Kiini cha mgogoro wa Diamond Platnumz, Harmonize hiki hapa

Muktasari:

  • Miaka miwili iliyopita, Harmonize aliachana na lebo ya WCB, akasema menejimenti ya WCB ilimtaka staa huyo wa umakondeni alipe Sh500 milioni aweze kung’oka.

Miaka miwili iliyopita, Harmonize aliachana na lebo ya WCB, akasema menejimenti ya WCB ilimtaka staa huyo wa umakondeni alipe Sh500 milioni aweze kung’oka.

Ametumbua jipu, kwamba ilibidi auze nyumba zake tatu apate pesa za kuwalipa WCB. Kwamba yalikuwa masharti ya mkataba, Harmonize akitaka kuondoka WCB, alipe Sh500 milioni na gharama za utengenezaji wa nyimbo zote.

Hivi karibuni Harmonize amesema alihaha kupata fedha za kulipa WCB. Kampuni ya vinywaji ya Sayona na Benki ya CRDB ndio walimpa fedha za kukamilisha Sh500 milioni. Hata hivyo, akatakiwa aongeze Sh100 milioni, alizopewa na meneja wake, Sebastian Ndege.


Mchanganuo wa 2021

Harmonize aliuza nyumba yake ambayo haikuwa imekamilika kwa Sh100 milioni. Sayona wakampa Sh200 milioni, halafu CRDB wakampa Sh200 milioni. Seba akaweka Sh100 milioni. Jumla Sh600 milioni.

Lipi sahihi? Nyumba tatu alizouza mwaka 2019 au fedha za CRDB, Sayona na Seba? Mpaka hapo utaona kwamba kuna mahali Harmonize hasemi ukweli.

Sisahau taarifa ya mwaka huu, Harmonize alisema angeongea kila kitu. Kama mwaka huu ndio alisema ukweli, basi 2019 aliongopa.

Hata hivyo, lipo ambalo halibishaniwi. Ni Harmonize kulipa Sh500 milioni. WCB hawajawahi kukanusha. Kiulizo kipo kwenye Sh100 milioni.

Mwaka 2019, Harmonize alisema alilipa WCB Sh500 milioni. Mwaka huu, amesema alizolipa ni Sh600 milioni. Kwa nini mwaka 2019 alipunguza?

Stori ya Harmonize na Bosi kubwa wa WCB, Diamond Platnumz ina matege mno. Utaona inazingirwa na wivu, uongo, tamaa na kufanya kazi kiswahili.

Kwa nini waligombana? Jibu ni vipengele vya mkataba (contractual terms). Kuna mkataba (makubaliano) yenye utashi wa pande zote zenye kusaini na ulaghai au shuruti. Wanasheria huliweka vizuri kwa lugha yao. Huita duress contracts, yaani mikataba isiyo na utashi au ufahamu.

Tafsiri ya duress ni nguvu, lazima au ushawishi wa kumfanya mtu atende jambo bila ridhaa yake. Mathalani, mtu anasaini mkataba akiwa ameshikiwa bunduki, anaambiwa asiposaini atauawa.

Anatekwa mwanaye, mkewe au mumewe, mzazi wake au ndugu yake, halafu anaambiwa asaini mkataba, vinginevyo mateka atauawa. Mikataba ya aina hiyo ni duress.

Kusaini mkataba na mtoto au mtu asiye na ufahamu wa kutosha kuhusu vipengele vya mkataba, hutafsiriwa kuwa aina nyingine ya duress.


Mwaka 2015

Harmonize ni kijana mdogo. Masikini sana. Ndoto yake ni kuwa mwanamuziki. Anaishi mjini Dar es Salaam na Diamond Platnumz ni staa aliyekaa juu ya nchi.

Huwezi kupata picha ya duress katika mikataba ya wasanii kama hutavaa viatu vya msanii underground anayetamani kutoka kimuziki. Ukimuuliza Afande Sele alivyomwona Sugu enzi hizo akitaka asaidiwe kimuziki, akiwa mkweli, utaelewa maana yake.

Jicho la msanii underground kwa msanii aliyefanikiwa ni kama malaika wa pepo. Kwa mantiki hiyo, mwaka 2015, Harmonize ambaye hakuwa akijua chochote, alimwona Diamond ni malaika wa pepo yake.

Jiulize, siku ya kiyama unaona jehanamu ilivyo halafu unaitwa na malaika wa pepo, anakwambia saini mkataba uingie, utapoteza muda? Tusiongopeane, utasaini haraka haraka na kuingia.

Ukishaingia peponi na kuijua pepo ilivyo, ndipo unaweza kumwona malaika wako wa pepo alikupiga, kwamba ulistahili zaidi.

