Diamond kuwania tena tuzo BET

Muktasari:

  • Kwa mara ya tatu msanii wa Bongofleva, Diamond Platnumz amechanguliwa kuwania tuzo za BET 2021 katika kipengele cha ‘Best International Act’ zitakazotolewa Juni 28, 2021.

Dar es Salaam. Kwa mara ya tatu msanii wa Bongofleva, Diamond Platnumz amechanguliwa kuwania tuzo za BET 2021 katika kipengele cha ‘Best International Act’ zitakazotolewa Juni 28, 2021.

Diamond anachuana na Wizkid, Burna Boy, Emicida, Headie, Aya Nakamura, Youssoupha na Young T & Bugsey.

Mwaka 2014 Diamond alitajwa kwa mara ya kwanza kuwania tuzo hizo na kuwa msanii wa kwanza Tanzania kufikia hatua hiyo. Aliwania kipengele Best International Act Africa lakini ushindi ulikuja kwenda kwa Davido wa Nigeria.

Mwaka 2016, Diamond  akatajwa tena kuwania kipengele hichohicho huku washindani wake wakiwa ni Wizkid, Yemi Alade, AKA, Cassper Nyovest na Black Koffie ambaye ndiye alitangazwa kuwa mshindi.

Baada ya kutochaguliwa kuwania BET 2017, Diamond akizungumza katika kipindi cha XXL cha Clouds FM, Juni 21, 2017 alisema lazima mwaka 2018 atachaguliwa kwani 2017 alishindwa kwa kuwa alikuwa na kazi ya kuwasimamia wasanii wa WCB Wasafi hivyo hakufanya nyimbo nyingi kubwa.

Licha ya matumaini hayo makubwa Diamond alijikuta akizikosa tuzo hizo mwaka 2018 na miaka iliyofuatia hadi mwaka 2021 alipotajwa tena.

Ikiwa atanyakua tuzo hiyo Diamond atakuwa msanii wa pili Tanzania kufanya hivyo baada ya Rayvanny ambaye aliishinda Juni 25, 2017 katika kipengele cha 'Viewer’s Choice Best New International Act' baada ya kuwabwaga wasanii kama Dave, Amanda Black, Changmo, Daniel Caesar, Remi na Skip Marley.

2001 na huandaliwa na kituo cha TV cha Black Entertainment Television, lengo la kuanzishwa kwake ni kusherehekea mafanikio ya kazi za Wamarekani weusi katika sanaa ya muziki, uigizaji, michezo mengineo hasa upande burudani.


Imeandikwa na Peter Akaro, Mwananchi