Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huyu sasa ndo Kajala Masanja

Muktasari:

  • Licha ya hayo, anafunguka mengi alipokutana na Mwanaspoti na kufanya mahojiano na zaidi ni juu ya ukimya wake kwani amekuwa ni wa kutafutwa kwa tochi, huku kwenye upande wa sanaa amesema anajiamini na mahusiano yake ya ghafla na kuhusu deni la Harmonize analodaiwa na benki.

MAISHA yana mapito yake. Kwa mwanadada Winniefrida Kajala Masanja amepitia mengi katika maisha yake yaliyojaa misukosuko, changamoto akikosea na kutafuta namna ya kuishi hadi kujipata na sasa mwenyewe anasema amekuwa mwanamke wa mfano mzuri na mabaya.

Licha ya hayo, anafunguka mengi alipokutana na Mwanaspoti na kufanya mahojiano na zaidi ni juu ya ukimya wake kwani amekuwa ni wa kutafutwa kwa tochi, huku kwenye upande wa sanaa amesema anajiamini na mahusiano yake ya ghafla na kuhusu deni la Harmonize analodaiwa na benki.

Nini watu hawakijui kutoka kwako?

Kajala: Kitu ambacho wengi hawakijui, mimi ni dansa mzuri sana na ndiyo maana wakati mwingine nikiwa kwenye muziki nashindwa kujizuia kupanda stejini kucheza. Tangu nikiwa nasoma shule ya sekondari nilikuwa dansa kwenye maklabu ya usiku. Unajua zamani maeneo ya Kinondoni  kulikuwa na klabu nyingi, kuna moja ilikuwa inaitwa 'Club Asset' na mara nyingi ndiyo nilikuwa nafanyia udansa hapo japo baadae nilikuwa dansa kwenye klabu nyingine nyingi hapa mjini, hii ni kwa wanaonijua tangu enzi hizo, ila kwa wa sasa wengi hawaijui hii (kicheko).

Kwa sasa uko kimya, nini sababu?

Kajala: Watu waelewe Kajala wa zamani sio wa sasa, nimebadirika sana. Sasa hivi muda mwingi nautumia kuwa na mjukuu wangu Amara, kwenda mazoezini na kwenye shughuli zangu.


Mahusiano Je?

Kajala: Kuhusu mahusiano, niko ya kimya kimya ambayo siyo ya mitandaoni, nimejifunza vitu kutokana na mambo yaliyopita ndiyo maana niko hivi kwa sasa."

Unajisikiaje ukivaa mavazi yanayokuacha wazi?

Kajala: Enheeee! Hapo hapo kwenye mavazi. Huwa najisikia vizuri tu sababu kwanza siwezi kupangiwa mavazi na mtu. Huwa navaa nguo zangu kwa mapenzi yangu na watu wasinihukumu  kwa mavazi. Unajua mitandaoni ukifuatilia sana kuna mahakimu wengi wa maisha binafsi ya watu, hivyo kwangu kuvaa nguo yoyote siyo nionekane sijiheshimu ama sijielewi, navaa ninayoiona napendeza.


Jina 'Sex Bibi' limetokana na nini?

Kajala: Kwanza unanionaje shoga yangu? Mimi si mzee kabisa? (Kicheko). Hivyo, jina la Sex Bibi nimetembea na biti la watu wa mitandaoni, maana kila nikiposti picha comment nyingi naambiwa mimi mzee. Jina lilianza kama utani na kwa kuwa nimeona watu wananiita hivyo, nikaona niliendeleze hivyo mimi ni Sex Bibi, ni mzee na nina mjukuu wangu kipenzi, kwa nini nisikubali mimi ni bibi?

Kipi unapenda na kipi hupendi?

Kajala: Napenda sana amani na upendo, kutuliza akili yangu sehemu iliyotulia, sipendi vurugu wala maneno maneno, sipendi kukata tamaa katika maisha yangu, napenda tu kampani ya kawaida, tukimaliza kila mtu ana zake. Pia napenda kuzungukwa na watu wanaojielewa, wanaoweza kunifanya nikacheka kila wakati.


Mtoko wako kwa siku ni kiasi gani?

Kajala: Hapa sasa nizungumzie kuanzia kujaza gari mafuta, mavazi, manukato, nywele, pochi, chakula, vinywaji. Natumia sh1.8 milioni hivi.


Una nguo za aina gani kabatini?

Kajala: Magauni mafupi, suruali za jeans na nguo za mazoezi na hapo kwanza kurudia nguo huwa siwezi, yaani naweza kuvaa nguo mwezi hadi miezi kadhaa mbele nikairudia.

Kweli una hasira na mambo ya kiaskari kama wengi wanavyodai?

Kajala: Daah! Hili sijui ila mimi najiona nipo sawa tu,  au  kwa kuwa nimelelewa katika mazingira ya kota za polisi, ndiyo maana wanasema hivyo? Maana baba yangu na mama yangu wote walikuwa ni maaskari polisi pale Oyster Bay.


Deni la Harmonize kutoka benki ni kweli linahusu matumizi yako kipindi upo naye?

Kajala: Ningekuomba shoga yangu tusimzungumzie huyu mtu, sitaki kuzungumza chochote kuhusu yeye, nakuomba sana.


Unapenda nini kutoka kwa mkwe wako Marioo?

Kajala: Kwanza Marioo ana heshima sana yule mtoto, msikivu pia na watu wasichokijua mimi nilianza kuwa shabiki wake kabla hata hajawa mkwe wangu, napenda nyimbo zake hata kabla hajawa na mwanangu Paula.


Kajala ni mtu wa namna gani?

Kajala: Ni mwanamke wa mfano wa mazuri na mabaya na sio wa kukata tamaa na maisha. Nimepitia misukosuko mingi nikajihisi kama niko kuzimu, lakini nikapambana na kuibuka tena na kurejea kileleni. Pia ni kati ya msanii anayejikubali.


Wewe ni timu gani?

Kajala: Mimi ni Mwananchi, naipenda sana Yanga, japo siku hizi nimepunguza kwenda uwanjani kutokana na majukumu, lakini zamani Yanga ikiwa inacheza ulikuwa hunikosi uwanjani?


Kitu gani hutosahau maishani?

Kajala: Mapito yangu, maana kuna siku nakaa nimetulia nakumbuka mapito yangu.