Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Christian Bella na miaka 20 ya ‘Asante Tanzania’

BELLA Pict

Muktasari:

  • Safari ya Bella haikuwa ya mkato mfupi. Akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), alianza muziki hapa Tanzania, hatua kubwa ikiwa kujiunga na bendi ya Akudo Impact, ambako alijijengea msingi imara wa uimbaji na nidhamu ya jukwaani.

MWANAMUZIKI wa dansi mwenye sauti ya kipekee, Christian Bella ‘CBO’, ameandaa tamasha la kihistoria la ‘Asante Tanzania’ litakalofanyika Mei 8, 2026 katika Ukumbi wa Mlimani City,i Dar es Salaam, kusherehekea miaka 20 ya safari yake ya muziki nchini, iliyoambatana na kupewa uraia wa taifa hili.

Katika mazungumzo yake na Mwanaspoti, Bella anasema tamasha hilo silo la kawaida, bali ni la kipekee lililobeba hisia, historia na shukrani za dhati kwa mashabiki pamoja na Serikali iliyomkabidhi uraia, Desemba 18, 2025.

“Hili si tamasha la kawaida, ni siku ya kusema ‘Asante Tanzania’ kwa moyo wangu wote. Nimeishi hapa, nimekulia hapa kisanaa, nimejifunza hapa, na leo hii ninajivunia kuwa Mtanzania kamili,” anasema Bella.

BEL 01

Kutoka Akudo hadi kileleni

Safari ya Bella haikuwa ya mkato mfupi. Akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), alianza muziki hapa Tanzania, hatua kubwa ikiwa kujiunga na bendi ya Akudo Impact, ambako alijijengea msingi imara wa uimbaji na nidhamu ya jukwaani.

Ndani ya Akudo Impact, Bella alijifunza mbinu za muziki wa dansi wa Kikongo na Kiswahili, na kuanza kuvutia mashabiki kutokana na sauti yake yenye hisia na uwezo wa kulitawala jukwaa.

“Akudo ilinilea kisanaa. Nilijifunza kuheshimu kazi, kuheshimu jukwaa na kuwapa mashabiki kile wanachostahili. Hapo ndipo nilipoanza kuelewa kuwa muziki ni maisha, si kazi tu,” amesema.

Baadaye, Bella aliamua kujitegemea kwa kuanzisha bendi yake binafsi ya Malaika Band, hatua iliyompa uhuru wa kuonyesha ubunifu wake kikamilifu.

“Kuanzisha Malaika Band ilikuwa ndoto yangu kubwa. Nilitaka kuwa na jukwaa langu, sauti yangu na maamuzi yangu. Haikuwa rahisi, lakini nilijua ipo siku itafanikiwa,” amesema.

BEL 02

Nyimbo zilizogusa mioyo ya wengi

Katika miaka 20 ya muziki, Bella ametoa nyimbo nyingi zilizogusa maisha ya watu, huku baadhi zikibaki kuwa alama ya mapenzi, maisha na familia.

Miongoni mwa nyimbo zake zilizotikisa ni ‘Nani Kama Mama’, ‘Nashindwa’, ‘Nisamehe’, ‘Nakuhitaji’, ‘Mapenzi Yako Wapi?’, ‘Rudi’, ‘Usilie’, ‘Nagharamia’ na zingine nyingi.

Mwanamuziki huyo anasema wimbo wa ‘Nani Kama Mama’ una nafasi ya kipekee moyoni mwake kutokana na ujumbe wake wa upendo na heshima kwa mama.

“Kila nikisimama jukwaani kuimba wimbo wa ‘Nani Kama Mama’, siimbi tu. Bali naona machozi ya mashabiki, nawakumbuka wazazi wangu, na nahisi nguvu ya upendo wa kweli,” anasema.

BEL 03

Bella anavyouwasha moto

Bella anatajwa kuwa mmoja wa wasanii wachache wa dansi wenye uwezo mkubwa wa kutawala jukwaa kwa muda mrefu bila kuwachosha mashabiki.

Katika hilo anasema, “siri yangu ni kuimba kwa hisia na kuwasiliana moja kwa moja na mashabiki. Jukwaani mimi siendi kuimba tu, naenda kuzungumza na watu kupitia muziki, nawaangalia, nawaskiliza, na wanarudisha nguvu hiyo hiyo. Hapo ndipo uchawi wa muziki unapotokea, na nikipanda jukwaani huwa sishuki hadi nimalize shoo.”

BEL 04

Kuhusu uraia, ‘asante Tanzania’

Kupata uraia wa Tanzania 2025 ilikuwa hatua muhimu katika maisha ya Bella baada ya kuishi nchini kwa miaka 20 akichangia kukuza muziki wa dansi.

Mwanamuziki huyo anasema kitendo hicho kilimfanya ajione kama amezaliwa upya masihani mwake.

“Nilipokabidhiwa uraia nilihisi kama nimezaliwa upya. Tanzania si sehemu tu ya kazi yangu, ni nyumbani kwangu,” anasema.

Mkali huyo wa dansi pia anazungumzia tamasha lake ambalo limepewa jina la ‘Asante Tanzania’ na nini mashabiki wakitarajie kupitia tukio hilo.

Kwa mujibu wa Bella, tamasha hilo litakalofanyika Mlimani City linatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya burudani mwaka huu.

Bella anasema: “Nataka iwe shoo ya kimataifa. Kila kitu kuanzia sauti, taa hadi performance iwe daraja la juu. Hii ni zawadi yangu kwa Watanzania.”

“Nitatoa kila kitu kuhusu muziki wangu jukwaani siku hiyo. Nataka kila mtu atakayekuja aondoke na kumbukumbu isiyofutika kichwani mwake.”

BEL 05

Shukrani kwa mashabiki

Bella hakusita kueleza kuwa mafanikio yake yote yametokana na mashabiki wake waliomsapoti kwa miaka yote.

“Mashabiki wangu wamekuwa nami kwenye kila hatua, wakati wa furaha na changamoto. Tamasha hili ni lao, ni kwa ajili yao,” amesema.