D Voice atakaa kwenye chati wiki 100 kama Zuchu?

Mwimbaji mpya wa WCB Wasafi, D Voice ana kibarua kizito mbele ya mtangulizi wake ndani ya lebo hiyo, Zuchu kutokana na mafanikio na rekodi zake alizoweka muda mfupi baada ya kutambulishwa miaka mitatu iliyopita.
D Voice tayari ametoa albamu yake ya kwanza, Swahili Kid (2023) yenye nyimbo 10 alizowashirikisha Diamond Platnumz, Lava Lava, Mbosso na Zuchu aliyesikika katika nyimbo mbili, BamBam na Nimezama.
Utakumbuka hadi sasa WCB Wasafi imeshawasaini wasaniii kama Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Mbosso (2018), Zuchu (2020) na D Voice (2023).
D Voice aliyetambulishwa hapo Novemba 2023 anaendelea kufanya vizuri na albamu yake, Swahili Kid ambayo imefikisha 'streams' milioni 18.2 Boomplay, huku akiwa ametoa video za nyimbo tano kati ya 10 za albamu hiyo.
Hata hivyo, mafanikio ya Zuchu kimuziki wanapelekea mashabiki kuwa na shauku ya kutaka kuona kama D Voice naye ataweza kufika huko kwa muda ule ule, hiki ndicho kibarua alichonacho kwa sasa. Je, Zuchu alifanya nini hasa?.
Kwanza EP iliyomtambulisha, I A Zuchu (2020) akiwashirikisha Khadija Kopa na Mbosso ilifanya vizuri, mathalani ilikaa tano bora kwenye chati za Boomplay Album kwa wiki 75, huku ukishika namba moja kwa wiki 35.
Muziki wake ulimfanya Zuchu kukuwepo katika chati za YouTube Music Tanzania kwa wiki zaidi ya 100 na ndiye msanii wa kike Bongo aliyekaa kwenye chati hizo kwa muda mrefu zaidi.
Utakumbuka ndiye msanii wa kwanza wa kike Afrika kufikisha wafuasi (subscribers) 100,000 YouTube kwa wiki mmoja, na wafuasi milioni 1 Instagram kwa miezi mitano tu. Hiyo ya kwanza D Voice tayari ameikosa.
Vilevile ni wa kwanza Afrika Mashariki kupata wafuasi milioni 1 YouTube kwa mwaka mmoja, msanii wa kwanza wa kike Tanzania kupata watazamaji (views) milioni 100 YouTube, na kwanza wa kike kupata wasikilizaji (streams) milioni 100 Boomplay.
Zuchu alishinda tuzo yake ya kwanza kutoka African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2020 kama Msanii Bora Chipukizi akiwa ni msanii wa pili ya WCB kufanya hivyo baada ya Harmonize mwaka 2016. Je, D Voice ataweza?.