Joti ashtukizwa tuzo za HAPAWARDS
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Joti amesema ushindi wa tuzo hauzoeleki ukiwa stejini, hivyo ameruka viunzi vyote na kuweza kupata ushindi wa kuwa mchekeshaji bora wa kiume.
MCHEKESHAJI mahiri nchini, Joti ameshukuru kupata tuzo ya Hollywood And African Prestigious Awards (HAPAWARDS 2024) kwenye kipengele cha mchekeshaji bora wa mwaka kupitia filamu yake ya komedi ya 'Maharage ya Mbeya'.
Akizungumza na Mwanaspoti, Joti amesema ushindi wa tuzo hauzoeleki ukiwa stejini, hivyo ameruka viunzi vyote na kuweza kupata ushindi wa kuwa mchekeshaji bora wa kiume.
Joti katika kipengele hicho cha mchekeshaji bora alikuwa anagombania na wachekeshaji wengine ambao ni Masanja Mkandamizaji na Tin White.
Amesema Joti aliposikia ameingia katika ushindani wa tTuzo haikuwa kazi rahisi kwake, kwani anaujua uwezo wa Masanja na Tin White.
"Namshukuru Mungu kupata hii tuzo, japo ni za kushtukiza, yaani unapewa taarifa kuwa umeingia katika tuzo bila hata ya kupigiwa kura, tumezoea kupigiwa kura hii ni unachaguliwa na kupewa taarifa," amesema Joti na kuongeza;
"Komedi yangu ya Maharage ya Mbeya, ile ya kiboga ndio imenipa ushindi, ushindi ambao hauzoeleki ukiwa stejini, hivyo nimeruka viunzi vyote na kuweza kupata ushindi wa kuwa Mchekeshaji Bora wa Kiume. Tanzania na hizi tuzo zinaandaliwa nje ya nchi basi mimi ni wa dunia."
Hata hivyo, Joti amesema huwa anafurahia komedi zote anazocheza zikiwa za uhusika akiwa amevaa gauni, Babu, Andunje (mtoto mdogo) na zingine nyingi.
Tuzo za HAPAWARDS zimekuwa zikitolewa kwa miaka saba mfululizo huko Marekani, lakini kwa mwaka huu kwa mara ya kwanza zimefanyika Afrika kwenye ukumbi wa The Super Dome Masaki.