Grammy yapigwa kalenda kisa Corona

Wednesday January 06 2021
grammy pic
By Mwandishi Wetu

TUZO kubwa zaidi za muziki duniani za Grammy zilizokuwa zinatarajiwa kufanyika Januari 31 mwaka huu zimesogezwa mbele na sasa zitafanyika Machi 14, 2021.

Mabadiliko hayo yametangazwa Rais wa jumuiya inayohusika na uandaaji wa tuzo hizo inayofahamika kama ‘The Recoring Academy’, Harvey Mason Jr, usiku wa kuamkia leo Jumatano Januari 06, 2021 ambapo ametaja sababu za kufanya hivyo kuwa ni ongezeko la wagonjwa wa Covid-19 katika jiji la Los Angeles ambapo sherehe za utoaji wa tuzo hizo hufanyika.

Sehemu ya maelezo ya Academy yanasema; “Baada ya mazungumzo na wataalamu wa afya, tumeamua kuzisogeza mbele sherehe za utoaji tuzo za Grammy na sasa zitafanyika Jumapili, Machi 14, 2021,”

“Tumeona ni uamuzi sahihi kufuatia muenendo wa Covid-19 ulivyo kwa sasa hapa Los Angeles, hospitali zimezidiwa, ICU zimefikia ukomo wa kupokea wagonjwa pia miongozo mipya kutoka serikali za mji ya jinsi ya kuendesha matamasha katika kipindi hiki zinatubana.” imeeleza hivyo taarifa hiyo.

Tuzo za Grammy hufanyika kila mwaka nchini Marekani kwa ajili ya kuwatuza wasanii waliofanya vizuri kwa mwaka uliopita kupitia vipengele mbalimbali kama vile Muimbaji Bora, Mwandishi Bora wa Mashairi, Mtayarishaji Bora wa Muziki, Video Bora ya muziki na zaidi.

Aidha, mbali na Grammy tuzo nyingi za muziki zilizofanyika nchini Marekani hivi karibuni zilifanyika kwa njia ya mtandao kama sehemu ya kuepusha misongamo inayoweza kuchochea kusambaa  kwa ugonjwa wa Covid-19. Mfano tuzo za Afrimma na Aeausa ambazo Tanzania ilikuwa na wawakilishi na walishinda.

Advertisement
Advertisement