Diamond akutanisha watoto wake, Zari aikubali

Muktasari:

  • Watoto hao ni Latifa Neseeb ’Tiffah,’ Nilan Naseeb aliozaa na mjasiriamli maarufu Zarina Hassan ’Zari’ pamoja na Naseeb Junior ambaye amezaa na msanii wa muziki na mtangazaji kutoka nchini Kenya, Tanasha Dona.

Dar es Salaam. Msanii maarufu nchini, Naseeb Abdul ’Diamond Platnumz,’ amewakutanisha kwa mara ya kwanza watoto wake ambao amewapata kutoka kwa mama wawili tofauti.

Watoto hao ni Latifa Neseeb ’Tiffah,’ Nilan Naseeb aliozaa na mjasiriamli maarufu Zarina Hassan ’Zari’ pamoja na Naseeb Junior ambaye amezaa na msanii wa muziki na mtangazaji kutoka nchini Kenya, Tanasha Dona.

Diamond na watoto wake hao wameonekana leo Ijumaa Oktoba 20, 2023 katika video fupi kwenye ukurasa wa kijamii wa Instagram wa mtoto wake Tiffah.

Diamond ameonekana yupo kwenye gari la kifahari (Cadillac Escalade Sky Captain) akiwa na watoto hao pamoja na bibi yao, Sanura maarufu kwa jina la mama Dangote.

Wanne hao wakiwa ndani ya gari hiyo wameonekana wakiwa wote wamevamilia nguo nyeupe, ambapo Diamond alikuwa amembeba Naseeb Juniour na pembeni ya kiti chake akiwa amekaa Tiffah ambaye alikuwa akichezea Ipad.

Wakati Nilan yeye alikuwa amekaa kiti cha pembeni na bibi yake akiwa anachezea simu janja ndogo.

Baadhi ya watu waliona video hiyo, wameonekana kuifurahi akiwemo Fatma Lugongo aliyeandika ’Furahia muda wako na familia Tiffa.”

Katika kuonyesha kuwa Zari naye amependa jambo hilo, ambalo ni wakati mzuri kwa kifamilia, aliiweka video hiyo kwenye ukarasa wa Tiffah ambao yeye ndiyo anausimamia.

Wadadisi wa mambo pia wanadhani itakuwa Zari ndiye aliyeirekodi video hiyo kutokana na ukweli kwamba hapendi kuwa mbali watoto kila wanapokuja kwa baba yao Tanzania.