Cheka amchapa Kaoneka KO atoa onyo

Muktasari:

Baada ya ushindi huo, Cheka bingwa wa zamani wa dunia wa WBF atazichapa na bondia kutoka Cameroon baadae mwaka huu jijini Arusha.

Bondia Francis Cheka jana amewathibitishia mashabiki wake kuwa bado hajachuja ulingoni baada ya kumchapa Shaban Kaoneka kwa Knock Out (KO) na kuwa bingwa wa PST kwenye uzani wa juu mwepesi (light heavy).

Cheka ambaye hakuwahi kuonekana ulingoni tangu Desemba 26, 2018, amerejea kwa kasi na kuchomoza na ushindi huo katika raundi ya sita ya pambano lililokuwa la raundi 10.

Mashabiki waliojitokeza kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro  kumshuhudia Cheka akirejea ulingoni walimpongeza kwa kiwango alichokionyesha huku mwenyewe akitoa onyo kwa mabondia wa uzani wake kuwa wajipange.

"Mwenye nafasi yake kwenye uzani wa light heavy ndio nimerudi, hivyo waliokuwa wakitamba sasa wajipange," amesema Cheka muda mfupi baada ya pambano hilo.

Mabondia wanaopigania uzani huo namba moja ni Said Mbelwa, Ibrahim Maokola, Mbaruku Kheri, Japhet Kaseba,
Kaoneka, Hafidhi David na  Kassim Somboko.

Akizungumzia pambano na Kaoneka, Cheka alisema awali alitarajia ashinde raundi ya nne, lakini uwezo wa mpinzani wake alimkwamisha.

"Kama sio kutumia uzoefu, Kaoneka angeniadhiri, ni bondia mzuri na alinipa upinzani hasa raundi nne za mwanzo.

"Kona yangu ilimsoma na tulipomaliza raundi ya tano, ilinipa maelekezo ya ngumi gani nicheze, mbinu ile ilimzima Kaoneka," amesema Cheka.

Kaoneka bondia pekee aliyewahi kumchapa kwa KO Hassan Mwakinyo alikiri kuzidiwa mbinu lakini akaomba pambano la marudiano.