Kasheshe lote la Harmonize Kenya

Wednesday May 04 2022
kasheshe pic
By THOMAS MATIKO

ILIKUWA wikiendi ndefu kwa Wakenya. Wikiendi ya siku tano. Ilianza na siku mbili (Ijumaa na Jumamosi) kutangazwa mapumziko ili kutoa heshima kwa marehemu Rais wa awamu ya tatu, Mwai Kibaki.

Ikafuata Jumapili, Mei Mosi, ikiwa ni Sikukuu ya Wafanyakazi. Na kutokana na hiyo kuangukia wikiendi, kidesturi hutakiwa kusherehekewa kwenye siku ya kazi, hivyo nayo jana Jumatatu ikawa ni sikukuu nyingine. Wikiendi ndefu inamalizika leo ikiwa ni sikukuu ya Eid-Ul-Fitr nchini humo kama ilivyotangazwa na Waziri wa Mipango na Masuala ya Ndani, Fred Matiangí. Kwenye siku hizo tano, Wakenya waliwekwa bize na vituko kibao. Ukiachana na malumbano ya hadharani kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto, staa wa Bongofleva, Harmonize na mchekeshaji Eric Omondi vilevile nao walitrendi.


HARMO AJIKUTA SELO

Alhamisi wiki iliyopita, Harmonize alitua Nairobi kwa ajili ya kutumbuiza kwenye shoo ya Afrika Moja iliyofanyika Jumamosi uwanjani KICC. Shoo hiyo iliandaliwa na mapromota Melamani Ltd. Hata hivyo shoo hiyo iliishia kuharibika na kuwaacha mashabiki wengi na hasira baada ya kuingia gharama kubwa ya kununua tiketi. Tiketi za kawaida ziliuzwa Sh2,000 (Sh 40,000), zile za VIP Sh5,000(Sh100,000) na VVIP Sh8,000 (Sh160,000)

Shoo hiyo haikubamba ikishindwa kuwavutia mashabiki huku utumbuizaji wa Harmonize aliyekuwa staa mkubwa ukishindwa kuwakosha.

Advertisement

Baada ya kufanya vitu vyake KICC, Harmonize alitakiwa kutumbuiza kwenye klabu ya Captain Lounge iliyoko Mombasa Road, Athi River.

Huko Harmonize alifika lakini baada ya dakika tano akaondoka. Mashabiki wengi waliokuwa wamelipia viingilio vya Sh1,000 (Sh20,000) wakashikwa na hasira na kutaka kumchapa na hapo kusababisha vurugu. Hata hivyo, mabaunsa wake pamoja na wale wa klabu walimwokoa huku maofisa wa polisi wakifika na kuwatimua mashabiki waliozua vurugu.

Harmonize alifanikiwa na kurejea hotelini. Hata hivyo, asubuhi ya Jumapili alikamatwa na maofisa wa polisi walioongozwa na Mkurugenzi Captain Lounge, Jor Barsil na kuzuiwa Kituo cha Polisi cha Kileleshwa.

Barsil alitaka Harmonize amrejeshee fedha zake akidai kuingia hasara kubwa baada ya jamaa kushindwa kutumbuiza lao sivyo amfikishe mahakamani. “Niliwalipa Melamini Sh450,000 (Sh9 milioni) ili Harmonize aje kwenye pati yetu kujumuika na mashabiki na kutangamana nao kwa muda wa lisaa limoja na nusu. Lakini alipofika, hakumaliza zaidi ya dakika tano na ndipo mashabiki wakazua rabsha alipoondoka wakidai warejeshewe fedha, “ alisema Barsil.

“Nami nikalazimika kuwaleta polisi wamkamate sababu aliniingiza hasara. Nilitengeneza jukwaa kwa Sh1 milioni ukiongeza na Sh300,000 nilizotumia kwenye matangazo ya pati.”

Kando na Captain Lounge, klabu zingine zilizodai kumlipa kwa ajili ya hafla kama hiyo ya meet and great (kukutana na kutengamana na mashabiki) ila hakutokea ni pamoja na Cocorico club na Volume Club Mombasa inayomilikiwa na Gavana wa zamani wa Nairobi, Mike Sonko.


