Hussein Jumbe (10) - Alazwa sello kisa gitaa

ILIPOISHIA...Jumbe anasema alipata udhamini na kupewa cheki ambayo aliipeleka ofisini na kufanikiwa kulipa suti za wanamuziki na viatu. Pia, mwanamuziki huyo anasema pesa hizo zilisaidia kuwalipa wanamuziki madai yao na vilevile walilipa studio.

Katika uzinduzi huo, Sikinde ilisindikizwa na TOT Bendi na Twanga Chopolopolo, ulifana na kufanikisha ahadi yake ya kwanza aliyoahidi wakati akichaguliwa kuwa meneja wa bendi.

Mwanamuziki huyo anasema uzoefu huo aliupata katika Bendi ya Msondo Ngoma kutokana na ukaribu wake na meneja wa bendi hiyo, Said Kibiriti...SASA ENDELEA


AWEKWA KITIMOTO KIZITO

Baada ya uzinduzi uliofana, Jumbe anasema aliitwa kwenye kikao na wanamuziki wenzake walitaka kujua amepewa kiasi gani na TBL, zimetumika ngapi na kiasi gani kimebaki?

Katika kikao hicho, Jumbe ilimlazimu kufafanua kuhusu cheki aliyopewa na TBL na kuwataka wanaotaka kujua wauulize uongozi ambao ndio wanaojua imetumika ngapi na imebaki ngapi.

“Niliwaambia cheki haikuandikwa Hussen Jumbe, bali iliandikwa DDC ndio maana siwezi kujua kimetumika kiasi gani na kiasi gani kimebaki.”


SAFARI YA UJERUMANI

Jumbe anasema baada ya kikao cha wanamuziki ambacho pia kilihudhuriwa na viongozi, aliitwa pembeni na mwanamuziki wa bendi hiyo, Hassan Rehan Bitchuka na kumwambia bendi ilikuwa ikitakiwa Ujerumani.

“Bitchuka aliniambia, Grabner Wener anakuja Tanzania na kuna uwezekano mkubwa wa kwenda Ujerumani na Uholanzi,” alifafanua Jumbe.

Kabla ya ziara hiyo, Jumbe anasema Sikinde ilifanya ziara Mbeya na Mwanza.

Juni 27, 2007 baadhi ya wanamuziki wa Sikinde wakiwamo, Bitchuka, Hemba na Jumbe walikuwa safarini kuelekea Ujerumani. Wengine walikuwa Habib Jeff Mgalusi, Hamis Milambo, Ally Jamwaka, Stephen Maufi, Shabani Lendi, Shaban Mabuyu (marehemu) na Mohammed Idd (marehemu).


WAVUNA PESA KIBAO

Baada ya kufanya shoo za Uholanzi na Ujerumani na kufana sana. Siku moja kabla ya kurudi Tanzania, walitembea madukani kwa ajili ya kufanya shoping.

Jumbe anasema walikiubaliana kujitoa Sikinde na kuunda umoja wao na wakipata vyombo waanzishe bendi yao.

Sababu ya kufanya hivyo ni DDC ilishindwa kutoa ushirikiano kwa ajili ya safari hiyo. Walikubaliana wakirudi nchini wasajili bendi yao na kufungua akaunti.

Jumbe alinunua gitaa lake binafsi. Lakini wenyeji wao waliwapa pesa za kutosha na vyombo vya muziki kama vile magitaa matatu, saxphone na trumpert.

“Tulikubaliana pesa tugawane na vile vifaa tulivyopewa viwe vya bendi na tukavikabidhi kwa uongozi,” anasema Jumbe.

Pia, mwanamuziki huyo anasema wanamuziki wenzake walimshauri gitaa alilinunua alibadilishe na mojawapo kati ya yale waliyopewa kwa niaba ya bendi.

“Gitaa nililonunua lilikuwa zuri, lakini yale mengine yalikuwa mazuri zaidi, nikakubaliana na ushauri wa wenzangu,” anasema.

Baada ya kurudi nchini, Jumbe alikabidhi vifaa alivyopewa kule Ujerumani kwa ajili ya bendi kwa fundi mitambo, Thomas Kibuga (marehemu kwa sasa) kwa kuandikishiana naye.


WAZO LA BENDI BINAFSI

Wanamuziki hao 10 waliporudi nchini kila mmoja alichanga laki moja na jumla kupata milioni moja. Kiasi hicho kilikua kichocheo cha kuanzisha umoja wao.

Hakupita muda mrefu wakampata mtu aliyekuwa tayari kununua vyombo vya muziki lakini sharti lake alitaka kila mmoja wao aweke nyumba yake rehani. Hawakukubali naye.

Wanamuziki hao walipata mtu mwingine ambaye alikuwa tayari kununua vyombo, basi dogo la kubebea wanamuziki na gari ya kubebea vyombo.

Mtu huyu alikuwa tayari kutoa mshahara wa mwezi mmoja wa kila mwanamuziki na kugharamia mazoezi kwa mwezi mmoja masharti yake alitaka kuwa mmoja wa kati ya wanamuiki hao.

“Wakati huo tulikuwa 12, aliongeza Yussuf Benard (marehemu), lakini Jeff alikataa wazo hilo,” anasema Jumbe.


ALAZWA SELO, KISA GITAA

Mwanamuziki huyo anasema alitafakari kwa muda jinsi maisha ya muziki yalivyokuwa na mitihani mingi na kuamua kutangza kupumzika shughuli za muziki.

“Niliandika barua ya kuomba kujiuzulu uongozi na kupumzika kwa miezi mitatu bila ya malipo. Barua yangu ikakubaliwa nikaondoka Sikinde,” anasema.

