Dk Abbas: Wasanii acheni kiki

Thursday June 02 2022
abas pic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Katibu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi amewataka wasanii kuwekeza kwenye maisha ya ukweli na sio ya kiki

Dk Abbas ameyasema hao leo Alhamisi Juni 2, 2022 akifungua mafunzo ya siku moja kwa wasanii chipukizi wa tasnia ya filamu jinsi ya kujiandaa na maisha ya ustaa.

Dk Abbasi amesema baadhi ya wasanii wamekuwa wakiishi maisha yasiyo ya kweli na mwisho wake huja kuabika vibaya haswa pale wanapopatwa na matatizo ikiwemo kuugua na kuanza kupitishiwa bakuli.

"Hatukatai kwamba ukifanya mendeleo kuonyesha watu kuwa umefanya kama moja ya kujenga hamasa kwa wengine,lakini sio ndio utumie kama mwanya kudanganya jamii kuwa una maisha fulani mazuri kumbe hakuna ukweli wowote ni kik tu ya kutafuta umaarufu halafu unapopata tatizo watu wanarudi nyuma kukusaidia kutokana na maisha yako uliyokuwa unawahadaa mitandaoni," amesema Katibu huyo.

Wakati kuhusu mafunzo hayo, amesema yamekuja wakati muafaka ambapo tasnia hiyo imekuwa ni ajira kwa vijana wengi lakini wengine wamejikuta wakilewa ustaa na kufanya mambo ya ajabu huku wakisahau kwamba watu wanatamani kuwa kama wao.

"Wasanii mnapaswa kuelewa kwamba kuna kamba nyembamba sana kati ya kazi mnayoifanyana maisha yenu halisi,hivyo kwa kufanya yasiyo yanaweza kuharibu sifa ya jina lako na jamii kwa ujumla ambayo inakuangalia kama kioo chake," amesema.

Advertisement

Aidha katika maisha yao ya kuelekea kuwa wasanii wakubwa,amewataka wasanii hao kuzingatia suala zima la maadili na kuepusha watu kuzima TV au kufumba macho pale wanapoangalia kazi zao.

"Tengenezeni movie zenye hadithi ya maisha halisi ya watu na sio kuja kuwa kero kwa wanaotazama na hata kama ni mavazi ya beach sio ndio uigize kama msanii aliyeko Miami kule Marekani kwani sisi tuna maadili yetu," amesema Dk Abbasi.


Awali,Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu,Dk Kiagho Kilonzo,amesema mafunzo hayo ni katika programu zao za kuwajengea uwezo wasanii wanaoingia kwenye kuwanda cha filamu.


Dk Kilonzo amesema mafunzo hayo wanayoyatoa kwa makundi, yataendeshwa mwaka mzima,lengo likiwa kumfikia kila msanii mchanga ili kujiandaa kuishi maisha ya ustaa hapo baadaye.


Kwa upande wao wasanii akiwemo Catherine Cledo na Ramadhan Lugendo, wamesema kupitia mafunzo hayo wamejifunza mengi ikiwemo kuhakikisha wanaishi katika ndoto zo na kuzitimiza.


Pia jingine ni kutakiwa kufanya kazi kama timu na kikubwa kilichowafurahisha ni kukutana na wasanii ambao tayari wamefanikiwa kwenye tasnia hiyo ambao wanaamini kwa namna moja au nyingine watakuwa viongozi wao wazuri wakuwaelekeza pale watakapoona wanapotoka na kuzidi kuwapa moyo pale watakapopatia.

Mwisho.

Advertisement