Dakika 10 na Lamata, ijue siri uandishi wa filamu zake

Muktasari:
- Uandishi wa miswada inayogusa maisha halisi ya Mtanzania wa kawaida, moja ya siri ya mafanikio kwa mshindi wa tuzo za uandishi bora wa hadithi na tamthilia nchini, Leah Mwendamseke ‘Lamata’.
Dar es Salaam. Mshindi wa tuzo ya uandishi bora wa miswada ya filamu na tamthilia nchini, Leah Mwendamseke ‘Lamata’ amesema mashabiki wamekuwa wakishindwa kutabiri mwendelezo wa kazi zake kwa kuwa aina ya uandishi wake ni ya kupindisha simulizi.
Lamata amesema hayo Januari 24, 2024 alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi Digital, kuhusu tawi ‘scene’ inayotoa uelewa na elimu kuhusu kinga na tiba ya saratani iliyopo ndani ya tamthiliya maarufu ya Juakali.
“Watu hawawezi kubeti kazi zangu, uandishi wangu naupindisha, Watanzania wengi wamezoea stori ambazo wanazijua kwamba kikitokea hiki, kitatokea kile wanachokihisi,” amesema na kuongeza:
“Mwandishi bora ni yule ambaye wanachokifikiria itakuwa hivi inakua tofauti, hiyo ndiyo maana ya mwandishi kufaulu. Ukiona maoni ya mashabiki ujue umefaulu, wengi wanasema uandishi wa filamu wa Lamata huwezi kubeti. Ndiyo ni kwa sababu wewe utakachowaza huwezi kwenda sawa na mimi.”
Lamata ambaye amewahi kutamba pia na tamthiliya ya Kapuni, amesema waandishi wengi wamekuwa wakitengeneza miswada inayofanana na yenye matukio yaleyale.
“Huwezi kutengeneza kila kitu kuhusu uchawi, sijui kama wenzangu mmewahi kuona uchawi ni vitu vya kufikirika, kusikika kuona kwenye runinga na huwezi kuona kwa macho vikifanyika,” amesema.
Lamata ametoa wito kwa waandishi kupenda kuandika miswada yenye maisha ya uhalisia, kwani nchi ina historia nyingi kabla ya uhuru na wengi hawazijui.
Amesema ni vema kutumia maisha ya kawaida katika kutoa mafunzo, kwani wasanii pia lazima waonyeshe mchango wao kwa jamii kwa kuandika miswada inayoigusa moja kwa moja.
“Ndiyo kama mimi, tamthiliya imependwa kwa kuwa kila tawi nililotengeneza mtu linamgusa. Stori ikianza kunigusa kama mwandishi moja kwa moja nikienda kwenye timu nawashauri hii stori kwa nini tusiingize hiki na kile inawagusa watu wengi wanashauri tunaifanya, kwa hiyo kinakuwa kitu ambacho tunakiandaa na tunaona kina ubora tunakifanyia kazi,” amesema.
Lamata ameongeza, “Kweli mimi ni mwandishi lakini pia ni kama mchungaji, mhubiri ni kama mwalimu nafanya kazi ya uandishi, lakini nafundisha ukweli.”
Kuhusu Wanyakyusa, Lamata amesema ameingiza stori ya kweli katika maisha ya kabila husika ambalo limeuvaa uhalisia.
“Wanyakyusa ni kabila ambalo nalijua, nimezaliwa, nimekulia na kusoma huko na mimi si Mnyakyusa mama na baba yangu ni Wabena wa Njombe na huko ndiyo kwetu,” amesema.
Amesema, “Wanyakyusa wamenilea, wengi wanasema mimi Mnyakyusa, huwa nami najihisi hivyo, ukiniambia kuhusu Kibena sikijui hata kukiongea lakini Kinyakyusa naweza kuongea na ninakisikia pia. Ni kabila ambalo nililisoma vizuri na ninalijua, linafurahisha nikaona kama linanifurahisha ni stori itakayopendwa na suala la ukabila tuliliingiza ili kunogesha.”
Minong’ono iliyopo miongoni mwa wasanii ni kuwa ‘Lamata mkali’ kauli hii imekuwa ikizungumzwa mara kwa mara, lakini mwenyewe amejibu:
“Nikwambie kitu, hata shule usipokuwa mkali wanafunzi watakusumbua tu. Mimi si mkali kila mahali, natengeneza kitu kizuri lazima utakuwa mkali watu nimewatengeneza kuanzia chini, ili nifikie malengo lazima niwe mkali.
“Huwezi kuja kwenye njia za Lamata ukafanya utakavyo, lazima utulie. Wenzako wote wanafika lokesheni saa mbili wewe unafika saa nane, kuanzia saa mbili watu wote 15 wakae ufike wewe saa nane wanakusubiri kesho huwezi kurudia,” amesema.
Kuhusu kufanya kazi na wasanii wa nje, Lamata amesema ni gharama kubwa lakini kwake anasoma na yuko darasani.
“Unapoleta watu kutoka nje wanakuja kukufundisha kuanzia adabu, ufanyaji wa kazi, usomaji wa muswada, kucheza na hata kuigiza. Mimi kuita watu waje ndani tunakuza soko letu twende kimataifa,” amesema Lamata.