Akiwa mapumzikoni alifuatwa na viongozi wa Bendi ya Mikumi Sound ya Morogoro waliokuwa wakihitaji huduma yake ya kuiongoza bendi hiyo.

Jumbe anasema alijiunga Mikumi Sound akiwa na wanamuiziki wawili waliotoka Sikinde, Hemba na Ramadhani Mapesa. Hata hivyo wawili hao hawakudumu na wakaamua kurudi katika bendi yao ya awali. Akiwa na bendi hiyo, Jumbe alifanikisha kurekodi nyimbo kadhaa zilizoipata umaarufu mkubwa kama vile Mlinzi wa Godown, Ua Jekundu, Usiku wa deni na Penzi haligawanyiki.

“Uzinduzi wa bendi nyimbo hizi ulitikisa Mji wa Morogoro na bendi ilipata umaarufu mkubwa sana,” anasema.

Jumbe anakumbuka jioni moja ya ikiwa ni siku Sikukuu ya Idd El Fitr alikamatwa na polisi na kulazwa lupango kwa kosa la wizi.

Anakumbuka alikamatwa siku ya Jumamosi na alilala selo Morogoro na Jumapili alisafirishwa chini ya ulinzi hadi Dar es Salaam na kulazwa katika selo ya Kituo cha Polisi cha Msimbazi.

“Jumatatu ndipo nilipojua nilishtakiwa na meneja mpya wa DDC, kwa kosa la wizi wa kuaminika la kujimilikisha gitaa lenye thamani ya shilingi laki tano na mashahidi ni wanamuziki wenzangu,” anafafanua Jumbe.

Mke wa Jumbe, Zakhia au Mama Ima alipata taarifa na Jumatatu alifika mahakamani sambamba na mmiliki wa bendi ya Mikumi Sound.

Hakimu alimuuliza Jumbe kama alikuwa na mashahidi wa kumsaidia kujibu shtaka hilo lakini mwanamuziki huyo alijibu hakuwa na mashahidi zaidi ya kitabu chake cha kumbukumbu ambacho alikionyesha akiwa amemsainisha fundi mitambo wa Sikinde aliyepokea vifaa vyote alivyovipokea Ujerumani.

Kesi hiyo ilihairishwa na kupangiwa tarehe nyingine.

Jumbe alikuwa akitokea Morogoro kusikiliza kesi hiyo. Hata hivyo, baada ya kuahirishwa kwa mara tatu upande wa waliomshitaki haukuwa ukitokea mahakamani, akaachiwa huru.


ARUDI TENA MSONDO

Mwaka 2008 Jumbe alirudi Msondo baada ya kutoka Mikumi Sound. Hakurudi hivivhivi. Aliibuka na kibao kikali cha Kiapo.

Ndani ya wimbo huo, Jumbe anaimba akiapa kurudi Msondo Ngoma huku akiweka ahadi ya kutowafanyia maudhi tena.

Juni 2009, akiwa na Msondo Ngoma pale Leaders Club mwanamuziki huyo alifutwa na mtu mmoja na kumwambia anaitwa katika meza iliyokuwa na wanawake wanne, akaenda.

Akiwa pale alianza kuwasalimia mmoja baada ya mwingine hadi akafika kwa mmoja wao aliyekuwa amevaa miwani meusi. Wakati akimsalimia akavua miwini. Ndipo Jumbe alipomtambua, alikuwa ni Sister May.


SAFARI YA TALENT

Sister May aliwaomba wenzake anaenda faragha na Jumbe na walikaa katika meza nyingine na kuzungumza mipango yao.

“Hakuwa na mazungumzo marefu, bali aliniambia anashukuru kurudi salama na kesho yake niende nyumbani kwake, Kariakoo kwa ajili ya kununua vyombo,” anasema Jumbe.

Kabla ya kuondoka Msondo Ngoma, Jumbe aliwaaga viongozi kwa kuwaambia mpango wake na wakawatafuta wanamuziki wengine wawili Juma Katundu na Edo Sanga.

Jumbe anasema hakuamini alipoenda nyumbani kwa Sister May na kukabidhiwa shilingi 14 milioni kwa ajili ya kwenda kununua vyombo.

“Niliwatafuta wanamuziki 10 na Sister May alinunua nyumba maeneo ya Tandale kwa Bi Nyau tukawa tunafanya mazoezi hapo,” anakumbuka. Anawataja wanamuziki aliokuwa nao katika bendi hiyo ni Rashid Sumuni, Omary Jamwaka, Lindunga, Dogo Ommy na Abbas Abdallah (marehemu).

Wengine ni Yahya Majaliwa, Masoud Kilimanjaro na kiongozi wa bendi alikuwa ni yeye mwenyewe, Jumbe.


SISTA MAY ATAKA NDOA

Baada ya mazoezi, bendi ilipata shoo ya kwanza kwa kukodiwa mkoani Dodoma kulikukuwa na onyesho la Miss Dodoma.

Bendi hiyo ilikuwa imeahidiwa kulipwa 2 milioni kwa ajili ya shoo hiyo na bendi ililipiwa gari ya kusafirisha vyombo na wanamuziki walilipiwa malazi na sehemu za kulala.

Jumbe anasema alitoa milioni moja kwa wanamuziki na laki tano yake na iliyobaki ni ya Sister May. Siku moja kabla ya safari, Sister May akabadilisha madai, akasema vyombo haviendi kokote mpaka afunge ndoa na Jumbe.

“Alisema nifunge naye ndoa kwanza kisha sherehe itafanyika baadaye. Siku zote alikuwa akiniita kaka, sasa alitaka kuniita mume,” anakumbuka Jumbe na kushusha tabasamu.

Anafafanua Sister May alitaka awe mke wa pili na aliahidi kumpa gari ya kutembelea Jumbe na kumruhusu kuvitumia vyombo vya muziki atakavyo.