KANUMBA: Maisha ya Bongo Movie yalivyobadilika baada ya kuondoka

Muktasari:
- Ni kwa nini? Ni kwa sababu Kanumba ni mmoja wa wasanii wa Bongo Movie walioleta mabadiliko makubwa kwenye tasnia hiyo nchini.
IMESHATIMIA miaka 13 sasa tangu kifo cha aliyekuwa muigizaji maarufu nchini, Steven Kanumba. Kila mwaka anakumbukwa na familia yake, waigizaji wenzake, wadau na mashabiki wa kazi za Bongo Movie.
Ni kwa nini? Ni kwa sababu Kanumba ni mmoja wa wasanii wa Bongo Movie walioleta mabadiliko makubwa kwenye tasnia hiyo nchini.
Kazi zake zilipendwa na watu wa rika zote na alipata nafasi ya kucheza filamu hadi nje ya nchi na kushirikiana na wasanii wakubwa wa kimataifa hasa Nigeria wakiwamo mwanadada Mercy Johnson. Filamu zake kali ni kama ‘Dar to Lagos’, ‘This Is It’, Danger Zone, She is My Sister na Family Tears.
Tangu kifo chake kilichotokea April 07, mwaka 2012, Bongo Movie imepitia mabadiliko mengi makubwa na madogo na tofauti na ‘enzi zake’ pamoja na wasanii wengine kama Jacob Steven ‘JB’, Raymond Kigosi ‘Ray’, Blandina Chengula ‘Johari’ na wengine wengi, ni wazi yapo ya kuvutia yameibuka na kuwafanya watu wengi kujiingiza kwenye sanaa hii baada ya Kanumba na wenzake kuwatengenezea njia.

FILAMU HADI TAMTHILIA
Kipindi cha kanumba tamthilia zilianza kufifia na kutawaliwa na filamu zaidi. Ushindani na kiwanda cha filamu cha Nigeria na Ghana ulikuwa mkubwa na kila msanii Bongo aliingia kwenye filamu na zilikuwa zinalipa.
Hata hivyo, baada ya Kanumba kufariki dunia, miaka michache baadaye soko la filamu lilionekana kushuka na ujio wa tamthilia kutoka mataifa ya nje ikiwamo Kenya kama Celina na Pete, Zambia tamthilia kama Mpali, Nigeria, Uturuki, China, Mexico, Colombia, Uphilipino, India na nchi nyingine.
Hizo zikaibua tamthilia za Bongo kama Huba, Siri, Jua Kali, Kombolela, Bunji, EONII, Mawio, Mzani wa Mapenzi, Saluni ya Mama Kimbo na nyingine nyingi ambazo zimekuwa zikiwavutia mashabiki wengi.

MAMBO KIDIGITALI
Tasnia hii pia imebadilika kutoka kizazi cha kuuza DVD na CD kipindi cha marehemu Kanumba na ziliuzwa madukani na mitaani na wengi walikopi nakala kwenye vibanda vya kuuzia CD na watu wengi walizitazama, lakini sasa ni kidigitali zaidi na kazi nyingi za wasanii zinapatikana katika mitandao ya kijamii kama YouTube, Azam Maxi, DSTV ShowMax na platform nyingine nyingi.
UZALISHAJI UMEKUA
Mabadiliko ya teknolojia yamesababisha mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya Bongo Movie na ni wazi kama Kanumba angekuwepo hadi sasa kushuhudia mabadiliko haya kazi zake zingekuwa bora kutokana na kipaji chake.
Vifaa vya kurekodia filamu vimekuwa vya kisasa, waongozaji, waigizaji, wahariri wa kazi na mambo mengine yanazingatia ubora na baadhi ya kazi zinaonyesha wazi mambo yamebadilika.
Tamthilia zinazoonyeshwa katika vituo mbalimbali vya runinga ni dhihirisho tosha watu wamejipanga na mambo yanazidi kunoga, tofauti na zamani na kamera zilikuwa chache, wataalamu hawakuwa wengi na hivyo, uzalishaji haukuwa na ubora. Hata stori zilizokuwa zikitungwa hazikuhitaji mazingira magumu ili wasishindwe kuzalisha, lakini sasa uwepo wa teknolojia kumerahisisha kuonyesha uhalisia wa stori kwani hata kusafiri wasanii wanasafiri na wanafanya vizuri.

