Praise Wisdom aibuka mshindi wa BBS 2026
Muktasari:
- Fainali hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Haddy Pro HQ uliopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, ilisisimua zaidi baada ya hatua ya nne bora kukutanisha washiriki wanawake pekee.
MASHINDANO ya kusaka vipaji yaliyopewa jina la Bongo Star Search (BBS) awamu ya 16, yametamatika usiku wa kuamkia Jumapili Julai 12, 2026, huku mshiriki Praise Wisdom kutoka nchini Uganda akiibuka kidedea na kufanikiwa kuondoka na zawadi ya gari jipya aina ya Mazda CX-3 pamoja na kitita cha Sh50 milioni kutoka Benki ya CRDB.
Fainali hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Haddy Pro HQ uliopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, ilisisimua zaidi baada ya hatua ya nne bora kukutanisha washiriki wanawake pekee.
Katika fainali hiyo, nafasi ya pili ilishikwa na Sophia Benson ‘Sofire’ kutoka mkoani Morogoro, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Summerellah wa Dodoma na nafasi ya nne ikishikiliwa na Freya kutoka DR Congo.
Akizungumza wakati wa kutoa zawadi hizo, Mkurugenzi wa BSS, Ritha Paulsen ‘Madam Ritha’, aliwapongeza washiriki wote waliofanikiwa kuingia hatua ya 10 bora, huku akiwataka vijana waende BBS kujaribu bahati zao.
“Vijana wale wa nyumbani wajue vipaji vyao vina nguvu, hivyo wanaweza kuja Bongo Star Search kujaribu bahati zao kwani inawezekana kabisa kuendeleza na kukuza kipaji kupitia mashindano haya,” amesemaRitha.
Baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Praise Wisdom alionyesha hisia zake na kuushukuru uongozi wa BBS kwa nafasi hiyo, akieleza kuwa safari yake haikuwa nyepesi tangu mwanzo.
“Nashukuru sana kwa kuibuka mshindi wa msimu huu, haikuwa safari rahisi hata kidogo, ushindani ulikuwa mkubwa na kila mmoja alikuwa na talanta ya pekee.
“Ushindi huu ni mwanzo mpya wa safari yangu ya sanaa na ninawaahidi mashabiki wangu nitafika mbali kimuziki sitawaangusha,” amesemaPraise.
Fainali hiyo iliyoanza na jumla ya washiriki 10. Katika mchujo wa kwanza, washiriki wawili waliondolewa na kubaki wanane.
Raundi ya pili ilishuhudia washiriki wengine watatu wakifungishwa virago, na kuacha watano pekee waliopambana kuingia hatua ya mwisho.
KAULI ZA WASHIRIKI WALIOTOLEWA
Zakasoul, ambaye alitolewa kabla ya fainali ya nne bora, amesemakutoshinda kwake hakumfanyi akate tamaa kwani BBS imemfungulia milango mingi.
“Sio mbaya kwa mimi kutoshinda kwani mwisho wa siku mshindi ni mmoja na asiyekubali kushindwa sio mshindani.
“Hata hii hatua niliyofikia namshukuru Mungu, kuna vitu vingi nimevipata ikiwemo kuongezeka kwa mashabiki kwenye mitandao yangu ya kijamii. Nawaahidi kuwa msanii mkubwa hapa nchini na nje ya nchi,” amesemaZakasoul.
Naye Bela, ambaye safari yake iliishia raundi ya kwanza, alishukuru kwa fursa hiyo akisema: “Ndio mashindano yalivyo, lazima apatikane bingwa mmoja tu, nawashukuru BBS kwa kunipa nafasi na nawatakia mashindano mema wale waliobaki.”
Kwa upande wake, Joshua Gully, mshiriki kutoka Jamhuri ya DR Congo, aliwashukuru waandaaji kwa kumpa marafiki wapya na uzoefu mkubwa, akiahidi kufanya vizuri zaidi katika tasnia ya burudani hapo baadaye.
Msimu huu wa 16 wa Bongo Star Search umetoa zawadi nono na viwanja kwa washindi wa nafasi mbalimbali. Kwenye upande wa uchekeshaji, Wadrama ameibuka kidedea na kujinyakulia Sh5 milioni huku kikundi cha madansa cha Terial Vision kutoka Buza jijini Dar es Salaam kikiondoka na kiasi cha Sh10 milioni.