Koffi, Diamond waingia ‘location’

Koffi, Diamond waingia ‘location’

Muktasari:

Kollabo ya Diamond na Koffi itakuwa ya tano  kwa Diamond kufanya na wasanii kutoka  DR Congo kwani alishanfanya na Fally Ipupa (Inama), Ya Levis (Penzi), Innos B (Yope Remix) na mkongwe marehemu Papa Wemba (Chacun Pour Soi).

MSANII nguli wa muziki kutoka DR Congo, Koffi Olomide  na msanii wa muziki wa Bongo Fleva nchini Diamond Platnumz waingia 'location'.

Diamond na Koffi leo Jumatatu Novemba 23, 2020 video yao imesambaa kwa kasi mitandaoni wakionekana kupiga picha jongefu.

Kollabo ya Diamond na Koffi itakuwa ya tano  kwa Diamond kufanya na wasanii kutoka  DR Congo kwani alifanya na Fally Ipupa (Inama), Ya Levis (Penzi), Innos B (Yope Remix) na mkongwe marehemu Papa Wemba (Chacun Pour Soi).

Katika video hiyo wasanii hao wameonekana wakicheza kibwagizo kilichopo kwenye wimbo wa Mobimba uliojizolea umaarufu huku baadhi ya kamera zikiwa zimewazunguka.

Moja ya kivutio katika video hiyo ni namna Koffi alivyovalia mavazi yake ambapo yameonekana kuwa gumzo na baadhi ya mashabiki waliona video hii akiwemo rebby happy's, ameandika "Mi naangalia nguo za koffi".

Wakati Ibbu phd's ameandika “Nilijua tu huyu mwamba atamvalisha kijana wetu shuka nilijua tu,”.

Focus gel's ameandika ‘Kofi na hizi nguo zake jamani kafanya nimkumbuke mama Rwakatare,"

Msanii huyu amekuwa akivaa mavazi tofauti yakiwemo yanayoonekana kama ya  wanawake.

Koffi alitua nchini siku tatu zilizopita na kupokelewa na mwenyeji wake Diamond, ambao kwa nyakati tofauti waliweka wazi kwamba wana kazi wanatarajia kuifanya ya kimuziki.

Juzi pia wawili hao walionekana wakiwa studio  na prodyuza Laizer wakiingiza sauti.

Baadhi ya mashabiki wameonekana kuwa na shauku ya kuuona na kuusikia wimbo huo, ukizingatia kwamba wote ni wakali katika muziki japokuwa Diamond alisema yeye ni Prince kwa Koffi.

_________________________________________

By NASRA ABDALLAH