Kumbuka pia kuwa wakati unasaini mkataba wa kuingia peponi, utakuwa na furaha iliyopitiliza, umakini hautakuwepo. Utataka usaini ili ukajionee yaliyomo. Ufaidi simulizi za mito ya maziwa na asali.

Njoo kwa Harmonize. Hajui pepo ya muziki ilivyo ila alifahamu kuwa Diamond yupo peponi na ni malaika wa pepo. Akatokeza kumvuta peponi, unadhani Harmonize angedengua?

Harmonize alipoambiwa na Diamond asaini mkataba aingie kwenye pepo ya muziki, angelaza damu? Bila shaka, alisaini akiwa na furaha iliyopitiliza.

Mwaka 2015 akatoa Aiyola, jamii ikamjua. Mwaka 2016 Bado ilifuata kisha Matatizo. Mpaka hapo Harmonize alikuwa ameshaijua pepo ya muziki. Hakuwa mshamba tena. Kipindi hicho angeambiwa asaini upya mkataba wake na WCB, Kuna vipengele angevikataa. Kumbe sasa, kiuhalisia, mkataba wa Harmonize na WCB, kwenye fikra za Harmonize, ulivunjika tangu mwaka 2016.

Tafsiri nzuri ya mkataba wa duress ni ule ambao anayesaini, muda mrefu unaofuata akiambiwa asaini upya, lazima akatae. Ni kama Harmonize, akili yake ya sasa inamwambia alikosea kusaini.


Dhambi ya mkataba

Mkataba ni makubaliano ya kisheria. Na asili ya mikataba ya muziki ni wajibu wa kila upande. Unachotoa na unachoingiza. Masharti lazima yawe sawa kuhusu mzigo ambao kila upande utabeba kwa kuvunja mkataba.

Mathalani, iliandikwa kuwa Harmonize alitakiwa kulipa Sh500 milioni na kurejesha gharama zote za nyimbo ambazo zilirekodiwa chini ya Wasafi ili kuvunja mkataba.

Sawa! Je, wajibu wa Wasafi kuvunja mkataba ni upi? Kama wao wangeamua kuachana na Harmonize, wangepaswa kumlipa nini? Mkataba wa masharti ya upande mmoja, ni aina nyingine ya duress.


Harmonize kasaidiwa?

Kampuni ya kusimamia muziki huwekeza katika maeneo ya aina mbili; label (utengenezaji na usimamizi wa muziki) na imprint (masoko ya muziki na mwanamuziki).

Kampuni kama Wasafi inapomchukua msanii, inabeba maudhui ya kutengeza na kusimamia muziki pamoja na masoko. Hufanya hivyo kupata faida. Sio msaada!

Wasanii wengi chipukizi wanapochukuliwa na mastaa wakubwa, hudhani wanasaidiwa, hivyo hunyenyekea na kusaini kiholela. Wafahamu kuwa hakuna recording company ya usamaria wema. Husaka fedha.

Kampuni inapofikia hatua ya kukusaini, maana yake huona faida ndani yako, kwa hiyo hupaswi kwenda kikondoo, kudhani unasaidiwa. Ni biashara. Soma vingele bila ushawishi, amua kwa maisha yako. Tena, shirikisha wanasheria.

Kingine, recording company nyingi hutaka kummiliki msanii muda mrefu, ipo hivyo. Mikataba ya muziki huwa haiendi kwa umri, bali kazi.

Wasiseme unasainiwa kwa miaka 20, kama WCB na Harmonize, bali, mnatengeneza albamu ngapi au nyimbo ngapi. Siku hizi soko la kidigitali, zinaangaliwa nyimbo zaidi kuliko albamu.

Suge Knight alipomtoa Tupac jela mwaka 1995 na kumlipia dhamana ya dola milioni moia, Tupac hakusaini umri wa kukaa Death Row Records miaka mingapi, bali walisaini albamu tatu.

Februari 2014, 50 Cent, alipokuwa anasaini mkataba na kampuni ya usambazaji ya Caroline, inayomilikiwa na taasisi ya Universal Music Group (UMG), alisema, alikuwa bado anadaiwa albamu moja na lebo ‘joint’ ya Shady-Aftermath, lakini alikubaliana kiroho safi na Dre pamoja na Eminem.

Kama Harmonize na Wasafi wangekubaliana idadi ya nyimbo au albamu, wala wasingeingia kwenye mgogoro. Wangeachana salama. Kama kungekuwa na idadi ya nyimbo anadaiwa, Harmonize angeingia studio kumalizia. Miaka 20 au 10 ya nini? Saini idadi ya nyimbo, zikitimia, kama kuna haja, mnasaini tena.