Huyo Mchopanga msimchukulie poa!

Ukweli wa elimu ya mteule wa `U-DC’ msanii Mchopanga

Muktasari:

  • Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa mkeka wa Wakuu wa Wilaya na kutajwa kwa jina la msanii Juma Chikoka maarufu kama `Mchopanga’ kumekuwa na mjadala  kuhusu elimu yake akilinganishwa na cheo alichopewa.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa mkeka wa Wakuu wa Wilaya na kutajwa kwa jina la msanii Juma Chikoka maarufu kama `Mchopanga’ kumekuwa na mjadala mitandaoni kuhusu elimu yake akilinganishwa na cheo alichopewa.

Mwanaspoti leo Jumapili Juni 20, 2021, imefanya mahojiano na msanii huyo ambaye amekuwa akiigiza kama mlinzi kwenye filamu nyingi, hakuwa tayari kuongea mambo mengi kwa kile alichoeleza ni mpaka atakapoapishwa.

Akigusia kuhusu elimu yake, Mchopanga ambaye kateuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya, ameeleza ana Shahada ya Masuala ya Sanaa, elimu aliyoichukulia Chuo Kikuu cha Bangalore nchini India.

Kama haitoshi amesema kwa sasa anasubiri kwenda kuanza masomo ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo huko anakwenda kusoma masuala ya Mahusiano kwa Umma.

Mchopanga ambaye amezaliwa mwaka 1983, kabla ya uteuzi huo amesema alikuwa ni Katibu Msaidizi Mkuu katika Idara ya Uenezi wa Umoja wa Vijana nafasi aliyokuwa anaishikilia hadi sasa.

Mteule huyo pia ameeleza kuwa mwaka 2010 aliwahi kugombea jimbo la Ilala lakini kura hazikutosha na mwaka 2011 ndipo aliajiriwa kama Ofisa wa Umoja wa Vijana(UVCCM).

Mwaka 2015 hakuweza kusimama na kugombea tena kwa kuwa alikuwa katika kitengo cha kusimamia wasanii, ambapo alifanya kazi chini ya Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba.

Hata hivyo, mwaka 2020 alijitosa tena kwenye kura za maoni ili kuwania kugombea jimbo la Ubungo nako huko kura hazikutosha na badala yale alipita Kitila Mkumbo, ambaye alipata tiketi ya CCM hivyo kulazimika kumuunga mkono na kumsaidia katika kampeni .

Ukweli wa elimu ya mteule wa `U-DC’ msanii Mchopanga

Kabla ya kwenda kusoma India, Mchopanga alisoma Shule ya

Msingi ya Uhuru jijini Dar es Salaam na kumaliza hapo mwaka 1998, kisha akajiunga na Shule ya Sekondari Kinondoni na kukamilisha masomo mwaka 2002 na baada ya hapo akachaguliwa kuendelea kidato cha tano Shule ya Sekondari Tambaza ambako alimaliza mwaka 2005.

Akiwa anasubiria majibu ndio akapata udhamini wa kwenda kusoma chuo nchini India na kumaliza mwaka 2008 na aliporudi ndio akaanza kujihusisha na masuala ya siasa.