Jux: Mimi kuoa? Bado sana

New Content Item (1)
New Content Item (1)

MSANII wa muziki wa RNB, Juma Mussa ‘Jux’ amedai kwa sasa bado hajafikiria mipango ya kufunga ndoa kama baadhi ya watu wanavyomtaka.

Jux amepiga stori na Mwanaspoti na kusema kuwa hawezi kukurupuka kuoa au kufuata maneno ya watu wa mitandaoni wanaosema si muoaji na kazi yake ni kukaa na wanawake muda mrefu na kuachana nao.

“Ni suala jema na ambalo linatakiwa lipewe nguvu na Mwenyezi Mungu pamoja na juhudi zangu. Nikisema Mwenyezi Mungu ni kumpata mtu ambaye ni ‘right choice’ kama mke ambaye nitaishi naye na sio kuoa kwa uamuzi wa mama au watu wa mitandaoni, yaani sitaki kukurupuka kwenye kuoa

“Unajua kuoa ni kujifunga kabisa huyo ni wa milele ingawa inatokea bahati mbaya mtu unaweza ukaacha mwanamke, lakini inabidi uchague chaguo ambalo unaweza ukaishi nalo. Isiwe unaoa kwa sababu ya ushawishi wa watu, mimi siwezi kuoa kwa mtindo huo na hata mama yangu mzazi huwa ananipigia kelele sana kwenye  suala kuoa, lakini huwa namuelewesha anaelewa,” alisema Jux.

Pia alisema kuwa hapendi kumchukua mwanamke na kuzaa naye halafu wakija kutengana mtoto analelewa na mwanamke mwingine, hivyo lazima aangalie maisha ya mtoto yanakuwaje ndio afikirie kuzaa.

Kutokana na hali hiyo, Jux alisema ndio maana huwa anakaa muda mrefu na mwanamke na akiona hawaendi sawa humwambia mapema wasitishe uhusiano.

Alisema anapenda Mungu amsaidie apate mtoto akiwa kwenye ndoa na ikitokea nje ya ndoa atajitahidi huyo mwanamke amuoe tu japo sio dhamira yake kuzaa nje ya ndoa .