ALIA NA ERIC OMONDI

Kwenye sarakasi lote hili, mchekeshaji Eric Omondi alihusika huku akiwa ndiye mwenyeji wa Harmonize na miongoni mwa waliohusika kumleta Kenya. Harmonize alipokamatwa, Omondi alidai staa huyo aligoma kuhudhuria meet and greet katika klabu hizo licha ya kulipwa. Omondi alidai kwa kuhofia kuwa Harmonize alikuwa na mpango wa kusepa na kurejea Tanzania aliwashurutisha wamiliki wa klabu hizo kufanya mpango akamatwe.

“Harmonize alitaka kurudi Tanzania na hiyo ingeniletea noma. Brand yangu ingeshuka. Ndio sababu tulifanya mpango akamatwe,” Omondi alidai sakata lilipolipuka.

Hata hivyo, Harmonize alikana kupokea fedha zozote kutoka kwa klabu yoyote huku akimgeuzia kibao Omondi.

“Eric Omondi namuona ni mtu mwenye heshima kubwa kwenye tasnia. Kwa hiyo akiniomba nimsapoti siwezi kukataa. Hata aliponiambia anataka tufanye hiki na kile nilimwambia aje Tanzania,” Harmonize alieleza baada ya kuachiliwa.

Harmonize alieleza baada ya kuachiliwa.

“Nikamwalika nyumbani tuyapange. Nilimwamini hata nilipokuja huku niliamini ataweza kuniunganisha na watu wengine. Lakini kumbe amekuwa akitumia hiyo vibaya.

“Anakuchukua pesa akiwaambia Harmonize atakuja. Captain Lounge aliniambia kakabidhiwa yeye tupitie tu mashabiki wanione. Sikujua kakusanya hela. Klabu kama Cocorico aliniambia kamfungulia dadake akaniomba nipitie pale baada ya shoo, asubuhi ndio nimefuatwa eti nimekataa kufanya appearance baada ya Eric kukusanya hela.”


SONKO AINGILIA

Huku mtafaruku huo ukiendelea Sonko anayemiliki klabu ya Volume One, Shanzu, Mombasa ambaye naye Harmonize alitakiwa kufika kwa ajili ya shoo, alipokea simu kutoka kwenye kituo hicho na kufika huko. Kuwasili kwa Sonko Kileleshwa saa nane mchana ndiko kulibadilisha upepo.

“Kulikuwa na ishu kidogo, ndio nikaitwa kutoa ufafanuzi. Kuna klabu alizopaswa kutumbuiza lakini hakuweza kwenda kutumbuiza sababu sio yeye ambaye alisaini mikataba na klabu hizo. Ni mabroka (madalali) wengine, wanaochukua pesa klabu zingine halafu wanashindwa kutimiza malengo. Si wajua Nairobi vijana lazima wajitafutie. Ni sisi tu Volume Club - Mombasa ndio tulikuwa tumesaini naye mkataba. Ilikuwa ishu ndogo tu, lilikuwa suala la mkanganyiko wa mawasiliano,” alifafanua Sonko.


HARMONIZE ARUDISHA PESA

Kwenye utatuzi wa mtafaruku huo baada ya Sonko kuingilia kati, Harmonize pamoja na Eric walilazimika kuwarejeshea wamiliki wa Cocorico Sh300,000 (Sh 6milioni) zilizokusanywa na msheshi huyo kwa ajili ya meet and great. Vile ile Harmonize aliingia mfukoni na kurejesha Sh450,000 (Sh9 milioni) za Captain Lounge. Hela alizokuwa amepokea kutoka Club Volume hakurejesha badala yake alisafiri hadi Mombasa baada ya kuachiwa kwa ajili ya shoo usiku wa jana.


HARMONIZE, ERIC WAYAMALIZA

Licha ya kukuru kakara zao ikiwemo Omondi kudai kuchapwa ngumi na Harmonize alipokuwa kituoni kumnusuru kituko alichokana mwanamuziki huyo akisisitiza, angewezaje kufanya hivyo mbele ya polisi, wawili hao waliishia kuyamaliza.

Advertisement