Fally Ipupa na kijiti cha Diamond BET 2022

Muktasari:

Licha ya lango kutanuliwa, ni mwaka wa pili mfululizo Afrika Mashariki inatoa msanii mmoja kuwania tuzo za BET. Lakini, mwaka huu Fally Ipupa kutoka DR Congo ndiye anawakilisha baada ya Diamond Platnumz kupata nafasi hiyo mwaka jana.

Licha ya lango kutanuliwa, ni mwaka wa pili mfululizo Afrika Mashariki inatoa msanii mmoja kuwania tuzo za BET. Lakini, mwaka huu Fally Ipupa kutoka DR Congo ndiye anawakilisha baada ya Diamond Platnumz kupata nafasi hiyo mwaka jana.

Hata hivyo, ikumbukwe DR Congo imejiunga rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki mapema mwaka huu, na kuongeza idadi ya nchi toka saba hadi nane ambazo ni Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan Kusini.

Hiyo ina maana kuwa kama DR Congo isingejiunga na jumuiya hiyo, basi mwaka huu Afrika Mashariki isingekuwa na mwakilishi kwenye tuzo hizo zinazofanyika Juni 26, 2022 katika ukumbi wa Microsoft Theater jijini Los Angeles, Marekani.

Tuzo hizi zinazoandaliwa na Black Entertainment Television (BET) tangu Juni 19, 2001 zinalenga kusherehekea mafanikio ya kazi za Wamarekani Weusi katika sanaa ya muziki, uigizaji na michezo.

Mwaka jana Diamond aliwania kipengele cha Best International Act, ikiwa ni mara ya tatu ambapo alichuana na wakali kama Wizkid, Emicida, Headie, Aya Nakamura, Youssoupha, Young T & Bugsey na Burna Boy aliyeibuka mshindi.

Fally Ipupa anawania kipengele hicho akichuana na wakali kama Drave (UK), Dinos (Ufaransa), Fireboy DML (Nigeria), Little Simz (UK), Ludmilla (Brazil), Major League DJZ (Afrika Kusini), Tayc (Ufaransa) na Tems (Nigeria).

Toka mwaka 2019 hadi 2021, Burna Boy wa Nigeria ameibuka mshindi mfululizo na kutambulika kama msanii aliyeshinda mara nyingi kwenye kipengele cha Best International Act ambacho BET walikianzisha mwaka 2010 kikijulikana kama Best International Act: Africa.

Ikumbukwe kuwa Eddy Kenzo kutoka Uganda ndiye msanii wa kwanza wa Afrika Mashariki kushinda tuzo ya BET, mwaka 2015 aliibuka mshindi katika kipengele cha Viewer’s Choice Best New International Act, huku Rayvanny akishikilia rekodi kwa upande wa Tanzania ambapo, mwaka 2017 alishinda katika kipengele hicho pia.

Kwa ujumla Beyonce Knowles wa Marekani ndiye anashikilia rekodi ya kushinda tuzo nyingi za BET kwa muda wote, akiwa nazo 31, amechaguliwa kuwania mara 66 huku mara 58 akiwa pekee na mara nane kupitia kundi la Destiny’s Child.

Wasanii wa kwanza kukabidhiwa tuzo ya BET ni kundi la Outkast liloundwa mwaka 1992 na wasanii wawili (Andre ‘3000’ Benjamin na Antwan ‘Big Boi’ Patton) ambao mwaka 2001 walishinda kipengele cha Best Group.

Wakati ameachia Extended Playlist (EP) yake, First of All (FOA) yenye nyimbo 10 Machi, mwaka huu Diamond alisema mwaka jana alijikita zaidi katika biashara kuliko muziki na hata nyimbo alizokuwa akiziachia zilikuwa za kujishikiza tu.

Ikumbukwe hadi mwishoni mwa mwaka jana wasanii na wengineo zaidi ya 25 toka kiwanda cha burudani nchini, walichaguliwa kuwania tuzo tano za kimataifa, ikiwemo BET katika vipengele zaidi ya 30, lakini ushindi ulipatikana katika vipengele sita tu sawa na asilimia 1.8.

Katika tuzo zote tano Diamond ndiye Mtanzania aliyetajwa katika vipengele vingi zaidi, vikiwa ni 17 vya peke yake, lakini alishinda viwili tu sawa na asilimia 0.3.

Utakumbuka hadi sasa Diamond amefanikiwa kushinda tuzo za kimataifa kama Channel O, MTV, Soundcity, Headies, Afrima, Afrimma, Kora, AEA, EAUSA, the HiPipo Music Awards, huku akishikilia rekodi ya kushinda tuzo saba za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) 2014 kwa usiku mmoja, hivyo kumfanya kuwa msanii pekee Bongo mwenye tuzo nyingi.

Katika hatua nyingine, Staa wa WCB Wasafi, Zuchu anawania vipengele tisa katika tuzo za East Africa Entertainment Awards (EAEA) 2022 akiwa ndiye msanii aliyetajwa kwenye vipengele vingi zaidi.

Vipengele hivyo ni Best Female Artist, Best International Collabo (Sere ft. Olakira), Best East African Collabo (Upendo ft. Spice Diana),

Artist of the Year, Best Bongo Hit Song (sukari), Best Video Tanzania (Nyumba Ndogo), Best Video East Africa Lovers Choice (For Your Love ft. Mbosso), Best Dance Video (Sukari) na Best video Uganda (Upendo ft. Spice Diana).

Pia Zuchu anawania tuzo za The Headies toka Nigeria katika kipengele cha Best Artist East Africa ambapo anashindana na Diamond, Harmonize, Meddy (Rwanda), Nikita Kering (Kenya) na Eddy Kenzo (Uganda).

Zuchu aliyetambulishwa WCB Wasafi Aprili 2020 na kuachi EP yake, I Am Zuchu yenye nyimbo saba akiwashirikisha wasanii wawili, Mbosso na Khadija Kopa, tayari ameshinda tuzo moja kutoka African Muziki Magazine Awards (AFRIMMA) 2020 kutokea Marekani kama Msanii Bora anayechipukia.