Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bado saa moja tu, mbivu mbichi sakata la Ibraah, Harmonize ijulikane

Muktasari:

  • Awali, wasanii hao waliitwa Jumatatu, lakini ni Ibraah pekee aliyefika katika ofisi hizo, huku Harmonize akituma mwanasheria wake, lakini haikuwekwa bayana kilichoendelea kwa vile Ibraah alidai amezuiwa kuzungumza kabla ya leo kuitwa tena Basata.

Lile sakata la msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ibraah kudai kutakiwa kulipa Sh1 bilioni ili aondoke katika lebo ya muziki ya Konde Gang inayomilikiwa na msanii Harmonize, litajulikana mchana wa leo wakati shauri hilo litakaposikilizwa katika ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Awali, wasanii hao waliitwa Jumatatu, lakini ni Ibraah pekee aliyefika katika ofisi hizo, huku Harmonize akituma mwanasheria wake, lakini haikuwekwa bayana kilichoendelea kwa vile Ibraah alidai amezuiwa kuzungumza kabla ya leo kuitwa tena Basata.

Mwanaspoti limeshafika eneo la tukio na kuzungumza na Mwanasheria wa BASATA Christopher Kamugisha, aliyesema wameshawasiliana na pande zote mbili na kwamba leo saa 7 mchana wanatakiwa kufika kwa ajili ya kusikilizwa, ikiwa na maana kuanzia sasa bado saa moja tu na ushei.

"Harmonize na Ibraah tuliwaita Jumatatu ya Mei 13, 2025 na walikuja ambapo Harmonize aliwakilishwa na mwanasheria wake, huku Ibraah alifika sambamba na mwanasheria wake pia," amesema Kamugisha na kuongeza;

"Tuliongea nao na tukawapangia leo Jumatano saa 7 mchana wafike wote wakiwa na wanasheria wao, kwa maana ya Harmonize afike na mwanasheria wake na Ibraah kadhalika, sisi kama walezi wa wasanii tunataka haya mambo yaishe na kila mmoja apate haki yake."

Uamuzi wa BASATA kuwaita Harmonize na Ibraah umekuja baada ya uongozi wa Kampuni ya Harmonize Ent. Ltd kupitia Lebo ya Konde Gang Music Worldwide, kutangaza Mei 12, 2025 kumsimamisha rasmi msanii Ibrahim Abdallah Nampunga 'Ibraah', kutoa na kushiriki katika shughuli zozote za muziki kama ilivyoainishwa katika mkataba na lebo hadi pale suala lake litakapopatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa mujibu wa mkataba na sheria za Tanzania. Hii ilitokana na Ibraah kutoa machapisho ambayo lebo hiyo inaona yanamvunjia heshima Harmonize ambaye ni bosi wa Konde Gang.

Lebo hiyo imempiga pia marufuku Ibraah kuchapisha, kutamka, au kufanya mawasiliano yoyote kuhusu suala hili kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii kama vile Instagram, WhatsApp, Facebook, na sehemu nyingine ikiwemo pamoja na mawasiliano ya aina yoyote ambayo yanaweza kuharibu taswira ya lebo au kumdhalilisha mkurugenzi muwekezaji wa lebo hiyo.

Hata hivyo, Ibraah ameonyesha kukaidi taarifa hiyo ya uongozi huo wa Konde Gang kwa kuendelea kuposti kazi katika akaunti yake ya mtandao wa Instagram.