Harmonize: Sizibi mashimo, nataka watoboe

Muktasari:
- Harmonize ameweka bayana kuwa anafahamu wapo watu wenye kuamini kuwa ameshiriki kukwamisha jitihada na mipango ya baadhi ya wasanii kiasi cha wengine kumuona kama mtu asiyependa maendeleo ya wengine.
MSANII wa Bongofleva, Harmonize, amefunguka madai ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimtaja kama mmoja wa wasanii wasiopenda maendeleo ya wenzio na hata kumtaja kuwa mwenye roho mbaya.
Harmonize ameweka bayana kuwa anafahamu wapo watu wenye kuamini kuwa ameshiriki kukwamisha jitihada na mipango ya baadhi ya wasanii kiasi cha wengine kumuona kama mtu asiyependa maendeleo ya wengine.
Jambo hilo, Harmonize alilikanusha akiwa chemba na Mwanaspoti Juni 29, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, akiweka wazi uhalisia wa maisha yake na namna anavyopenda kushiriki katika kuhakikisha anaunga mkono harakati za wengine kutoboa na si kweli kwamba anaziba njia.
“Mimi siamini kwamba mtu mwingine akifanikiwa ndio mimi nitafeli hapana, watu wakati mwingine naona wanaandika kwenye mtandao kwamba nina roho mbaya, lakini sijawahi kuwa na roho mbaya.
“Naweza kusema mimi ni mmoja wa wasanii ambao tumetoa wasanii wenye nguvu katika nchi, na sijawahi kuwa na tatizo na mtu, labda tu unaweza kusikia wachonganishi wakizungumza mambo ambayo baadaye yanakuja kuwa chuki,” anasema.
Aidha, Harmonize anasema amekuwa anapenda kushiriki kazi za wasanii wenzake kwasababu anaamini muziki ni maisha yao hivyo akifanya hivyo anakuwa ameshiriki kuchangia kufanikiwa maendeleo ya mtu.
“Tena siku hizi mtoto wa watu ninasapoti kazi zao, napenda kushiriki, napenda kuona ifanikiwe kwa sababu naamini kwa namna moja au nyingine muziki ni maisha ya watu, akifanikiwa mtu unakuwa umemkomboa kimaisha.” amesema Harmonize.
WATOTO WA KIKE
Harmonize katika pilikapilika zake za muziki, inaonyesha amefanya kazi nyingi na wasanii wa kike na kazi hizo zimefanya vizuri, hapa anaelezea sababu ya kutoa sapoti kwa wanamuziki wa kike.
“Hapo sasa ndio maana nilisema huu muziki upo kwa ajili ya kutoa burudani na kusapotiana sisi wanamuziki kwa wanamuziki, hapo nyuma nilishiriki kwa wingi kazi na wanamuziki wa kike sababu kwanza nilitaka kuchanganya ladha ya sauti katika nyimbo zangu, pili kupelekana mjini, namaanisha mimi nimefikia hatua hii na mwingine inabidi nimfikishe hatua fulani hata kama anajiweza kimuziki unamuongezea hatua ya kufikia sehemu nyingine,” amesema.
Harmonize alifanya kazi na Abigail Chams na wimbo wake ‘Closer, Nandy alimpa shavu Harmonize katika wimbo wake ‘Acha Lizame’, Maua Sama alimshirikisha Harmonize katika wimbo wake ‘Niteke Remix’, Jane Musso wimbo wake wa Omoyo aliamua kumshirikisha Harmonize kwenye remix ya wimbo huo na kujikuta akirudi tena sokoni kama msanii mpya, Maua Sama alimshirikisha Harmonize katika wimbo wake ‘Niteke Remix’, Queen Darlin aliwahi kumshirikisha Harmonize katika wimbo uitwao ‘Mbali’, Angella katika wimbo wake wa ‘Kioo’ na wengine wengi.
ATOA NENO KWA WASANII WENZAKE
Harmonize amesema ni vizuri wasanii wa Afrika kuwa na nyimbo za Kiingereza katika orodha za nyimbo zao ili kuwafikia watu wengi duniani, yeye anaimba nyimbo za Kiingereza ili dunia upate kuuelewa muziki wa Tanzania.
“Wasanii wa Afrika wasiache kuimba kwa lugha ya kwetu, lakini wahakikishe wanaimba na nyimbo za Kiingereza ili kuendana na dunia, muziki wetu ni mzuri lakini wakati mwingine unawapa ugumu watu kuelewa tunachoimba.
“Najivunia soko la muziki wa Afrika, kuna wasaznii ambao wanaweza kuimba Kiswahili, ambao wanaweza kuimba Kiingereza na wanaoweza kuimba vyote. Afrika Mashariki tunakuja kwa kasi, na kwa namna hii tunaweza kuacha ‘ku-perform’ shoo za mchana kwenye matamasha makubwa, kwa sababu tunawapa machaguo,” amesema.