Chanzo cha bifu la Daz Nundaz na Solid Ground Family

Muktasari:
- Akiwa na miaka zaidi ya 20 katika muziki ameshaandika historia yake na muziki wake unaendelea kuishi katika nyoyo za mashabiki wake ambao amewapatia albamu mbili ‘Elimu Dunia na ‘Karibu Tanzania’. Fahamu zaidi.
KWA wakati wake Daz Baba alitengeneza nyimbo kubwa zilizofanya vizuri akiwa na kundi la Daz Nundaz na hata aliposimama pekee bado alizidi kuuwasha moto na hadi sasa ni miongoni mwa walioleta ladha ya tofauti katika muziki.
Akiwa na miaka zaidi ya 20 katika muziki ameshaandika historia yake na muziki wake unaendelea kuishi katika nyoyo za mashabiki wake ambao amewapatia albamu mbili ‘Elimu Dunia na ‘Karibu Tanzania’. Fahamu zaidi.
1. Wakati Daz Baba anaaanza muziki, miongoni mwa wasanii aliokuwa anawakubali sana ni pamoja na Missy Elliott kutokea Marekani, huyu anatajwa kama Malkia wa Rap akiwa ameshinda tuzo nne za Grammy na kuuza zaidi ya rekodi milioni 40 duniani kote.
2. Kundi lake la Daz Nundaz lilianza na wasanii watano tu ila baadaye walikuja kuongezeka wengine ambao waliunda makundi yao chini ya Daz Nundaz na kuwa kama familia moja, makundi hayo ni Sewa Side na Scout Jentaz.
3. Wimbo wa kwanza wa Daz Nundaz kuachia ni ‘Maji ya Shingo’ na ulitoka mwaka 1998 chini ya Miikka Mwamba ambaye pia alikuja kutengeneza nyimbo nyingine za kundi hilo ‘Kamanda’ na ‘Barua’ ambao pia P-Funk Majani alishiriki.
4. Ugomvi kati ya Daz Nundaz na Solid Ground Family uliibuka baada ya Solid Ground kurudia wimbo wa Ferooz uliokuwa bado haujatoka wala kurekodiwa rasmi ambao ulikuwa kwenye kanda (tape) aliyoipoteza Ferooz akiwa shule.
Wengi wanalikumbuka kundi la Solid Ground Family kwa nyimbo zao kama Bush Party, Mechi Kali, Asubuhi Mchana Usiku, Athumani, Kichaa, Happy Birthday n.k.
5. Daz Nundaz wanaamini wao ndio waliotambulisha muziki wa kuimba kwenye Bongo Fleva na sio Dully Sykes kupitia wimbo ‘Julieta’ kama inavyotajwa na wengi na hata msanii huyo.
Hoja ni wakati ‘Julieta’ inatoka, tayari Daz Nundaz walikuwa washatoa nyimbo kama ‘Kamanda’ na ‘Barua’ ambazo zilifanya vizuri zaidi.
6. Wimbo wake ‘Wife’ akimshirisha Albert Mangwair ndiyo ulikuwa wa kwanza kwa Daz Baba kutoa kama solo baada ya kufanya kazi na kundi la Daz Nundaz kwa muda mrefu na kutamba na nyimbo kama Maji ya Shingo, Barua, Kamanda n.k.
7. Daz Baba alikutana na Fid Q mkoani Arusha na ndipo akamuomba ashiriki katika wimbo wake ‘Namba Nane’ ila tayari alikuwa asharekodi wote lakini akaona awepo mtu wa rap ili kuleta ladha tofauti.
8. Mwana FA ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, anaamini mdundo wake bora wa Bongo Fleva kwa muda wote ni ule wa wimbo wa Daz Baba ‘Nipe Tano’ uliotengenezwa na P-Funk Majani.
9. Daz Baba alisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ili kumwomba Afande Sele ashiriki katika wimbo wake ‘Elimu Dunia’ ambao ndio umebeba jina la albamu yake ya kwanza. Afande Sele alikubali ombi hilo na mengine sasa ni historia.
10. Na albamu nzima ya kwanza ya Daz Baba, Elimu Dunia (2004) yenye nyimbo 10 ilirekodiwa Bongo Records kwa P-Funk Majani, albamu hiyo ilitoa nyimbo maarufu hadi sasa kama Wife, Nipe Tano, Namba Nane n.k.