Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Davido anavyoiheshimisha Bongofleva duniani

Muktasari:

  • Licha ya hilo, Davido anaipa heshima kubwa Bongofleva kwa kufanya kazi na wasanii wake, na kwa Afrika Mashariki, ni Tanzania pekee iliyonufaika zaidi na kipaji cha mkali huyo wa kibao cha Unavailable (2023).

MKALI wa Afrobeats kutokea Nigeria, Davido ni mwanamuziki mwenye nguvu kubwa ya ushawishi bara Afrika kutokana na sanaa yake na mtindo wake wa maisha unaochochewa na utajiri wake na familia yake kwa ujumla.

Licha ya hilo, Davido anaipa heshima kubwa Bongofleva kwa kufanya kazi na wasanii wake, na kwa Afrika Mashariki, ni Tanzania pekee iliyonufaika zaidi na kipaji cha mkali huyo wa kibao cha Unavailable (2023).

Ikumbukwe Davido alianza muziki katika kundi la KB International nchini Marekani, alipata umaarufu alipoachia wimbo wake, Dami Duro (2011) ambao ni wa pili kutoka kwa albamu yake ya kwanza, Omo Baba Olowo.

DAVI 04

Ukubwa wake Afrika uliongezeka baada ya mwaka 2016 kusaini mkataba na lebo ya Sony Music, kisha miezi michache baadaye kuanzisha lebo yake, Davido Music Worldwide (DMW) na kuwasaini Dremo na Mayorkun.

Baadaye alirekebisha mkataba na Sony Music na kutoa nyimbo tano ukiwamo Fall (2017) ambao ulikuwa wimbo wa kwanza Nigeria kukaa kwa muda mrefu zaidi chati ya Billboard. Je, huku kwenye Bongofleva Davido kafanya nini?.

DAVI 01

Diamond Platnumz & Davido

Baada ya Davido kuja Bongo katika tamasha la Fiesta 2013, ndipo Diamond akarekodi na staa huyo ngoma yake, My Number One Remix (2013) baada ya kusaidiwa na Sallam SK ambaye wakati huo hakuwa meneja wa Diamond.

Kwa bahati nzuri, My Number One Remix (2013) ndio ukawa wimbo ya kwanza kumtangaza Diamond kimataifa ambapo kwa mara ya kwanza aliwania tuzo za MTV MAMAs (2014) kama Msanii Bora wa Kiume na Wimbo Bora wa Kushirikiana.

Sasa kufutia mafanikio ya mradi huo, ndipo Diamond akamuomba Sallam SK awe meneja wake rasmi, ombi ambalo lilikubaliwa na hadi sasa wanafanya kazi pamoja.

Baada ya Davido, Diamond ameweza kushirikiana na wasanii wengine wa Nigeria kama kama P-Square, Iyanya, Mr. Flavour,  Adekunle Gold, Teni, Tiwa Savage na Rema, mshindi wa MTV VMAs  2023.

DAVI 03

Joh Makini & Davido

Rapa huyu kutoka makundi ya River Camp Soldiers na Weusi, alimshirikisha Davido katika ngoma yake, Kata Leta (2017) iliyotayarishwa na Nahreel kutokea The Industry ila video yake ilifanyika Afrika Kusini. 

Kwa mujibu wa Joh Makini, Davido ndiye aliyeomba wafanye kolabo hiyo kupitia mtandao wa X, zamani Twitter, ndipo wakapanga na kurekodi kisha wakakutana Afrika Kusini walipomalizia kurekodi.

Davido alikuwa msanii wa pili kutokea Nigeria kushirikishwa na Joh Makini ambaye awali alitoa ngoma na Chidinma, Perfect Comb (2016), kolabo iliyokuja baada ya kukutana Nairobi, Kenya kwenye msimu wa nne wa Coke Studio Africa.

Joh Makini, mshindi wa TMA kama Msanii Bora wa Hip Hop 2012, alitoka kimuziki na wimbo wake, Chochote Popote (2006) uliotengenezwa na Dunga wa Mandugu Digital, huku ukijumuishwa katika albamu yake ya kwanza, Zamu Yangu (2007).

DAVI 02

Dayna Nyange & Davido

Mwimbaji huyu aliyeanza kupata umaarufu kupitia nyimbo zake kama Mafungu (2009) na Nivute Kwako (2011), alisafiri hadi Nigeria ili tu kurekodi na Davido na hata video ya wimbo huo ilifanyika huko huko.

Wawili hao walitoa wimbo uitwao Elo (2021) ambao pia ulibeba jina la Extended Playlist (EP) ya kwanza yake Dayna, mshindi wa tuzo mbili za BEA 2017 kutokea Nigeria.

Ikumbukwe Dayna kabla ya kujikita katika muziki, aliwahi kushiriki mashindano ya urembo, Miss Dodoma na kushika nafasi ya nne, akiwa ni sawa na Lulu Diva ambaye alishinda Miss Kiba kisha Miss Pwani.

Na kipindi anaanza muziki, Dayna alikuwa akifanya rap na sio kuimba kama ilivyo sasa, hiyo ni baada ya rapa kutoka kundi la Weusi, Nikki wa Pili ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, kumshauri kuachana na rap badala yake aanze kuimba.