Dudubaya ashinda rufaa, afutiwa adhabu

Muktasari:

Aprili 14, 2020 Basata ilimfutia usajili wa kazi za Sanaa msanii Godfrey Tumaini pamoja na cheti chake cha usajili chenye namba BST.2164 kutokana na tabia zake za utovu wa nidhamu na uvunjifu wa maadili.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, ametoa msamaha kwa msanii wa Bongo flava, Godfrey Tumaini maarufu kwa jina la Dudubaya huku akiweka masharti ya kuwa chini ya uangalizi kwa miezi sita.

Msamaha huo ulioanza Julai 21, 2020 umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Basata, Habbi Gunze kwa niaba ya Waziri Mwakyembe.

Hatua hii inakuja baada ya msanii hiyo kukata rufaa kwa Waziri huyo mwenye dhamana na sanaa.

"Dudubaya ameruhusiwa kuendelea na shughuli za Sanaa kwa sharti la kuwa chini ya uangalizi wa Basata kwa muda wa miezi sita na endapo ataendelea na tabia yake ya uvunjifu wa maadili atafutiwa usajili wake na msamaha wake tajwa uliotolewa.

Taarifa hiyo iliyopo kwenye ukurasa wa Instagram wa baraza hilo, imesema" Dudubaya atatakiwa kuzingatia maadili katika kazi zake za Sanaa,ikiwa ni pamoja na kuacha tabia yake ya kutumia lugha ya matusi,kashifa na maneno yanayochochea chuki miongoni mwa jamii,".

Pia imesema katika kipindi chote cha matazamio Basata litakuwa inafuatilia kwa karibu mwenendo wake ili kujiridhisha kama anazingatia maelekezo na masharti aliyopewa.

Aprili 14, 2020 Basata ilimfutia usajili wa kazi za Sanaa msanii Godfrey Tumaini pamoja na cheti chake cha usajili chenye namba BST.2164 kutokana na tabia zake za utovu wa nidhamu na uvunjifu wa maadili.

Aidha na Basata imetumia nafasi hiyo kuwataka wasanii wote kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Sekta ya Sanaa nchini.