Huduma za Basata, Cosota na Bodi sasa kuzipata kiganjani

Tuesday November 23 2021
basata pic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Huduma za taasisi zinazoshughulika kusimamia sanaa nchini Tanzania sasa mtu ataweza kuzipata kutumia simu za kiganjani baada ya kuzinduliwa kwa mfumo wa huduma ya kidigitali.
Taasisi hizo ni Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (Cosota) na Bodi ya filamu.
Mfumo huo ulizinduliwa jana Novemba 22, 2021  na Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo jijini humo, Innocent Bashungwa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara hiyo na wasanii.
Bashungwa amesema kuanza kwa huduma hiyo kutawapunguzia adha wasanii kwenda kupata huduma hiyo kwenye ofisi hizo na sasa kuipata wakiwa hata sebuleni kwao kupitia simu za kiganjani.
"Mfumo huu wa kidigitali ni mzuri, ninachoomba kwa taasisi husika kuendelea kutoa elimu ya mara kwa mara  kwa wasanii mpaka hapo watakapoelewa kuitumia mifumo hiyo," amesema Waziri Bashungwa.

Kwa nyakati tofauti wakielezea mfumo huo akiwemo Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Matiko Mniko, amesema kupitia mfumo huo ukiachilia mbali wasanii kujisajili, pia  wataweza kupata vibali vya kwenda kufanya show nje ya nchi na wale wa nje ya nchi kuja nchi.
Wakati Ofisa Mwandamizi Tehama kutoka Cosota, James Sagenge, amesema kwa mfumo huo, wasanii wataweza kupata taarifa pia ya mirabaha yao na kusaili kazi zao na wadau wanaotaka kutumia kazi zao kupata vibali kupitia mfumo huo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dk Kiagho Kilonzo, amesema kupitia mfumo,wasanii wataweza kupata vibali vya kutengeneza filamu ndani ya siku moja badala ya siku 30,vibali ya uhakika siku tatu na vitambulisho siku mbili.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Elia Mjata, aliwataka wasanii kuutumia mfuko huo kwa kuwa ilikuwa kilio chao cha muda mrefu kuchukua muda kupata mrefu kupata huduma na kubainiasha kuwa hatua hii itapunguza pia urasimu na gharama.

Katibu wa Shirikisho la Muziki wa dansi Tanzania (Chamudata), Hassan Msumari akizungumza kwa niaba ya wasanii wa wanamuziki, amesema wamehemewa kwa kilichofanywa na serikali kwani huduma hiyo itakuwa mkombozi kwao na kilio chao kimepata dawa.

Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho, Abraham Ngambale, amesema kubwa katika mambo waliyopambana nayo ni takwimu, kwani wasanii wametawanyika na hivyo kushindwa kuwa na utambuzi na hivyo kufikiwa na fursa mbalimbali zinazojitokeza kwa wasanii, hivyo mfumo huo wana imani unaenda kulitatua hili kwa mapana.

Advertisement