Kinata MC: Kwa singeli hili lazima tutoboe

Monday June 21 2021
kinata pic

KWA sasa singeli inayotamba mtaani ni ile ya ‘Do Lemi Go’, singeli iliyoimbwa na msanii Kinata MC akimshirikisha Ibrah kutoka pale lebo ya Konde Gang.

Moja ya kivutio katika wimbo huo ni lugha ya Kiingereza iliyotumika na katika sherehe mbalimbali kwa sasa goma hili lazima lipigwe na watu kuinuka kwenye viti.

Mwanaspoti imefanya mahojiano na Kinata MC na kuzungumza mambo mbalimbali na kubwa ni kutaka kujua nini alifikiria kuimba wimbo uliochanganywa na lugha ya Kiingereza.

Alisema, moja ni ubunifu na pili ni kutaka kuutangaza muziki huo kimataifa kutokana na ukweli nchi nyingi zinazungumza na kusikia Kiingereza.

“Ifike mahali muziki wetu sasa upae kimataifa, wazungu wasiishie tu kupenda midundo bali waelewe hata kinachoimbwa ndani yake na ndio maana niliamua kuweka na Kiingerea mle ndani.

“Kwa kufanya hivi naamini siku moja singeli tutatoboa tu kimataifa na nimeamua kujikita kuimba nyimbo zangu kwa kuchanganya lugha ya Kiingereza mpaka wajue hawajui,” alisema Kinata MC.

Advertisement

Kuhusu hatua ya kuimba na msanii wa Konde Gang, alisema imemsaidia kumtangaza kutokana na ukweli ni lebo kubwa na hivyo kuchangia kusukuma muziki wake na kumfanya ajulikane zaidi.

Alibainisha kabla ya wimbo huo alitoa nyimbo sita huko nyuma, lakini huu umeenda sana sababu aliyoitaja ni umechangiwa na Konde Gang kuutangaza.

Advertisement