TUZO
Enzi zake, Kanumba aliwahi kushinda tuzo kadhaa ikiwamo ya Mini Ziff kutoka Zanzibar kwa filamu yake ya ‘This Is It’ kushinda.
Pia alishinda tuzo za Mwigizaji Bora mwaka 2006, 2007 na mwigizaji bora wa mwaka 2007/8.
Yeye pamoja na wasanii wenzake kipindi hicho, hawakuwa na tuzo nyingi na walitegemea zaidi mauzo ya kazi zao, lakini kwa sasa kumeibuka tuzo nyingi ndani na nje ya nchi na wasanii wamekuwa wakifaidika nazo.
Tanzania People’s Choice Awards (TPCA) hizi ni tuzo ambazo zinaandaliwa na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) likishirikiana na taasisi mbalimbali.
Baadhi ya wasanii kama Elizabeth Michael (Lulu), JB, Ray, na wengine walinyakua baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye tasnia hiyo.
Nyingine ni Zanzibar International Film Festival (ZIFF) tuzo hizi hutolewa kila mwaka ikiwa na vipengele vinne, filamu bora, Muigizaji bora, uandishi bora na sinematografia na baadhi ya wasanii kama Catherine Credo, Amil Shivji wamechukua tuzo hizo.
Nyingine ni za Steps Entertainment Awards, Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA) na nyinginezo.

WANAPITA MULE MULE
Ni wazi wasanii wengi wa kiume waliibuka ili kushika nafasi ya Kanumba ambaye aliiteka tasnia ya filamu. Hata hivyo, wakaja wengi na kufanya kazi kwa bidii na baadhi wameenda mbali na alipoishia Kanumba hasa kutokana na uwepo wa teknolojia mbalimbali kwenye uzalishaji na usambazaji wa kazi zao.
Wasanii hao ni kama Isarito, Gabo, Rammy Galis na kazi zao zinatamba mjini kama ilivyokuwa kwa Kanumba.
WAGENI
Ukuaji wa Bongo Movie ulianza kipindi cha Kanumba na waigizaji wa nje pia walikuja kushirikiana naye wakiwamo Mercy Johnson, Emmanuel France, Nkiru Silvanus, Ramsey Nouah na wengine.
Hata hivyo, kwa sasa wamezidi kuongezeka waigizaji kutoka mataifa mbalimbali ikiwamo Kenya, Uganda, Rwanda, Nigeria na wazungu pia wamekuwa wakionekana kwenye kazi za Bongo Movie.
Watu wa tasnia toifauti pia wamekuwa wakiingia Bongo Movie na kuonyesha wazi inazidi kukua. Wachezaji mpira kama Haruna Niyonzima na wengine.
Mwaka 2018, muigizaji Wema Sepetu alimleta muigizaji maarufu kutoka Ghana, Van Vicker aliyemshirikisha kwenye tamthilia yake iliyokwenda kwa jina la D.A.D.
Hata hivyo, msanii huyo hakuishia hapo na mwaka 2022 alikuwa miongoni mwa waigizaji kwenye tamthilia ya Jua Kali inayoongozwa na prodyuza mwanamama, Lamata Leah.
Ukimuondoa huyo wapo pia wazungu kwenye tamthilia ya Mawio, Yulia Bays na Mario Zungu na Mzambia Cassie Kabwita aliyeigiza kama Kai.
Wapo pia baadhi ya wasanii wa Tanzania ambao wamepata madili ya kuigiza nje akiwemo Othman Njaidi maarufu kama Patrick Kanumba.
Kwa sasa yupo kwenye tamthilia ya “Sultana” inayorushwa na Citizen TV ya Kenya, akicheza kama Jabali Junior mhusika mkuu katika mfululizo huo.

WASIKIE HAWA
Msanii mkongwe wa Bongo Movie, Shamila Rashid Ndwangila maarufu Bi Star alisema “Sisi ndio tulimpeleka Kaole, tulikabidhiwa na Mtitu Gemu alitukabidhi vijana wawili Kanumba na Set alisema tufanye muvi nao tukifanya tutafika tunapopataka kwa sababu Bongo Movie ina pesa,” alisema na kuongeza
“Ni muigizaji ambaye alikuwa bora na pengine bado tunaendelea kumkumbuka kutokana na uwezo wake sisi tunaomjua tangu anaanza alitamani kufanya makubwa ndani ya muda mchache aliodumu kwenye tasnia.”
Kwa upande wa msanii wa Blandina Changula maarufu Johari alisema “Bado nina machungu makubwa nashindwa kuzoea ikifika ile siku naona kama amekufa jana lakini ukweli ni miaka 13 sasa tangu Kanumba atutoke nakumbuka vitu vingi sana,”
“Harakati za sanaa ilipofika inaniuma kutokana aliipambania sana tasnia na sasa inalipa ndio hivyo hayupo, tulifanya tasnia hii ifike mahali fulani ingawa hatukufikia malengo makubwa ya kimataifa zaidi.”