize maswali mengi sana, moyo wangu uliniuma kupita kiasi, nikajiapiza kwamba sitakaa nioe katika maisha yangu,ndio maana nimechelewa sana kuingia katika mahusiano.

Anaongeza”Tangu nimechekwa nikiwa na miaka 16 sikuwahi kuwa na mahusiano na nilianza nikiwa na miaka 27 na sasa nina miaka 30, mwanamke wa kwanza aliyenitoa uvulana wangu tulikuwa marafiki sana na alikuwa na watoto, kuna siku aliniambia ana hisia na mimi ikachukua siku mbili kumaliza kila kitu.

“Baada ya hapo nikapata safari ya kwenda Marekani ambako nilikaa zaidi miezi sita, akashindwa kunivumilia akapata mtu mwingine, mimi pia nikapata mzungu ila baada ya kurejea Tanzania umbali ukatufanya tuachane, kwa sasa jimbo lina mtu ingawa sieleweki, wadau wajue hivyo tu”.

Anaulizwa umewahi kutongozwa na mastaa wa kike? Anajibu “ Ndio ni zaidi ya watatu ingawa siwezi kuwataja majina yao, nawapenda mahusiano na watu wa kawaida pia siwatongozi maana nilishaapa sitawatongoza, kinachotokea mazoea yanazaa mahusiano.

“Zamani niliwahi kujifungia ndani  miezi mitatu,mimi ni mkimya vile jamii ilivyokuwa inaniona kama siyo mtu wa kawaida nilikuwa naumia moyoni, ila mama alikuwa ananiambia tembea mtaani lazima watu watakuzoea, nikaja kupata ujasiri baada ya kuanza kidato cha kwanza shule ya bweni, tulikuwa wanafunzi zaidi ya 1000 nilipendwa na kila mtu.

“Nikawa nacheza mpira wa kikapu, hilo pia likachangia kupata mashabiki ambao wananipenda na kunipa moyo, lakini bado haikuondoa kuwachukia wanawake, katika familia yetu mimi ni mtoto wa pili kati ya saba, mrefu nipo pekee yangu wenzangu wote wa kawaida hata baba na mama wapo kawaida tu.”

Anaulizwa unaweza ukawa mwanamke wa kimo kifupi sana? Anajibu” Siwezi kuoa mwanamke ambaye ananifikia magotini kwa urefu wangu nitakuwa namuonea, ila naweza nikaoa mwanamke anayefika kiunoni.”

Kuhusu ushabiki wa soka anasema anaipenda Simba, mastaa anaowakubali ni Aishi Manula, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin.

“Wachezaji wengi kwa sasa Simba ni wapya na majina yao ni magumu, ila huniambii kitu kuhusu kuishabikia timu hiyo kwa Yanga nawakubali Ibrahim Bacca, Dickson Job, Clatous Chama, kuhusu Aziz Ki kashuka inabidi ajitathimini kurejesha makali yake.”


LOVE -MSANII WA TAMTHILIA

Msanii anayefanya vizuri katika tamthilia ya Jua Kali jina la uigizaji anajulikana kama Love,  jina lake halisi ni Hallein Haman ni kati ya wanaoshambuliwa katika mitandao ya kijamii, akiposti picha yake baadhi wanamsema vibaya kutokana na muonekano wake.

Mara kadha amekuwa akisema “Najiamini, mimi ni mzuri kuliko wote, sijali wanachokomenti mitandaoni, siku wakiacha ujinga na kujitambua wataacha na kufanya vitu vya maana.”


SHERIA YA TANZANIA

Kwa mujibu wa Kifungu cha 157 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya Tanzania, mtu anayefanya udhalilishaji anaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka mitano, au faini, au adhabu zote mbili kulingana na uzito wa kosa.

Kifungu hiki kinahusisha vitendo vyote vya kusema au kufanya jambo linalomdhalilisha mtu, ikiwemo kumtukana au kumdhalilisha kwa maneno au kwa njia nyingine yoyote, ikiwa ni pamoja na kudhalilisha kwa sababu ya sura, mavazi, au hali ya nje ya mtu.


SAIKOLOJIA

Mtalamu wa saikolojia Charles Nduki, anasema wanaowajaji watu kutokana na mionekano wanakuwa wamepungukiwa na uelewa wa kihisia kujiwekea katika nafasi ya anayemtendea ingerudi kwake inakuaje.

“Ukiachana na hilo nyuma ya pazia wanakuwa na maumivu makali hivyo anakuwa anadhihaki wengine ili kujaribu kuponya makovu yake, wakishindwa kuelewa wanawaumiza wengine na kusababisha kuwaondolea kujiamini, kujichukia, kujiona hawapo sawa.

Anaongeza”Niliwahi kupokea kesi moja ya mtoto aliyejiua alikuwa wa kike ana umri kati ya miaka 14 au 15, alikuwa mnene, mfupi na  kilo 100, hivyo alikuwa anachekwa na wenzake shuleni, ikaenda akashindwa kuhimili akachukua maamuzi ya kukatisha uhai wake.

“Wazazi wakiona watoto wao wana changamoto ama mapungufu, ikitokea wanakosea jambo bora wawachape kuliko kutaja viungo vyao, ukiachana na hao kuna wengine ni jasiri hata ukimdhihaki kiasi gani, anakuwa hana muda na hayo.”