Harmonize kwa Malaika ni kama Wolper, Kajala, Poshy

Muktasari:
- Harmonize leo Desemba 4,2024 katika Insta story yake ameweka video fupi iliyo na ujumbe wa kukanusha habari za yeye kutoka kimapenzi na Malaika. Maneno hayo yalikuwa yanasikika hivi:
'Haya maneno sio mageni, labda kwa wageni wa jiji'. Ndivyo anavyomaanisha staa wa Bongo Fleva, Harmonize akikanusha kuhusu kutoka kimapenzi na mwanamitandao, Malaika Cute ambaye kwa sasa ndio habari ya mjini.
Harmonize leo Desemba 4,2024 katika Insta story yake ameweka video fupi iliyo na ujumbe wa kukanusha habari za yeye kutoka kimapenzi na Malaika. Maneno hayo yalikuwa yanasikika hivi:
"Sina mahusiano na Malaika, Malaika ni rafiki yangu, ila nawashauri wanawake fanyeni Surgery ili mpendeze muwe kama Ex wangu, sababu Dunia ya sasa inataka wanawake wa hivyo, mfano mimi x wangu nilimlipia hela ili akafanye Surgery sababu alikuwa hajiamini."
Mara kadhaa akionekana na mwanamke mwingine, Harmonize amekuwa akikanusha kutoka naye kimapenzi, kisha baadaye huweka wazi ni wapenzi ikiwa ni uvumilivu kumshinda.
Hii aliwahi kufanya kwa baadhi ya wanawake aliowahi kuwa nao kimapenzi na baadhi yao ni wasanii Wolper ambaye pia ni mwanamitindo, Kajala Masanja na mwanamitandao, Poshy.
Mwaka 2016, Harmonize kwa Wolper walianza kuonekana karibu hasa sehemu za starehe na picha na video zao nyingi ziliwekwa mitandaoni. Awali baadhi ya watu walidhani sio wapenzi bali wanatafuta tu kiki na hata Harmonize alipoulizwa alikana sio wapenzi bali ni marafiki tu.
Hata hivyo, kadri siku zilivyoendelea kwenda, uzalendo uliwashinda na kuamua kuweka wazi uhusiano wao kuwa ni wapenzi na Harmonize akaonekana kumtumia Wolper kama video queen katika wimbo wake wa 'Niambie'.
Mwaka 2021, Harmonize pia alianza ukaribu na msanii Kajala Masanja na walionekana sehemu tofauti tofauti, ikiwamo safari ya Zanzibar na mwanadada huyo alionekana kumbeba mtoto wa Harmonize.
Hata hivyo, Harmonize alipoulizwa kama ni wapenzi awapenzi alisema ni mtu wake wa karibu na anapenda tu jinsi anavyopenda kufanya mazoezi
Baada ya muda walikuja kuweka wazi ni mapenzi na mwaka 2022 wakaachana kabla ya kurudiana mwaka huohuo. Harmonize alitoa wimbo 'Nitaubeba' na video Queen alikuwa Kajala.
Mwaka huu, 2024, Harmonize aliwahi kuwa karibu na mwanadada Poshy Queen na baada ya kuulizwa alisema ni rafiki yake na shabiki yake, lakini baadae walikuja kuweka wazi ni wapenzi, lakini baada ya muda wakaachana.
Sasa, kaibuka Malaika na uhusiano wao umekuwa ukivuta hisia za wengi na kuwa mjadala tangu waanze kuonekana hadharani.
Kutokana na matukio yao mengi, kuna viashiria vya kuwa kwenye penzi na katika ukurasa wa Instagram ndipo stori zilipoibuka baada ya Harmonize kushare video ya Malaika akiwa studio anapigwa picha, huku wimbo unaosikika ni 'You Better Go' wa msanii huyo.
Ujumbe uliotolewa kwenye posti hiyo ya Oktoba 14, ulionekana kuwa wa mahaba zaidi ya kazi na mashabiki walichukulia kama hatua ya kwanza ya uhusiano wao.
Tukio la pili ni la Malaika Kupokea tuzo kwa niaba ya Harmonize wakati wa sherehe ya tuzo za muziki Tanzania. Tukio hilo lilizua gumzo huku wengi wakiona hatua hiyo kama ishara ya wazi ya nafasi maalum ya Malaika kwenye maisha ya Harmonize.
Video ya Kimahaba ya Wimbo 'Wangu' ambao Marioo amemshirikisha Harmonize, Video zinazosambaa kupitia insta story ya Harmonize zinawaonyesha Harmonize na Malaika wakifurahia muda wa karibu kimahaba. Video hiyo ilikuwa imeambatana na wimbo 'Wangu'. jambo lililoonekana kama njia ya Harmonize kueleza hisia zake kwa mashabiki bila maneno ya moja kwa moja.
Kwa mfululizo wa matukio haya, mashabiki wengi wanaamini Malaika ni chaguo jipya la Harmonize kutokana na urembo wake na umbo lake vinadhihirisha aina ya mwanamke anayevutiwa naye. Huku wakizidi kuonekana pamoja, bado mashabiki walikuwa wanasubiri tamko rasmi kutoka kwao, hata hivyo, leo Harmonize amefunguka kuwa ni rafiki yake tu.