Jose Chameleone akamata soko la muziki miaka 19 Afrika

Muktasari:

  • Huu ndio umekuwa ujanja wake wa kumfanya kuwa kivutio kwa wengi wanaompenda na kumchukia.

Mwanamuziki Jose Chameleone ameendeleza ubunifu wa sanaa yake jambo ambalo limemfanya aendelee kutamba. Anapenda kujifagilia na pia kuonyesha mali zake na vitu vingi vya bei mbaya anavyomiliki.

Huu ndio umekuwa ujanja wake wa kumfanya kuwa kivutio kwa wengi wanaompenda na kumchukia.

Uwezo wake wa kuivuta na kuiteka hadhira nao umeyafanya makampuni mengi kupenda kufanya kazi naye kwa sababu ya soko analovuta.

Chameleone aliyeanzia sanaa yake ya  muziki jijini Nairobi, amekuwa kwenye gemu kwa zaidi ya miaka 19 sasa.

Kwa miaka yote hiyo ambayo kwenye gemu, Chameleone amefanikiwa kujiundia brandi ya uhakika. Hakosi shoo iwe ni ndani, au nje ya taifa lake kila wikendi. Itakumbwa  Machi 2014, aliweka historia ya kuwa mwanamuziki wa kwanza kujaza Uwanja wa Lugogo, Oval Uganda na mashabiki 40,000.

Brandi yake imemfanya kuwa miongoni mwa wasanii ghali zaidi Afrika Mashariki. Chameleone huchaji USh6 milioni kwa shoo za ndani ya nchi kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la Hipipo la Uganda. Mwaka juzi jijini Kampala alipiga shoo ghali zaidi kuwahi kutokea katika ukanda huu, iliyoitwa ‘One mic, ‘One man Show’.