Ishu za Paula zimekuchosha? We sikiliza ngoma hizi

Muktasari:

YANAYOENDELEA kwenye mitandao ya kijamii, ya kumhusu binti wa prodyuza P Funk na mwigizaji Kajala Masanja, Paula sio kwa ajli ya kila mtu.

YANAYOENDELEA kwenye mitandao ya kijamii, ya kumhusu binti wa prodyuza P Funk na mwigizaji Kajala Masanja, Paula sio kwa ajli ya kila mtu.

Wengine yanawachukiza ile mbaya kwa sababu kwanza yamejaa udhalilishaji, uvunjaji wa sheria za nchi, uvunjaji wa maadili na yanaumiza muziki wa Bongo Fleva na sanaa kwa jumla.

Kama huna habari ya kinachoendelea ni, inadaiwa msanii Harmonize aliyekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Kajala, alikuwa akimuwinda Paula ambaye ni mtoto wa mpenzi wake. Yaani Harmonize alikuwa anataka kula kuku na kifaranga chake.

Hayo yamejulikana kupitia mazungumzo ya meseji zilizovujishwa zinazodaiwa za Harmonize kwenda kwa binti huyo pamoja na video za utupu zinazodaiwa kuwa ni za Harmonize alizokuwa akimtumia Paula.

Sasa kasumba hiyo imezua vita vikali kati ya Harmonize na Rayvanny kwa sababu Rayvanny anadaiwa pia ni mpenzi wa Paula. Timu hizi mbili zimeandikiana nyimbo za kuchambana (diss track) sio kitoto, yaani Harmonize na baadhi ya wasanii wake wa Konde Gang wanamwimba Rayvanny na wakati Vanny Boy naye na baadhi ya wasanii wa Wasafi wanamwimba Konde Boy na timu yake.

Sakata hili limeteka kila sehemu, mitandao yote ya kijamii na vyombo vya habari vinavyohusika na burudani kiasi kama wewe ni mpenda burudani unaweza kukosa kabisa taarifa ya burudani mpya zinazoendelea.

Sasa kama wewe unapenda burudani, lakini unachukizwa na skendo na kiki za wasanii, kwa wakati huu unaweza kufanya mambo haya.


SIKILIZA NGOMA HIZI MPYA

Kabla na baada ya sakata kuanza kuna wasanii lukuki walitoa ngoma kali. Kwa bahati mbaya hazisikiki kwa sababu zinamezwa na hii kiki.

Wimbo kama Utanambia Nini wa mkongwe Profesa Jay unastahili kupewa uzito zaidi ya skendo ya Paula na ‘waume zake’ kwa sababu kwanza ni wimbo wa Profesa Jay uliokuja baada ya kukaa kimya kwa miaka mingi kutoka na shuhuli za Ubunge. Pia ni wimbo ambao amewekeza sana kama wanavyofanya vijana wa sasa, ukiangalia ubora wa video unaweza kugundua hili.

Msanii Marioo ametoa wimbo wa For You, moja ya ngoma zake zinazostahili kusikilizwa sana. Kwa mujibu wa Marioo mwenyewe wimbo huo ulistahili kutoka mapema mwezi jana lakini alisitisha kutokana na skendo kama hii inayoendelea sasa, ambayo kwa mwezi uliopita ilikuwa inahusu Rayvanny kusambaza video zinamwonyesha yeye na Paula wakipigana mabusu ya kimahaba.

Kupitia akaunti yake ya Instagram Marioo aliandika, ‘Mabroo, mkimaliza kutrend, mtatuambia tutoe muziki.’

Rosa Ree ameachia wimbo wa kuitwa Satan, moja ya ngoma zinazostahili kupewa sikio kwa sababu humo ndani rapa huyo muangamizaji wa biti ameeleza mambo mengi kuhusu namna shetani alivyojaribu kuharibu maisha yake kwa kumkutanisha na mpenzi aliyemtambulisha kwenye matumizi ya mihadarati.

Billnas ameachia wimbo wa kuitwa Tatizo, moja ya ngoma zake bora baada ya kukaa miezi kadhaa bila kazi mpya ya kwake huku watu wakimtupia lawama siku hizi amepunguza mzuka wa kutoa kazi.

Rapa wa kike, Frida Amani ameachia wimbo wa kuitwa Madam President. Wimbo wenye ubunifu wa juu. Humo ndani amechukua sehemu ya hotuba ya Rais mama Samia Suluhu na kuifanya ni mashairi yanayomuhusu yeye. Ubunifu unaostahili kuepwa sikio kuliko stori za Rayavnny na mkwewe Harmonize.

Nyandu Tozzy ameachia bonge moja la EP. Inaitwa 26 LIFE na humo ndani kuna ngoma sita zilizoshiba.

Mbosso ameachia video ya wimbo wa Baikoko aliomshrikisha Diamond Platnumz kitoka kwenye albamu yake ya Definition of Love. Wakati Rayvanny pia ameachia video ya wimbo wa kiulaini aliomshirikisha Juxkutoka kwenye albamu yake ya Sound of Africa.


Au tazama filamu hizi

Kama ni mtu wa filamu, tazama filamu npya ya muongozaji mwanamke Seko Shamte inayoitwa Binti. Filamu ambayo ni hadithi ya wanawake wanne wanaobadilisha mitazamo ya iliyozoeleka juu ya wanawake kwa kutumia uanamke wao.

Filamu inaonyeshwa kwenye kumbi za Century Cinema za Mlimani City mpaka tarehe 15.

Lakini pia tamthilia ya vichekesho ya kitimtim inaendelea baada ya muda mrefu kuto kuonyeshwa kwa episode mpya.

Unaweza kujipoza na hayo kama habari za Paula, Rayvanny, Harmonize na Kajala zimekuchosha.